pagead2.googlesyndication.com pagead2.googlesyndication.com

Mwandishi afariki dunia Dar

MWANDISHI wa habari mkongwe, Maurus Sichalwe, amefariki dunia jana nyumbani kwake Mwananyamala Kanisani, Dar es Salaam akiwa na umri wa miaka 83.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Benedict Sichalwe, ilieleza kuwa Maurus alikuwa akisumbuliwa na saratani ya tumbo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Maurus alianza kufanya kazi mwaka 1952, katika magazeti ya Nationalist na kufanya kazi ndani na nje ya Tanzania ikiwa ni pamoja na All Radio India, mjini New Delhi, India katika miaka ya mwanzoni ya 1960.
Pia kwa zaidi ya miaka 20 alifanya kazi katika kampuni za magazeti ya Standard na Nation hadi kufikia cheo cha Naibu Mhariri Mtendaji wa gazeti la Taifa Leo.
Baada ya kurejea nchini Desemba 1983, alifanya kazi katika kampuni ya magazeti ya CCM, Uhuru na Mzalendo kwa miaka nane (1984 – 1992).
Mwaka 1992, alihamia Kampuni ya Business Times katika maandalizi ya kuanzishwa kwa gazeti la kwanza la kila siku binafsi kwa lugha ya Kiswahili, Majira. Lakini alikaa kwa muda mfupi kabla ya kuhamia katika gazeti la kwanza la michezo la Dimba.
Akiwa msanifu habari wa gazeti la Dimba, alidumu na kampuni hiyo iliyoanza kuchapisha magazeti ya Rai, Mtanzania, Bingwa, na The African kwa zaidi ya miaka 15 hadi alipostaafu. Marehemu ameacha watoto tisa na wajukuu 16.
Mungu alilaze roho yake mahali pema peponi. Amina.

0 comments:

Post a Comment