GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu amesema hali ya ukuaji wa uchumi nchini imeendelea kuwa ya kuridhisha na kwamba wastani wa mfumuko wa bei katika miezi sita ya kwanza ya mwaka huu umeendelea kushuka hadi kufikia asilimia 5.5 Juni mwaka huu na asilimia 4.9 Agosti 2016 kutoka asilimia 6.8 iyokuwapo Desemba 2015.
Aidha, amesema kupotea kwa fedha kunatokana na Serikali ya Awamu ya Tano kudhibiti makusanyo ya kodi, kuziba mianya mbalimbali ya upotevu wa fedha na kubana kazi zisizokuwa rasmi ‘misheni town’ na fedha hizo kuelekezwa kusaidia umma badala ya kwenda kwa wachache wanaojipatia isivyo halali.
Pia amesisitiza kuwa hakuna mdororo wa uchumi kwa kuwa ipo miradi mikubwa ya viwanda na miundombinu inayoendelea na inayotarajiwa kuanza kazi siku za usoni ambayo itachangia katika kuimarika kwa uchumi; hivyo kuweka takwimu sahihi tofauti na madai ya baadhi ya wanasiasa wa upinzani kuwa kuna mdororo wa uchumi.
Profesa Ndulu akitoa taarifa kuhusu hali ya uchumi wa Tanzania jana jijini Dar es Salaam, alisema katika robo ya kwanza ya mwaka 2016 ukuaji wa Pato la Taifa ulikadiriwa kuongezeka kwa asilimia 5.5 ikilinganishwa na asilimia 5.7 kipindi kama hicho mwaka jana.
Kadhalika alisema wastani wa mfumuko wa bei katika miezi sita ya kwanza ya mwaka 2016 umeendelea kuwa mzuri, ukiendelea kushuka hadi kufikia asilimia 5.5 Juni mwaka huu na asilimia 4.9 Agosti 2016 kutoka asilimia 6.8 Desemba mwaka jana.
Kuhusu hali ya ukuaji wa uchumi, alisema zipo shughuli mbalimbali zilizochangia ukuaji huo wa uchumi kwa kiasi kikubwa ikiwamo kilimo asilimia 11.7, biashara asilimia 10.6, uchukuzi asilimia 10.1, sekta ya fedha asilimia 10.1 na mawasiliano asilimia 10.0, sekta ya fedha asilimia 13.5, mawasiliano asilimia 13.4 na utawala wa umma asilimia 10.2.
Matazamio ya ukuaji wa uchumi 2016 Profesa Ndulu alisema kwa kuangalia viashiria mbalimbali inaonekana kuwa hali ya uchumi nchini itaendelea kuimarika katika mwaka 2016 na kuwa asilimia 7.2.
Alivitaja viashiria hivyo kuwa katika uzalishaji wa umeme, uzalishaji wa saruji, uzalishaji wa malighafi za viwandani, mauzo ya bidhaa za viwanda nje ya nchi, makusanyo ya kodi na mikopo itolewayo na mabenki ya biashara.
Alisisitiza kuwa hakuna mdororo wa uchumi kwa kuwa ipo miradi mikubwa ya viwanda na miundombinu inayoendelea na inayotarajiwa kuanza kazi siku za usoni ambayo itachangia katika kuimarika kwa uchumi.
Aliitaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni pamoja na ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa, ujenzi wa bomba la mafuta la Uganda ambalo litahusu vilevile upanuzi wa bandari ya Tanga, ujenzi wa eneo la kibiashara Kurasini itakayokuwa mhimili wa biashara kati ya China na ukanda wa Afrika.
Alisema miradi mingine ni ule wa kuzalisha megawati 240 za umeme wa Kinyerezi II, kupanua viwanja vya ndege nchini, ujenzi wa maghala ya Taifa ya kuhifadhi chakula yenye uwezo wa kuhifadhi tani 350, ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha saruji cha Dangote na ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza marumaru Mkuranga mkoani Pwani.
Miradi mingine ni ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha mbolea mkoani Lindi na kiwanda cha bidhaa za chuma mkoani Pwani ambacho kiko mbioni kukamilika. Alisema kwa miradi yote hiyo ni dhahiri kuwa hali ya uchumi nchini ni nzuri na inatoa matumaini makubwa kwamba shughuli halali za kiuchumi zinaendelea kama ilivyotarajiwa hapo awali.
Alisema lengo la ukuaji wa Pato la Taifa ni asilimia 7.2 kwa mwaka huu, na litafanikiwa, ambapo inachangiwa na ukweli kwamba Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga katika kuimarisha uchumi endelevu usiokuwa na mianya ya rushwa, usimamizi thabiti wa rasilimali za umma, ujenzi wa miundombinu bora kwa lengo la kujenga uchumi wa viwanda chini ya mpango wa maendeleo wa miaka mitano. Mwenendo wa mfumuko wa bei Mchumi huyo alisema kushuka kwa mfumuko wa bei kwa wastani kulichangiwa zaidi na bei zisizojumuisha bei za vyakula na nishati zikifuatiwa na zile za nishati na mafuta.
Alisema wastani wa mfumuko wa bei usiojumuisha bei za vyakula na nishati ambao ni kiashiria sahihi zaidi cha utekelezaji wa sera ya fedha, umeendelea kubaki katika viwango vya chini yaani,wastani wa asilimia 2.8 katika miezi sita ya mwanzo ya mwaka huu.
Alisema hali hiyo inatokana na hatua mbalimbali thabiti zilizochukuliwa za sera ya fedha na bajeti katika kudhibiti ujazi wa fedha na ukwasi katika uchumi.
Hata hivyo, alisema mfumuko wa bei utaendelea kubakia katika viwango vya tarakimu moja katika siku zijazo na kufikia lengo la muda wa kati ya asilimia tano ikitokana na matarajio ya hali nzuri ya hewa itakayochangia kupungua kwa kasi ya kuongezeka kwa bei za vyakula.
Kadhalika, alisema pamoja na ongezeko dogo la bei ya mafuta nchini inayotokana na mwenendo wa bei katika soko la dunia, utulivu wa thamani ya Shilingi, mwendelezo wa sera thabiti ya fedha, usimamizi mzuri wa mapato ya serikali na upatikanaji wa umeme utokanao na gesi utasaidia kupunguza gharama za uzalishaji viwandani.
Alisema hata hivyo, ni muhimu kuzingatia kuwa upungufu wa mavuno ya mazao ya chakula uliojitokeza kwa baadhi ya nchi za ukanda wa kusini mwa Afrika unaweza kusababisha shinikizo la mfumuko wa bei katika siku za usoni. Deni la Taifa Alisema kasi ya uongezekaji wa deni imepungua kwa sababu ukopaji nje ya nchi katika masoko ya kibiashara umepungua.
Hata hivyo, alisema deni la nje liliongezeka kwa asilimia 2.6 na kufikia Dola za Marekani milioni 16,281 Juni mwaka huu sawa na asilimia 77.8 ya deni la taifa kutoka Dola za Marekani milioni 15,864 Desemba mwaka jana.
Alisema kuongezeka kwa deni hilo kulitokana na kuongezeka kwa mikopo mipya pamoja na malimbikizo ya malipo ya madeni, ambapo katika deni hilo la nje, asilimia 83.4 ni deni la serikali na taasisi za umma.
Alisema pamoja na ongezeko hilo, takwimu zinaonesha kuwa deni hilo bado ni stahimivu kwani deni la nje kwa thamani ya sasa ni karibu ya asilimia 20 ya Pato la Taifa, ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 50 ya Pato la Taifa kutoka vigezo vya kimataifa, hali hiyo ikionesha bado kuna nafasi kubwa ya kukopa bila kuhatarisha ustahimivu wa deni hilo.
Akiba ya fedha za kigeni Alisema hazina ya fedha za kigeni imeendelea kuwa ya kuridhisha na kuendelea kukidhi mahitaji ya fedha za kigeni kwa ajili ya kuagiza bidhaa na huduma nje ya nchi ikiwa ni pamoja na kuongeza imani kwa wawekezaji katika uchumi wa Tanzania.
Alisema japokuwa kumekuwepo na ucheleweshwaji wa fedha za wahisani na mikopo ya kibiashara kutoka nje ya nchi, hadi Juni 2016 akiba ya fedha za kigeni ilifikia dola za Marekani milioni 3,870.3 ambazo zinatosheleza kuangiza bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa takriban miezi minne.
Kadhalika alisema rasilimali za fedha za kigeni za mabenki zilikuwa kiasi cha dola za Mmarekani milioni 835.0.