pagead2.googlesyndication.com pagead2.googlesyndication.com
Showing posts with label politics. Show all posts
Showing posts with label politics. Show all posts

Chadema yalaumiwa kutumia tetemeko kisiasa


UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Mkoa wa Kagera umelalamikia kitendo kinachofanywa na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutumia janga la tetemeko la ardhi mjini hapa kufanya siasa na propaganda potofu.
Pia umoja huo umeitaka na kuishauri Serikali kuacha kazi ya uhakiki, ugawaji wa misaada yote kwa waathirika ifanywe na askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka alimueleza suala hilo Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Salum Kijuu, alipomtembelea ofisini kwake.
Alimweleza kuwa kinachofanywa na Chadema ni kituko na fedheha ya kisiasa. Alisema baadhi ya viongozi wa chama hicho wanatumia tetemeko hilo kujaribu kujijenga kisiasa huku wakiwabagua wanachama wa CCM kwa itikadi za kisiasa.
Alisema uhakiki na utoaji wa msaada katika awamu ya kwanza ulifanyika kukiwa na ubaguzi na upendeleo huku baadhi ya shehena za mizigo ya misaada na vifaa vya ujenzi ikiandikwa maneno “ukawa pamoja”.

Vitambulisho vya Taifa kutumika uchaguzi ujao

VITAMBULISHO vya Taifa huenda vikatumika katika Uchaguzi Mkuu ujao wa Rais, Wabunge na Madiwani.
Hayo yalisemwa jana na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Rose Mdami wakati akitoa maelezo kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai kwenye Ukumbi wa Pius Msekwa bungeni mjini hapa katika hafla ya kumkabidhi kiongozi huyo wa Bunge kitambulisho chake cha taifa.
Mdami alisema tayari mamlaka hiyo imechukua taarifa za wapigakura kutoka kwenye kanzidata ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na kuzichakata na kuna uwezekano mkubwa vitambulisho vya taifa vikatumika katika uchaguzi ujao na kuirahisishia kazi tume hiyo kufanikisha uchaguzi huo wa Rais, Wabunge na Madiwani.
"Vitambulisho tunavyovitoa sasa vina saini ya mtu husika, hivyo vitatumika benki. Tumewashirikisha pia NEC ambao wametupa 'database' (kanzidata) yao, tumezichakata na tunaendelea na taratibu ili ikiwezekana Vitambulisho vya Taifa vitumike katika Uchaguzi Mkuu wa 2020 badala ya vile vya tume," alisema Mdami.
Akishukuru, Ndugai aliipongeza mamlaka hiyo kwa kuwa na mipango mizuri, lakini akaishauri serikali kuweka sharti kuzilazimisha benki kutoruhusu mtu kufungua akaunti bila kuwa na kitambulisho cha taifa.
Spika pia alihoji sababu za Nida kuwa na vitambulisho vyenye rangi tatu tofauti na kujibiwa na Mdami kuwa kitambulisho cha kwanza ni cha raia mzawa, cha pili cha raia wa kigeni anayeishi nchi na cha mwisho kwa ajili ya wakimbizi.
"Kwa sasa si rahisi mkimbizi kujichanganya mitaani huko na kupatiwa kitambulisho cha taifa. Tunashirikiana na Tamisemi kuhakikisha hakuna udanganyifu tena. Mtu anayejaza fomu ya kupatiwa kitambulisho anatakiwa kupitia vipengele 72 ambavyo si rahisi kuvighushi kama si mzawa," alisema Mdami.

Ndulu: Hali ya uchumi inaridhisha


GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu amesema hali ya ukuaji wa uchumi nchini imeendelea kuwa ya kuridhisha na kwamba wastani wa mfumuko wa bei katika miezi sita ya kwanza ya mwaka huu umeendelea kushuka hadi kufikia asilimia 5.5 Juni mwaka huu na asilimia 4.9 Agosti 2016 kutoka asilimia 6.8 iyokuwapo Desemba 2015.
Aidha, amesema kupotea kwa fedha kunatokana na Serikali ya Awamu ya Tano kudhibiti makusanyo ya kodi, kuziba mianya mbalimbali ya upotevu wa fedha na kubana kazi zisizokuwa rasmi ‘misheni town’ na fedha hizo kuelekezwa kusaidia umma badala ya kwenda kwa wachache wanaojipatia isivyo halali.
Pia amesisitiza kuwa hakuna mdororo wa uchumi kwa kuwa ipo miradi mikubwa ya viwanda na miundombinu inayoendelea na inayotarajiwa kuanza kazi siku za usoni ambayo itachangia katika kuimarika kwa uchumi; hivyo kuweka takwimu sahihi tofauti na madai ya baadhi ya wanasiasa wa upinzani kuwa kuna mdororo wa uchumi.
Profesa Ndulu akitoa taarifa kuhusu hali ya uchumi wa Tanzania jana jijini Dar es Salaam, alisema katika robo ya kwanza ya mwaka 2016 ukuaji wa Pato la Taifa ulikadiriwa kuongezeka kwa asilimia 5.5 ikilinganishwa na asilimia 5.7 kipindi kama hicho mwaka jana.
Kadhalika alisema wastani wa mfumuko wa bei katika miezi sita ya kwanza ya mwaka 2016 umeendelea kuwa mzuri, ukiendelea kushuka hadi kufikia asilimia 5.5 Juni mwaka huu na asilimia 4.9 Agosti 2016 kutoka asilimia 6.8 Desemba mwaka jana.
Kuhusu hali ya ukuaji wa uchumi, alisema zipo shughuli mbalimbali zilizochangia ukuaji huo wa uchumi kwa kiasi kikubwa ikiwamo kilimo asilimia 11.7, biashara asilimia 10.6, uchukuzi asilimia 10.1, sekta ya fedha asilimia 10.1 na mawasiliano asilimia 10.0, sekta ya fedha asilimia 13.5, mawasiliano asilimia 13.4 na utawala wa umma asilimia 10.2.
Matazamio ya ukuaji wa uchumi 2016 Profesa Ndulu alisema kwa kuangalia viashiria mbalimbali inaonekana kuwa hali ya uchumi nchini itaendelea kuimarika katika mwaka 2016 na kuwa asilimia 7.2.
Alivitaja viashiria hivyo kuwa katika uzalishaji wa umeme, uzalishaji wa saruji, uzalishaji wa malighafi za viwandani, mauzo ya bidhaa za viwanda nje ya nchi, makusanyo ya kodi na mikopo itolewayo na mabenki ya biashara.
Alisisitiza kuwa hakuna mdororo wa uchumi kwa kuwa ipo miradi mikubwa ya viwanda na miundombinu inayoendelea na inayotarajiwa kuanza kazi siku za usoni ambayo itachangia katika kuimarika kwa uchumi.
Aliitaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni pamoja na ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa, ujenzi wa bomba la mafuta la Uganda ambalo litahusu vilevile upanuzi wa bandari ya Tanga, ujenzi wa eneo la kibiashara Kurasini itakayokuwa mhimili wa biashara kati ya China na ukanda wa Afrika.
Alisema miradi mingine ni ule wa kuzalisha megawati 240 za umeme wa Kinyerezi II, kupanua viwanja vya ndege nchini, ujenzi wa maghala ya Taifa ya kuhifadhi chakula yenye uwezo wa kuhifadhi tani 350, ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha saruji cha Dangote na ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza marumaru Mkuranga mkoani Pwani.
Miradi mingine ni ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha mbolea mkoani Lindi na kiwanda cha bidhaa za chuma mkoani Pwani ambacho kiko mbioni kukamilika. Alisema kwa miradi yote hiyo ni dhahiri kuwa hali ya uchumi nchini ni nzuri na inatoa matumaini makubwa kwamba shughuli halali za kiuchumi zinaendelea kama ilivyotarajiwa hapo awali.
Alisema lengo la ukuaji wa Pato la Taifa ni asilimia 7.2 kwa mwaka huu, na litafanikiwa, ambapo inachangiwa na ukweli kwamba Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga katika kuimarisha uchumi endelevu usiokuwa na mianya ya rushwa, usimamizi thabiti wa rasilimali za umma, ujenzi wa miundombinu bora kwa lengo la kujenga uchumi wa viwanda chini ya mpango wa maendeleo wa miaka mitano. Mwenendo wa mfumuko wa bei Mchumi huyo alisema kushuka kwa mfumuko wa bei kwa wastani kulichangiwa zaidi na bei zisizojumuisha bei za vyakula na nishati zikifuatiwa na zile za nishati na mafuta.
Alisema wastani wa mfumuko wa bei usiojumuisha bei za vyakula na nishati ambao ni kiashiria sahihi zaidi cha utekelezaji wa sera ya fedha, umeendelea kubaki katika viwango vya chini yaani,wastani wa asilimia 2.8 katika miezi sita ya mwanzo ya mwaka huu.
Alisema hali hiyo inatokana na hatua mbalimbali thabiti zilizochukuliwa za sera ya fedha na bajeti katika kudhibiti ujazi wa fedha na ukwasi katika uchumi.
Hata hivyo, alisema mfumuko wa bei utaendelea kubakia katika viwango vya tarakimu moja katika siku zijazo na kufikia lengo la muda wa kati ya asilimia tano ikitokana na matarajio ya hali nzuri ya hewa itakayochangia kupungua kwa kasi ya kuongezeka kwa bei za vyakula.
Kadhalika, alisema pamoja na ongezeko dogo la bei ya mafuta nchini inayotokana na mwenendo wa bei katika soko la dunia, utulivu wa thamani ya Shilingi, mwendelezo wa sera thabiti ya fedha, usimamizi mzuri wa mapato ya serikali na upatikanaji wa umeme utokanao na gesi utasaidia kupunguza gharama za uzalishaji viwandani.
Alisema hata hivyo, ni muhimu kuzingatia kuwa upungufu wa mavuno ya mazao ya chakula uliojitokeza kwa baadhi ya nchi za ukanda wa kusini mwa Afrika unaweza kusababisha shinikizo la mfumuko wa bei katika siku za usoni. Deni la Taifa Alisema kasi ya uongezekaji wa deni imepungua kwa sababu ukopaji nje ya nchi katika masoko ya kibiashara umepungua.
Hata hivyo, alisema deni la nje liliongezeka kwa asilimia 2.6 na kufikia Dola za Marekani milioni 16,281 Juni mwaka huu sawa na asilimia 77.8 ya deni la taifa kutoka Dola za Marekani milioni 15,864 Desemba mwaka jana.
Alisema kuongezeka kwa deni hilo kulitokana na kuongezeka kwa mikopo mipya pamoja na malimbikizo ya malipo ya madeni, ambapo katika deni hilo la nje, asilimia 83.4 ni deni la serikali na taasisi za umma.
Alisema pamoja na ongezeko hilo, takwimu zinaonesha kuwa deni hilo bado ni stahimivu kwani deni la nje kwa thamani ya sasa ni karibu ya asilimia 20 ya Pato la Taifa, ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 50 ya Pato la Taifa kutoka vigezo vya kimataifa, hali hiyo ikionesha bado kuna nafasi kubwa ya kukopa bila kuhatarisha ustahimivu wa deni hilo.
Akiba ya fedha za kigeni Alisema hazina ya fedha za kigeni imeendelea kuwa ya kuridhisha na kuendelea kukidhi mahitaji ya fedha za kigeni kwa ajili ya kuagiza bidhaa na huduma nje ya nchi ikiwa ni pamoja na kuongeza imani kwa wawekezaji katika uchumi wa Tanzania.
Alisema japokuwa kumekuwepo na ucheleweshwaji wa fedha za wahisani na mikopo ya kibiashara kutoka nje ya nchi, hadi Juni 2016 akiba ya fedha za kigeni ilifikia dola za Marekani milioni 3,870.3 ambazo zinatosheleza kuangiza bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa takriban miezi minne.
Kadhalika alisema rasilimali za fedha za kigeni za mabenki zilikuwa kiasi cha dola za Mmarekani milioni 835.0.

Breaking News:Upinzani waahirisha Operation UKUTA


Viongozi wa upinzani wakati wa kikao na wanahabari Dar es Salaam
Muungano wa vyama vya upinzani nchini Tanzania umeahirisha maandamano ya kitaifa ambayo yalikuwa yamepangiwa kufanyika kesho.
Viongozi wa upinzani, akiwemo Edward Lowassa wa Chadema, wametangaza hatua hiyo kwenye kikao na wanahabari Dar es Salaam.
Wamesema wameahirisha maandamano hayo kwa kipindi cha mwezi mmoja baada ya kusikia ombi la viongozi wa kidini na wadau wengine waliowaomba kukumbatia na kuyapa muda mazungumzo.

Majaliwa kupokewa rasmi Dodoma Alhamisi


WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa anatarajiwa kuhutubia mkutano mkubwa wa kwanza wa hadhara katika uwanja wa Jamhuri akiwa mkazi wa Mkoa wa Dodoma mara tu baada ya kupokewa rasmi mkoani hapa Alhamisi wiki hii.
Taarifa hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya Dodoma Mjini, Christina Mndeme, wakati wa mkutano wake na viongozi wa dini uliofanyika mjini hapa mwishoni mwa wiki.
Alieleza kuwa, baada ya Waziri Mkuu kupokelewa katika eneo la Mtimba, msafara wake utaelekea uwanja wa Jamhuri ambapo atazungumza na wananchi wa mkoa wa Dodoma.
Mkuu huyo wa wilaya aliwaomba viongozi wa dini, kushirikiana na serikali wilayani kumpokea waziri mkuu.
Alisema, waziri mkuu anahamia rasmi mjini hapa kwa ajili ya makazi na kuendesha shughuli zake mbalimbali, ikiwemo za chama na Serikali.
Kauli hiyo imetolewa wakati Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge, ikisema ukarabati wa nyumba ya Waziri Mkuu upo katika hatua ya mwisho kukamilika.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, Jenista Mhagama alisema hayo, baada ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ukarabati wa makazi hayo.
Aidha, Mhandisi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Joseph Mhamba, alisema shughuli zote za ukarabati zinazofanywa na Wakala wa Majengo (TBA), zinaendelea vizuri. Mhamba alisema kazi itakamilika kama ilivyopangwa.
Kwa upande wake, Mhandisi Kashimilu Mayunga kutoka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma Mjini (Duwasa), alisema kazi inayoendelea ni kuchimba mitaro na kulaza mabomba. Alisema kazi hiyo imekamilika kwa zaidi ya asilimia 70 na wanachosubiri sasa ni pampu.
Meneja wa mtandao wa Shirika la Simu (TTCL), Flavian Mziray alisema kazi ya kupeleka mawasiliano makazi ya Waziri Mkuu, inakaribia kukamilika.

Alichokisema Zitto Kabwe Juu Ya UKUTA

BUNGE LA MAREKANI LAIWEKEA VIKWAZO IRAN


Sambamba na kutimia mwaka mmoja tangu kufikiwa makubaliano ya nyuklia kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kundi la 5+1, baraza la wawakilishi nchini Marekani, limepasisha vikwazo vipya dhidi ya taifa hili.
Jana baraza la wawakilishi nchini Marekani ambalo linaundwa na silimia kubwa ya wawakilishi kutoka mrengo wa chama cha Republican, lilipitisha mpango wa vingee viwili wa vikwazo hivyo kwa kupigiwa kura ya ndio na wajumbe 246 kati ya 179 waliopinga mpango huo. Wawakilishi wa Marekani pia walipitisha kwa kura 246 kati ya 181 mpango wa kupiga marufuku Iran kunufaika na mfumo wa kifedha wa Marekani na pia sarafu ya dola katika miamala yake ya kigeni. Kabla ya hapo pia yaani siku ya Jumatano, baraza hilo la wawakilishi la Marekani lilipiga marufuku ununuzi wa maji mazito kutoka Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Miswada hiyo dhidi ya Iran ya Kiislamu imepitishwa katika hali ambayo Rais Barack Obama wa Marekani ametishia kuipigia kura ya veto kuipinga.

DAESH WAUA KUNDI LA WATU KTK MJI WA NICE, UFARANSA

Zaidi ya watu 84 wameripotiwa kuuawa katika shambulio lililotokea katika mji wa Nice kaskazini mwa Ufaransa.
Lori lililokuwa likienda mwendo wa kasi lilijipenyeza katika mkusanyiko wa watu waliokuwa wakishiriki maonesho ya fataki kuadhimisha siku ya kitaifa ya Bastille, ambayo huandamana na shamra shamra kila mwaka. Polisi walifanikiwa kumuua dereva wa lori hilo baada ya kujiri majibizano ya risasi yaliyochukua muda mrefu kwenye tukio hilo. Kamanda wa polisi wa mji wa Nice amekielezea kitendo cha dereva huyo kuwa cha kigaidi na amewataka wananchi kuchukua tahadhari. Kundi la Daesh limekiri kuhusika na shambulio hilo lililotokea nchini humo wakati wa sherehe za maadhimisho ya Siku ya Bastille. Rais François Hollande wa Ufaransa, sanjari na kulaani shambulizi hilo, amedai kuwa, nchi yake itaendeleza mashambulizi dhidi ya wanachama wa kundi hilo, nchini Syria. Inafaa kuashiria hapa kwamba, Ufaransa ni moja ya nchi waungaji mkono kwa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh nchini Syria kwa lengo la kutaka kuiondoa madarakani serikali halali ya Rais Bashar al-Assad wa nchi hiyo

Zitto aanika majina mabilioni ya Uswisi


Dar es Salaam. Kiongozi mkuu wa chama chama cha ACT – Wazalendo, Zitto Kabwe jana alianika orodha ya majina ya watu wanaotuhumiwa kuhodhi akaunti zenye mabilioni ya fedha nje ya nchi, lakini akasita kuyataja kutokana na sababu za kisheria.
Zitto aliwapa waandishi wa habari orodha hiyo akisema waende kufanyia kazi kwa kuwahoji wahusika kulingana na taaluma yao.
Orodha hiyo ina majina yenye asili ya kiasia isipokuwa wachache ambao wanaonekana wana majina ya kibantu.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Mwembeyanga, Temeke, Dar es Salaam, Zitto alisema: “Majina ninayo haya hapa niwataje nisiwatajee! Ni wengi sana wengine wanamiliki kampuni kubwa.”|
Alisema Zitto alisema wamejaribu kuishinikiza Serikali ichukue hatua, lakini inaonekana kutotaka kufanya hivyo na kwamba anaamini waandishi wa habari kwa kutumia taaluma yao wataweza kuwaanika wahusika.
Wakati maofisa wa ACT wakigawa orodha ya majina hayo, wananchi walionekana kuwa na shauku ya kupata nakala ya karatasi hiyo yenye majina 99 ya wafanyabiashara hao maarufu ndani na nje ya nchi, lakini kiongozi huyo hakuwa tayari kuwapatia na badala yake akiwaambia wasome magazeti ya kesho (leo).
Zitto alisema kwamba kati ya majina ya raia hao wenye mabilioni ya fedha nchini Uswisi, kuna wengine wanamiliki kihalali lakini wengine wamejirundikia isivyo halali.
‘’Nimeamua leo kuiweka orodha hii wazi kama shinikizo kwa Serikali kutoa taarifa ya uchunguzi kabla ya Bunge kuvunjwa wiki ijayo. Kila mwandishi wa habari aliyepo kwenye mkutano huu nimempatia nakala yenye majina 99 ya Watanzania au watu wenye uhusiano na Tanzania ambao wana akaunti HSBC ya Uswisi. Jumla ya akiba katika akaunti benki hii pekee ni Dola 114 milioni za Marekani,’’ alisema.
Wakati huohuo, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa ametawazwa kuwa chifu wa mkoa na wazee wa Dar es Salaam na kuitaka serikali kuhakikisha inawarudishia wananchi chenji zinazotokana na ufisadi wa Escrow , EPA na Richmond. Akizungumza katika kongamano hilo la wazee la kutafakari uchaguzi wa mwaka 2015, Dk Slaa alisema ingawa wazee waliungana na Hayati Mwalimu Nyerere kupambana na maadui wa tatu ambao ni ujinga, umaskini na maradhi lakini kwa sasa ameongezeka adui wa nne ambaye ni ufisadi.
“Ujinga alioupinga Mwalimu na wazee umeondoka? Lakini ujinga, umaskini na maradhi na kuna adui wa nne ambaye ni ufisadi,” alisema.
Alisema hakuna Mtanzania ambaye atakwenda dukani na Sh10,000 kununua chumvi na kibiriti halafu akaacha chenji yake dukani kwa makusudi na hivyo Watanzania bado wanadai fedha zao zilizopotea kutokana na ufisadi.
Kadhalika Dk Slaa alisema kitendo cha wazee hao kukutana katika kongamano hilo kinaashiria kuwa wana kiu, njaa na matumaini ya kutaka mabadiliko
“Mwalimu pia alipokewa na wazee wa Bagamoyo ambao walimuombea dua, akaenda kwenye makaburi na waliunganisha nguvu kumng’oa Mwingereza na kupata uhuru na mimi nawataka wazee wa Dar es Salaam kuongeza nguvu kuing’oa CCM,” alisema Dk Slaa.
Alizungumzia pia uandikishaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura na kuwataka wakazi wa Dar es Salaam kuwa makini na kuhakikisha wanajiandikisha.
Awali, katika kongamano hilo, Naibu Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu na Shura za Maimamu nchini Sheikh Rajab Katimba aliizungumzia kauli ya Katibu wa Itikadi na Uenezi, wa CCM Nape Nnauye ya kuwa CCM itashinda kwenye Uchaguzi Mkuu ujao hata kwa bao la mkono na kusema ni ya kichochezi.
“Wakati nchi inajitahidi kuwa na amani na kuwa na uchaguzi wa haki na huru, kiongozi wa chama anazungumza uchochezi mkubwa ambao kama viongozi wengine wangeusema sidhani kama wangekuwa salama,” alisema.
Sheikh Katimba aliwaasa Ukawa kuwa na umoja na kuwataka wawaite wazee ili wawape ushauri badala ya kulumbana kwani huu si wakati mwafaka wa kuwa na migogoro.

Hiki ndicho walichoamua Wagiriki kuhusu madeni yao


Mamilioni wa raia nchini Ugiriki wanapiga kura ya maamuzi kuhusu iwapo watakubali ama kukataa masharti yaliowekwa na wakopeshaji ili kulipa deni wanalodaiwa.
Akipiga kura,waziri mkuu Alexis Tsipras amesema kuwa hakuna anayeweza kupuuza uamuzi wa raia.
null
Serikali yake ya mrengo wa kushoto imewashauri wapiga kura kuyakataa mapendekezo yaliyotolewa na wakopeshaji wake.
Lakini viongozi wa Ulaya wameonya kuwa kura ya 'LA' itasababisa Ugiriki kuondoka kwenye nchi zinazotumia sarafu ya Yuro.
null
Kura ya maoni inaonyesha kuwa huenda matokeo yakakaribiana sana.
Benki nchini Ugiriki zimefunwa tangu wiki iliyopita huku uchumi ukiathirika pakubwa

Lowassa Afichua kimya cha muda mrefu

 
HATIMAYE Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, jana alivunja ukimya wa muda mrefu alipofanya mahojiano ya ana kwa ana na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari.
Katika mkutano huo,Lowassa aliitumia nafasi hiyo kutangaza msimamo wake wa siasa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Lowassa aliitumia fursa ya mahojiano hayo, yaliyofanyika nyumbani kwake eneo la Area C mjini hapa, kuwaeleza wahariri kuwa hana mpango wa kuhama CCM licha ya kuwapo shinikizo la chini kwa chini la kumtaka aondoke na kwamba wale wote wanaomtaka au wanaotamani aondoke, wanapaswa kuondoka wao.
Kauli hiyo aliitoa wakati akijibu swali iwapo CCM hakitamteua kuwa mgombea urais atachukua uamuzi gani kwa sababu jina lake limekuwa likihusishwa na mpango wa kukihama endapo jina lake halitapitishwa.
Alisema maisha yake yote ya siasa yamekuwa ndani ya CCM na kauli zinazomuhusisha na kuhama chama hicho, amekuwa akizisikia na kuzipuuza kwa sababu jambo hilo hawezi kulifanya.
“Nimekuwa mwanachama wa CCM tangu mwaka 1975, maisha yangu yote ya siasa yamekuwa ndani ya chama hiki isipokuwa muda mfupi ambao nilikwenda kupigana vita Uganda na nilipokuwa nikifanya kazi katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (IACC). Sitahama chama isipokuwa wasionitaka waondoke wao,” alisema Lowassa.
Lowassa ambaye alikataa kujibu baadhi ya maswali ya wahariri waliotaka kujua iwapo minong’ono ya muda mrefu inayohumusisha na kuwania urais ni ya kweli, alisema suala hilo litajulikana Jumamosi, Mei 30 katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha.
Alisema hapo atatoa hotuba ya kuanza kwa safari ya matumaini huku akisisitiza ana uhakika na anakichofanya na hana mpango mwingine mbadala isipokuwa wa mafanikio.
Akizungumzia tetesi ambazo zimekuwa zikisambaa kwa muda mrefu sasa kuhusu kulegalega kwa uhusiano wake na Rais Jakaya Kikwete, Lowassa alieleza kushangazwa na hilo na kuhoji msingi wa baadhi ya watu kuzungumzia urafiki binafsi kati yake na Kikwete.
Alisema tangu alipojiuzulu nafasi ya uwaziri mkuu 2008, amesikia mengi yakisemwa kwa uzuri na ubaya kumuhusu yeye, likiwamo la kulegalega uhusiano wake na Kikwete, lakini aliamua kuwa kimya kwa sababu kunyamaza ni hekima.
Alisema mbali na taarifa hizo alizoziita za upotoshaji kuhusu uhusiano wake na Rais Kikwete kuzorota, zipo nyingine nyingi za aina hiyo ambazo zimekuwa zikiibuliwa na kutangazwa katika vyombo mbalimbali vya habari kwa sababu za uhasama na chuki za siasa.
“Tangu nilipoondoka kwenye uwaziri mkuu, nimekuwa kimya kwa sababu wakati mwingine kunyamaza ni hekima. Niliamua kuwa kimya kwa vile niliogopa upotoshaji. Siasa zetu hapa nchini zimekuwa za chuki, uhasama na kusingiziana na inatupa shida kweli, nikaamua kunyamaza.
“Sasa wanaozusha kuwa uhusiano wangu na Rais Kikwete umezorota wamepata wapi? Hili suala la urafiki wangu na rais acheni kulipotosha,” alisema Lowassa.
Waziri Mkuu huyo wa zamani alizungumzia pia minong’ono ambayo imekuwa ikimuhusisha na kujilimbikizia mali pamoja na ushiriki wake katika harambee hususan anazoalikwa kwenye nyumba za ibada na kiwango cha fedha anachochangia.
Alisema wote wanaodhani amejilimbikizia mali kwa njia za ufisadi wafuatilie jambo hilo kwenye Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Akifafanua hilo, alisema amekuwa mbunge kwa zaidi ya miaka 20 na kwa mujibu wa mila na utamaduni wa jamii yake, kiongozi lazima awe na mali hasa ng’ombe na nyumba.
“Nina mali, nina nyumba na ng’ombe kati 800 na 1,200, mwenye shaka na mali zangu aende kamati ya maadili. Lakini katika jamii yangu kiongozi ni lazima uwe na mali na mimi nachukia sana umaskini na Watanzania tusikumbatie umaskini. Utajiri si dhambi na mimi natafuta uongozi ili kuuondoa umaskini wa Watanzania,” alisema Lowassa.
Kuhusu ushiriki wake katika harambee na kiasi cha fedha anazochangia, alisema utamaduni wa kuchangia shughuli za maendeleo umesaidia jamii nyingi za watu katika maeneo mbalimbali duniani kufanikisha malengo yao,
Alisema kwa kutambua hilo amekuwa mstari wa mbele kushiriki na kuhamasisha watu kuchangia.
“Jirani zetu wa Kenya, wamefanikiwa sana katika baadhi ya mambo yao kwa sababu ya harambee za aina hii na ndiyo maana mimi pia nimekuwa mstari wa mbele kuwahamasisha watu kuchangia shughuli zao za maendeleo.
“Sina fedha kama hizi zinazosemwa lakini nina marafiki. Hawa ndiyo ninaowatumia kufanikisha malengo ya harambee ninazoshiriki ingawa hili nalo limekuwa likipotoshwa kama ilivyotokea juzi juzi hapa watu wakasema nimeita watu 300 na kuwakaribisha hapo mlipokaa ninyi. Angalieni wenyewe eneo hili mlipo kweli wanaweza kuingia idadi hiyo ya watu?” alisema Lowassa.
AFYA YAKE
Akizungumzia suala la afya yake, Lowassa alisema yuko fiti kwa chochote kile na amekiomba chama chake kuweka utaratibu wa kuwapima afya makada wake wote wanaoutaka urais.
“Niko fiti, wanaosema naumwa ni wazushi, siasa zimekuwa za uhasama, kusingiziwa na kutafutana hata nikikimbia kilomita 100 watasema Lowassa mgonjwa. Nilikimbia kilomita tano ikaandikwa nimekwimbizwa Ujerumani kutibiwa.
“Mimi nakiomba chama kiweke utaratibu wa watu wote wanaotaka urais wapime afya zao, niko fiti na niko tayari kwa chochote, tukutane kwenye uwanja wa mapambano,” alisema.
UWAZIRI MKUU
Alipoulizwa kama angeendelea kuwa waziri mkuu hadi leo Serikali ya awamu ya nne ingekuwaje, Lowassa alisema hali ingekuwa tofauti kabisa na anaamini kamwe asingekuwa na kazi ya kuomba kura kwa sababu angepita bila kupingwa.
“Nadhani tungekuwa tunaongea mambo mengine leo wala nisingeomba kura, ningepita barabarani na kupunga mkono tu,” alisema.
TATIZO LA AJIRA
Kuhusu tatizo la ajira nchini, mbunge huyo wa Monduli alisisitiza kuwa ni bomu na lisiposhughulikiwa mapema litalipuka.
“Vijana wengi kujiingiza kwenye biashara ya bodaboda ni kielelezo cha ukosefu wa ajira, suala hili kwangu ni kipaumbele namba moja, mbili na tatu,”alisema.
NGUVU YA UPINZANI
Kuhusu nguvu ya vyama vya siasa vya upinzani nchini, alisema upinzani umeanza kupata nguvu mijini na vijijini, hivyo chama tawala kisibweteke wala kufanya mchezo na upinzani.
“Hata hivyo,Rais Kikwete amejitahidi kutekeleza ilani ya chama kwa kiasi kikubwa, hilo linaweza kukisaidia chama,”aliongeza.
SAKATA LA RICHMOND
Kuhusu suala la Richmond, Lowassa alisema hakuna haja ya kulizungumzia suala hilo kwa sababu limeshasemwa na kuandikwa sana, ingawa anaamini hakukuwa na makosa kwenye mkataba wa mitambo hiyo na hata Rais wa Marekani,Barack Obama na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Hilary Clinton walisema mitambo hiyo haina shida.
“Suala la Richmond sioni haja ya kulizungumzia zaidi, limeshasemwa na kuandikwa sana lakini mnapaswa kujua ubishi ule umerigharimu taifa Dola za Marekani bilioni 120, hata hivyo nilijua tatizo si Richmond, tatizo lilikuwa ni uwaziri mkuu,” alisema.
VIPAUMBELE
Kwa upande wa vipaumbele vyake, alisema kwake elimu kwanza, kilimo baadaye na kwamba hakubaliani na mpango wa Kilimo Kwanza.
“Mataifa mengi yaliyoendelea yaliwekeza zaidi kwenye elimu, ukiwekeza kwenye eneo hilo ni rahisi kuendelea.
“Nawaambieni kweli tukiwekeza kwenye elimu tutaibadili nchi hata tatizo la ajira litakwisha.
VISASI
Kuhusu visasi, Lowassa alisema hana kisasi na mtu, hata dini yake haimruhusu na inamtaka kusamehe saba mara sabini.
“Sina kisasi na mtu na sina mpango wa kufukua makaburi, naomba tuchape kazi na kujenga nchi yetu.
Tangu alipojiuzulu uwaziri Mkuu mwaka 2008 Lowassa hakupata kujitokeza hadharani kuzungumza na vyombo vya habari.
Hii ni mara ya kwanza kwa Lowassa katika kipindi cha takriban miaka saba sasa, kujitokeza mbele ya wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini kujibu na kutoa ufafanuzi wa mambo ambayo yamekuwa yakielekezwa kwake.
Majibu ya Lowassa aliyoyatoa jana kwa wahariri kuhusu tuhuma na madai mengi ambayo yamekuwa yakimuandama, yamekuwa mjadala kwa kipindi chote cha takriban miaka saba ya ukimya wake na yamekuwa yakitafsiriwa kwa namna tofauti tofauti na mashabiki na wapinzani wake wa siasa.

Saudia yazuia ndege za Iran kutuaYemen, Iran watuma Misaaada kupitia Oman

Iran inatuma misaada nchini Yemen kupitia Oman
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Hilali Nyekundu ya Iran amesema kuwa Tehran inatuma misaada ya kibinadamu huko Yemen kupitia nchi nyingine za pambizoni mwa Ghuba ya Uajemi khususan Oman. Ali Asghar Ahmadi amesema kuwa hatua ya Saudi Arabia ya kuzizuia ndege za Iran zilizobeba misaada ya kibinadamu kutua katika uwanja wa ndege wa San'aa mji mkuu wa nchi hiyo ni kitendo kisicho cha kibinadamu na kinachokinzana na sheria za kimataifa. Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Hilali Nyekundu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, pamoja na kuweko vizuizi hivyo, lakini jumuiya hiyo hadi sasa imeweza kuwatumia wananchi wa Yemen shehena tatu za bidhaa muhimu za mahitajio kupitia taasisi moja ya misaada ya kibinadamu ya nchini Oman. Ahmadi amesema, anataraji kuwa misaada hiyo ambayo inajumuisha bidhaa za chakula, madawa na suhula za kitiba, itawawafikia wananchi wa Yemen hivi karibuni. Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Hilali Nyekundu ya Iran amesema kuwa taasisi hiyo iko imejiandaa pia kutuma misaada ya kibinadamu kwa waathirika wa zilizala huko Nepal

Iran: Matamshi ya Stephen Harper ni ya kipumbavu

Iran: Matamshi ya Harper ni ya kipumbavu
Msemaji wa Wizara ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekosoa vikali matamshi ya Waziri Mkuu wa Canada, Stephen Harper na kuyataja kuwa ya kijuba na kipumbavu. Bi. Marzie Afkham amesema madai ya Harper kwamba Wairani wanaishi chini ya utawala wa kiimla yanaonyesha jinsi kiongozi huyo alivyo na chuki dhidi ya taifa hili. Kwenye hotuba yake ya siku ya Jumamosi mbele ya Wairani wanaoishi Canada, Waziri Mkuu Stephen Harper alidai kwamba Iran inaendeshwa kidikteta na kwamba raia wa nchi hii hawajui ladha ya demokrasia. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema Harper anajaribu kutumia madai ya uongo ili kuwashawishi Wairani wenye uraia wa Canada waunge mkono chama chake kwenye uchaguzi ujao wa bunge.
Uhusiano wa Iran na Canada ulivurugika zaidi mwaka 2012 baada ya serikali ya Ottawa kutangaza kuwa imefunga ubalozi wake hapa mjini Tehran na baadaye kuanza kutoa madai ya uongo na ya kipropaganda dhidi ya viongozi na serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Serikali Iwakamate Maaskofu Waliotoa Tamko - Waislam, Vinginevyo Waislam Wote watapiga Kura Ya HAPANA


Taasisi ya dini ya Kiislam imeitaka serikali kuwakamata maaskofu na wachungaji ambao  inadai wametoa matamko ya kichochezi na endapo serikali itashindwa kuwakamata, basi jumuiya hiyo itawahamasisha waamini wa dini ya kiislam popote walipo kuipigia kura ya Hapana Katiba inayopendekezwa na Bunge Maalum la Katiba.
 
Kauli ya taasisi hiyo yenye misimamo mikali inatokana na Tamko lililotolewa  na muunganiko wa jumuiya ya Kikristo,ikiwemo Baraza la Maaskofu katoliki (TEC),Jumuiya ya Kikristo Tanzania(CCT)  na  Baraza la Makanisa la kipentekoste(CPCT) ambao wote  kwa pamoja waliwataka waumini wa dini ya kikristo nchini kuipigia kura ya Hapana katiba inayopendekezwa kutokana na serikali  kuruhusu mahakama ya Kadhi kisheria.
 
Akitoa tamko la Taasisi ya Dini ya Kiislam  ambalo ni muunganiko wa taasisi za dini hiyo zaidi ya 11 hapa nchini,Naibu Katibu Mkuu wa Taasisi hiyo Sheikh Rajab Katimba wakati wa Mkutano na Vyombo mbalimbali vya habari  jana  Jijini Dar es Salaam, aliitaka serikali kuwachukulia  hatua maaskofu hao kwa madai ya kufanya uchochezi.
 
“Serikali iwachukulie hatua za kisheri maaskofu na wachungaji kwa kutoa matamko yakichochezi yaliyokusudia kuumiza hisia ya kidini kwa waislam kinyume cha sheria ya kanuni ya Adhabu sura ya 16.
 
"Tunataka  Maaskofu  hao  wakamatwe,wafikishwe mahakamani na  dhamana  izuiliwe kama inavyofanya kwa masheikh pindi wanapotoa kauli zinazopingana na mtazamo wa serikali,lasivyo hatutaipigia kura ya Ndiyo katiba iliyopendekezwa”alisema Seikh Katimba.
 
Aidha, Sheikh Katimba  aliitaka  Serikali kuendelea na Mchakato wa uundwaji mahakama ya kadhi kwa kufuata maoni yaliyotolewa mbele ya kamati ya sheria na utawala wa bunge kwa kuzingatia mambo muhimu  mawili.
 
Mosi: Serikali iache njama na hila za kuigeuza mahakama ya Kadhi inayohitajika kuwa miliki ya taasisi ya BAKWATA na MUFTI wa BAKWATA.
 
“Endapo serikali itaendelea na kuwasilisha muswaada wa Mahakama ya Kadhi unaoipa mamlaka Bakwata kuunda,kusimamia,kuteua makadhi nakadhalika kinyume na maoni ya Waislam wengi itakuwa imethibitisha kuwa serikali haikuwa na nia ya kweli ya kuunda na kuanzisha mahakama ya Kadhi” alisema Sheikh Katimba.
 
Pili: Serikali igharamie mahakama hiyo kama inavyogharimia uendeshaji wa mashauri yaliyopo kwenye mahakama za kawaida yanayohusu sheria za kiislam ambayo mara nyingi yanaamuliwa kwa makosa.
 
“Na pia mahakama  hiyo igharamiwe na serikali  kama inavyogaramia huduma za makanisa chini ya mkataba maarufu uitwao memorandum of understanding (MOU) , mkataba  ambao haukuwahusisha wala kutaka ridhaa ya waislam” alisema  sheikh  huyo.

Edward Lowassa: Nimeshawishika kuwania urais TZ

Edward Lowassa: Nimeshawishika kuwania urais TZ
Hatimaye mbunge wa Monduli nchini Tanzania, Edward Lowassa, amesema ameshawishika kugombea urais wa nchi hiyo kwa tiketi ya chama cha CCM na ametangaza rasmi kuwa, atachukua fomu ya kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho tawala. Lowassa ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu ya Nne huko Tanzania, kwa muda mrefu amekuwa akitajwa kuwa mmoja wa makada wa CCM wenye nia ya kugomea urais, lakini hakuwahi kutangaza nia ya kuwania nafasi hiyo. Lakini jana, alizungumzia suala la urais ambalo lilimfanya yeye na wenzake watano wafungiwe kwa kipindi cha miezi 12 kujihusisha na harakati hizo baada ya Kamati Kuu ya CCM kuwatia hatiani kuwa walianza kampeni mapema kabla ya muda kufika. "Nimepata barua za ushawishi kutoka kwa watu wengi, lakini nyinyi nimeshawishika," alisema Lowassa nyumbani kwake mjini Dodoma wakati alipokuwa anazungumza na masheikh wa misikiti ya Wilaya ya Bagamoyo wanaokadiriwa kufikia 50 ambao pia walikwenda mjini humo kwa ajili ya kumshawishi aingie kwenye kinyang'anyiro cha urais na kumkabidhi mchango wa Sh700,000 kwa ajili ya kuchukulia fomu.

NIMEJIUNGA RASMI NA ACT - ZITTO KABWE

Aliyekuwa mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe leo ametangaza rasmi kujiunga na Chama cha ACT Wazalendo.
Katika maelezo yake kwa waandishi wa habari jijini Dar es salaam leo, Zitto amesema kuwa amejiunga na chama hicho tangu jana Jumamosi (Machi 21, 2015) kupitia tawi la Tegeta Dar es salaam na kupewa kadi namba 71.
Amesema ameamua kujiunga na chama hicho ili kuendeleza mapambano ya demokrasia nchini kwa kuwa chama hicho ni wazalendo wa kweli.
Naye msanii wa Hip Hop nchini Seleman Msindi maarufu kwa jina la Afande Sele ametangaza kumfuata Zitto Kabwe kwa kuachana na CHADEMA na kujiunga na ACT Wazalendo.
Ifuatayo ni sehemu ya alichozungumza Zitto Kabwe mbele ya waandishi wa habari leo
 
"Nimejiunga na ACT kwa sababu ninaona kwamba huku ndiko kunakoendana na kile ambacho mimi nimekipigania kwa miaka yote tangu nianze siasa, ambacho ni kuweka mbele maslahi ya Taifa dhidi ya kitu kingine chochote. Kwa kifupi nimepigania uzalendo kwa nchi yangu na huu ndiyo msingi mama wa Chama cha ACT - Wazalendo.
Kama mnavyojua mimi ni mjamaa na ninaamini katika misingi ambayo Mwalimu Nyerere aliisimamia. ACT-Wazalendo ni chama pekee nchini kinachokubaliana na Itikadi ya ujamaa na kinaamini katika Falsafa ya Unyerere ikiwa na lengo la kuirudisha nchi katika misingi iliyoasisi taifa. Ninajiunga na ACT-Wazalendo kwa sababu ni chama kinachoamini katika msingi wa uadilifu na kimeweka miiko na maadili ya viongozi katika kuhakikisha kwamba viongozi wote wa ACT-Wazalendo wanakubaliana nayo kwa kusaini. Naamini kuwa na miiko na maadili kwa viongozi ni mwanzo wa kuhakikisha kwamba jamii yetu inaishi katika uadilifu na kwamba viongozi wanakuwa mfano wa uadilifu katika jamii. Uadilifu ni nguzo muhimu katika kujenga mfumo madhubuti wa uwajibikaji nchini kwetu.
Nimejiunga na ACT-Wazalendo kwa sababu ninakubaliana na imani yao kwamba Kujitegemea, bidii, umakini na weledi katika kazi ndiyo msingi wa maendeleo.
Hakuna namna nchi yetu na wananchi watapiga hatua ya kimaendeleo bila sisi sote kufanya kazi kwa bidii na kwa kuzingatia umakini na weledi. Ninakubaliana na ACT-Wazalendo kwamba raslimali za Taifa lazima zitumike kuondosha umaskini wa watu wetu.
Ninajiunga na ACT-Wazalendo kwa sababu ninakubaliana na imani yao kwamba Umoja ni ngao muhimu katika ujenzi wa taifa letu na Afrika kwa ujumla. Lazima tuirudishe nchi yetu katika misingi iliyoasisi taifa hili. Lazima tuirudishe nchi yetu katika heshima na uongozi wa bara hili la Afrika.
Ninaahidi kufanya kazi na vijana, wanawake, wanaume na watu wote wanaoamini katika siasa safi na siasa za hoja. Tunataka tufungue ukurasa mpya wa siasa hapa nchini. Siasa za masuala ya nchi yetu. Siasa za masuala ya vijana, wanawake, wazee, wakulima, wafanyakazi, wajasirialimali, wafanyabiashara na wote wanahangaika kuijenga nchi yetu na katika kuondoa umaskini.
Tunataka tuzungumze namna bora ya kuendesha elimu, afya, hifadhi ya jamii, na ajira. Tunataka tujenga hoja mbadala kuhusu namna endelevu ya kujenga uchumi shirikishi ambapo kila mwananchi anajisikia sehemu yake."

EU yaonya juu ya njama za kuigawa Masjidul Aqsa

EU yaonya juu ya njama za kuigawa Masjidul Aqsa
Umoja wa Ulaya umetahadharisha juu ya njama zinazofanywa na utawala haramu wa Israel za kutaka kuugawa msikiti mtakatifu wa al-Aqsa huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Ripoti ya EU iliyochapishwa kwenye gazeti la The Guardian la Uingereza inasema kuwa, kuendelea ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi zilizoghusubiwa za Palestina, kushadidi njama za kuigawa Masjidul Aqsa  pamoja na hujuma za kila mara za Wazayuni dhidi ya Wapalestina kunahatarisha mustakabali wa Mashariki ya Kati na kwamba hali hiyo inazidi kuzuia uwezekano wa kuweko kile kinachotajwa kuwa ni ‘suluhu kwa njia ya mataifa mawili’. Ripoti ya umoja wa Ulaya pia imeashiria udharura wa kushinikizwa zaidi utawala haramu wa Israel ili ukubali kurudi kwenye meza ya mazungumzo na Wapalestina bila masharti. Umoja wa Ulaya umesema Israel inapaswa kuheshimu sheria zote za kimataifa na kusimamisha mara moja ujenzi zaidi wa vitongoji kwenye ardhi za Wapalestina.

"Iran haitishwi na vikwazo wala nguvu za kijeshi" - Muadhamu

"Iran haitishwi na vikwazo wala nguvu za kijeshi"
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, kuondolewa vikwazo ni sehemu ya mazungumzo ya nyuklia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kundi la 5+1. Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei amesema hayo leo mbele ya hadhara kubwa ya wafanyaziara na majirani wa haram tukufu ya Imam Ali bin Mussa al-Ridha (as) mjini Mash'had ambapo sambamba na kuashiria mazungumzo ya nyuklia ya Iran na nchi za Ulaya na Marekani amebainisha kuwa, upande wa pili unaofanya mazungumzo na Iran hususan Marekani una haja na mazungumzo na kwamba, hitilafu zilizoko baina ya Wamarekani hazina maana kwamba, Washington haina haja na mazungumzo haya. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, salamu za Rais Barack Obama wa Marekani kwa mnasaba wa sikukuu ya Nouruz hazikuwa na ukweli na kubainisha kwamba, Marekani ndiyo sababu kuu ya mashinikizo dhidi ya taifa la Iran na imekuwa ikifanya kila iwezalo ili kulitwisha taifa hili ubeberu wake. Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa, hakuna mtu ndani ya Iran ambaye hataki kadhia ya nyuklia ipatiwe ufumbuzi, bali kile ambacho taifa la Iran halikitaki ni utumiaji mabavu, ubeberu na utwishaji mambo wa Marekani. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, taifa la Iran halitishwi na vikwazo wala nguvu za kijeshi kwani limesimama kidete na liko imara. Amebainisha kwamba, katika mazungumzo yake na kundi la 5+1, Iran haifanyi mazungumzo kuhusiana na masuala yasiyo ya kimantiki. Aidha Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, inachotaka Iran ni utulivu na kushikwa hatamu na wananchi wenyewe wa mataifa ya Mashariki ya Kati, lakini siasa za Marekani ni kuleta vurugu na machafuko.

Masheikh 50 Waandamana Kwenda Kwa LOWASSA Kumtaka Agombee URAIS 2015.......Wamkabidhi 700,000 Imsaidie Kuchukua Fomu

MASHEKHE wapatao 50 kutoka Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani, leo wamemkabidhi kiasi cha shilingi 700,000/- za kuongezea kuchukua fomu ya kuwania Urais 2015. 
  Mashekhe hao wakiongozwa na Yusuf Surulu (kulia kwenye picha juu) na Alli Mtumwa (wapili kulia) wamemkabidhi fedha hizo nyumbani kwake mjini Dodoma na kushuhudiwa na Mbunge wa Urambo Magharibi, Prof Juma Kapuya.

Mashekhe hao kutoka maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Bagamoyo, wamesema katika salamu zao kuwa wameona mtu pekee anayefaa kushika wadhifa huo ni yeye (Lowassa) hivyo wanamsihi atangaze nia na achukue fomu ya kugombea na wapo nyuma yake katika dua.
  Lowassa amewaambia viongozi hao wa dini kuwa makundi mbalimbali ya jamii yamekuwa yakimuomba kugombea Urais lakini wao wamemfanya ashawishike sasa kufanya hivyo wakati ukifika.
"Ila nataka kuwaahidi, naheshimu sana maneno yenu na nayakubali kwamba siku ikifika kwa taratibu za chama nitachukua fomu," alisema.
Lowassa amesema endapo Mungu atamjalia kushinda uchaguzi, atahakikisha anaendeleza pale Rais Jakaya Kikwete katika nyanja mbalimbali za elimu, afya kilimo kwanza, na huduma nyingine muhimu kwa jamii.
Lowassa amesema "nikifanikiwa nitaanza na elimu, na kufanya elimu kipaumbele chetu kwani elimu ndio msingi wa kila kitu."  
Mbunge wa Monduli na Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa (kushoto) akiwa amepokea fedha zilizo changwa na Mashekhe kutoka Wilaya ya Bagamoyo. Walio mkabidhi fedha hizo ni Shekhe Yusuf Surul (kulia) na Ally Mtumwa. Mwingine ni Mbunge wa Urambo Magharibi, Prof. Juma Kapuya. MASHEKHE hao wakiwasili nyumbani hapo kwaajili ya mazungumzo na Lowassa. Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowassa akiwasikiliza viongozi wa msafara huo. Edward Lowassa akizungumza na Mashekhe hao mjini Dodoma. Mashekhe hao kutoka maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Bagamoyo, Mlingotini, Kaole, Chalinze, Lugoba, Msata na kwingineko. Duaa ilisomwa na viongozi hao wa dini. Edward Lowassa akiwasindikiza viongozi hao.

Raia wa Rwanda na Kenya huru kuingia Uganda kufanya kazi

Serikali ya Uganda imeondoa ada ya kibali cha kufanyia kazi nchini humo pamoja na mahitaji ya viza miongoni mwa raia wa Kenya na Rwanda wanaoingia na kutoka taifa hilo.
Uamuzi huo uko sambamba na uidhinishaji wa mtindo wa uhuru wa kutembea chini ya Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Soko la pamoja ambayo iliafikiwa mwaka 2009 na marais Museveni wa Uganda,Mwai Kibaki wa Kenya na Jakaya Kikwete wa Tanzania,Paul Kagame wa Rwanda na Pierre Nkurunziza wa Burundi.
Kamishna wa udhibiti wa uhamiaji katika wizara ya maswala ya ndani bwana Anthony Namara ameliambia gazeti la Monitor jumamosi kwamba raia wa mataifa hayo mawili pia hawatahitajika kutoa viza ama vibali vyovyote vya usafiri ili kuingia Uganda isipokuwa vitambulisho vyao pekee.
Amesema kuwa Kenya na Rwanda tayari zinaidhinisha mpango huo wa uhuru wa kutembea ambao unalenga kuimarisha utalii katika eneo hili mbali na kuruhusu usafiri wa wataalam katika mataifa haya matatu.