pagead2.googlesyndication.com pagead2.googlesyndication.com

Mawakili wa Kenyatta waitaka tena ICC kufuta kesi


Mawakili wanaomwakilisha Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya wamerejelea wito wao kwa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kufuta mashitaka ya uhalifu dhidi ya ubinaadamu dhidi yake, liliripoti shirika la habari la AFP siku ya Alhamisi (tarehe 10 Julai).
"Tumefika hatua ambapo hakuna ushahidi wowote" kuunga mkono mashtaka haya, wakili Steven Kay anayemuwakilisha Kenyatta aliwaambia majaji mjini The Hague siku ya Jumatano.
"Ni hoja yangu kwamba kwenye hatua hii mahakama hii ilifute suala hili," Kay aliiambia ICC, ambako Kenyatta anakabiliwa na kesi tano kutokana na jukumu lake kwenye ghasia za baada ya uchaguzi mwaka 2007-2008 zilizopelekea mauaji.
Mahakama hiyo ilikutana siku ya Jumatano kwa kile kilichoitwa mkutano wa kutambua hadhi kuangalia maendeleo ya kesi iliyoahirishwa sana ya Kenyatta, ambayo sasa imepangiwa kuanza tarehe 7 Oktoba.
Upande wa mashtaka ulitumia fursa hiyo kueleza kukerwa kwao na serikali ya Kenya, unayoituhumu kwa kushindwa kusaidia kwenye uchunguzi wake.
Timu ya utetezi ya Kenyatta imeiomba ICC kufuta mashtaka dhidi ya mteja wao mara kadhaa.
Majaji waliahirisha kesi hiyo mwezi Machi ili kuipa serikali muda wa kutafuta nyaraka za kifedha zinazohusiana na kesi dhidi ya Kenyatta. Nyaraka hizo zinajumuisha rikodi za kampuni, taarifa za kibenki, rikodi za uhamishaji wa ardhi, marejesho ya kodi, rikodi za simu na rikodi za kubadilisha fedha za kigeni, ambazo upande wa mashtaka wanatarajia zitamhusisha Kenyatta na vurugu hivyo vilivyosababisha mauaji.
Katika kesi nyingi, upande wa mashtaka "haujapokea rekodi zozote kama hizo," mwendesha mashtaka Benjamin Gumpert alisema. Kwa mujibu wa kumbukumbu za benki ya Kenyatta, waandesha mashtaka hakupata karatasi za maelezo ya fedha, lakini wakataka uhakikisho wa serikali ya Kenya kwamba "iliwasilisha akaunti zote za Bwana Kenyatta."
Mwanasheria Mkuu wa Kenya Githu Muigai aliitetea serikali, kwa kusema kuwa maombi ya nyaraka zote zilitolewa "kwa nia njema".
"Lakini pia hatuna nyenzo, wala wezo wa kiufundi au mfumo wa kisheria kuweza kufanya uchunguzi kwa niaba ya mwendesha mashtaka".
Lakini Fergal Gaynor, mwanasheria anayewawakilisha wahanga wa vurugu, aliilaumu serikali kwa "sera za makusudi za kizuizi".

0 comments:

Post a Comment