pagead2.googlesyndication.com pagead2.googlesyndication.com

Sheikh Ponda, DPP kortini leo

Dar es Salaam. Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda leo anatarajiwa kuwa na kibarua kingine kigumu katika kupangua kigingi cha kufutiwa shtaka la kukaidi amri ya mahakama, alichowekewa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Sheikh Ponda kwa sasa anasota mahabusu kutokana na kesi ya jinai inayomkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro, akidaiwa kufanya makosa ya uchochezi katika maeneo mbalimbali mjini Morogoro na kukiuka amri ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
 Hata hivyo Ponda kupitia kwa Wakili wake Juma Nassoro, amewasilisha maombi ya marejeo, akiiomba Mahakama Kuu ifanye marejeo ya uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro kukataa maombi yake ya kumfutia shtaka hilo.
Maombi hayo yalitarajiwa kusikilizwa na Jaji Agustine Mwarija juma lililopita lakini yaligonga mwamba baada ya DPP kuwasilisha pingamizi mahakamani hapo akiiomba mahakama iyatupilie mbali maombi hayo, pamoja na mambo mengine akidai kuwa, yamewasilishwa kinyume cha sheria.
Kutokana na pingamizi hilo, Jaji Mwarija aliahirisha usikilizwaji wa maombi hayo ya msingi hadi leo kwa ajili ya kusikiliza pingamizi hilo la DPP.
Katika pingamizi hilo, DPP kupitia kwa Wakili wa Serikali, Bernard Kongola alidai kuwa maombi hayo yamewasilishwa kinyume na kifungu cha 372 (2) Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).
Alidai kwa mujibu wa kifungu hicho mtu haruhusiwi kuwasilisha ombi la marejeo ambayo yanatokana na uamuzi au amri ya mahakama ya chini ambayo haimalizi kesi.
Hii ni mara ya pili kwa Sheikh Ponda kuwasilisha mahakamani hapo maombi hayo baada ya Mahakama Kuu kuyatupilia mbali kutokana na pingamizi lililowekwa na DPP.
Maombi hayo ya kwanza yalitupiliwa mbali  na Jaji Rose Teemba,Desemba 11, 2013, baada ya DPP kumwekea pingamizi kuwa hati ya kiapo iliyokuwa ikiunga mkono maombi yake ilikuwa na kasoro za kisheria.
Credit, mwananchi

0 comments:

Post a Comment