Rasimu ya Katiba
inayopendekezwa iliyowasilishwa bungeni juzi, imeondoa Ibara 28 zikiwamo
zinazowataka viongozi wa umma kutopokea zawadi kwa manufaa yao binafsi
wala kufungua akaunti ya benki nje ya nchi pasipo sababu maalumu,
Mwananchi limebaini.
Ibara ya 15 iliyokuwamo katika Rasimu ya Warioba
ilisema: “Kiongozi wa umma wakati anapotekeleza shughuli za kiserikali,
akipewa zawadi, zawadi hiyo itakuwa ni mali ya Jamhuri ya Muungano na
ilitaka Bunge kutunga sheria itakayosimamia, pamoja na mambo mengine,
thamani, kiwango, aina na uhifadhi wa zawadi kwa Jamhuri ya Muungano.
Mbali na ibara hiyo, pia Ibara ya 16 iliyohusu ufunguaji akaunti nje ya
nchi, imeondolewa.
Ibara nyingine zilizoondolewa ni pamoja na ya 17
iliyopendekeza uwazi wa mali ikimtaka kiongozi wa umma kutangaza thamani
ya mali na madeni yake mara tu baada ya kupata uongozi.
Pia Ibara ya 129 iliyokuwa inawaruhusu wananchi
kumvua madaraka mbunge ambaye atashindwa kuwasilisha au kutetea kwa
dhati hoja zinazotokana na kero za wapigakura wake au ataacha kuishi au
kuhamisha makazi yake kutoka eneo la jimbo la uchaguzi kwa zaidi ya
miezi sita bila sababu za msingi imeondolewa.
Ibara 28 zilizoondolewa
15. (1) Kiongozi wa umma wakati
anapotekeleza shughuli za kiserikali, akipewa zawadi, itakuwa ni mali ya
Jamhuri ya Muungano na ataiwasilisha kwa Katibu Mkuu Kiongozi kupitia
kwa katibu mkuu wa wizara au kiongozi wa taasisi ya Serikali
inayohusika, akiainisha:
(a) aina ya zawadi; (b) thamani ya zawadi; (c) sababu ya kupewa zawadi; na (d) mtu au mamlaka iliyotoa zawadi hiyo.
(2) Neno “zawadi” kama
lilivyotumika katika ibara hii linajumuisha kitu chochote chenye thamani
atakachopewa kiongozi wa umma katika utekelezaji wa shughuli za umma.
(3) Bunge litatunga sheria
itakayosimamia, pamoja na mambo mengine, thamani, kiwango, aina na
uhifadhi wa zawadi kwa Jamhuri ya Muungano.
16. Kiongozi wa umma-
(a) Hatafungua au kumiliki akaunti ya benki nje ya Jamhuri ya Muungano isipokuwa tu kwa namna ambayo sheria za nchi zinaruhusu; na (b) hataomba au kupokea mkopo au faida yoyote kwa namna au mazingira ambayo yanashusha hadhi au heshima ya utumishi wa umma.
17.-(1) Kiongozi wa umma
atalazimika kutangaza na kuwasilisha, ndani ya siku thelathini baada ya
kupata uongozi na baada ya kuacha uongozi, mali na thamani yake na
madeni yake katika Tume ya Maadili ya Uongozi na Uwajibikaji.
(2) Bila ya kuathiri masharti ya ibara ndogo ya (1), Kiongozi wa umma atalazimika kutangaza na kuwasilisha taarifa ya mali na madeni: (a) yake binafsi; (b) ya mwenza wake wa ndoa; na (c) ya watoto wake walio chini ya umri wa miaka kumi na nane, mara moja kila mwaka kwa Tume ya Maadili ya Uongozi na Uwajibikaji.
(3) Bunge litatunga sheria itakayosimamia, pamoja na mambo mengine: (a) ngazi au orodha ya viongozi wa umma wanaopaswa kutangaza mali na madeni yao; na (b) utaratibu wa kuwasilisha taarifa ya mali na madeni kwa Tume ya Maadili ya Uongozi na Uwajibikaji kwa mujibu wa Katiba hii.
18.-(1) Kiongozi wa umma
hatashiriki katika kufanya uamuzi wa jambo au shughuli yoyote ambayo ana
masilahi nayo yeye binafsi, mwenza wake, mtoto wake, jamaa yake, rafiki
au mtu yeyote wa karibu.
(2) Kiongozi wa umma
hatazungumzia kitu chochote katika Baraza la Mawaziri, Bunge, Kamati au
chombo kingine chochote rasmi ambacho ana masilahi nacho ya moja kwa
moja au vinginevyo, isipokuwa tu kama atatoa taarifa ya mgongano huo wa
masilahi katika chombo hicho.
(3) Itakuwa ni marufuku kwa
kiongozi wa umma kushiriki katika uamuzi unaohusu kuongeza au kuboresha
masilahi kwa namna yoyote ile yanayohusu wadhifa alionao na endapo
atashiriki, basi masharti hayo mapya yataanza kutumika kwa kiongozi wa
umma atakayekuja baada ya kiongozi husika kuondoka au kumaliza muda wa
kukaa katika nafasi ya madaraka iliyompatia fursa ya kushiriki katika
kuamua masilahi husika.
(4) Masharti ya ibara ndogo ya (3),
hayatamhusu kiongozi wa umma ambaye kutokana na asili ya nafasi ya
madaraka au aina ya kazi zake anapaswa kushiriki katika upangaji wa
mishahara au maslahi mengine ya watumishi wa umma.
(5) Kiongozi wa umma hataruhusiwa
kushika nafasi za madaraka zaidi ya moja au kutumikia mihimili ya dola
zaidi ya mmoja kwa wakati mmoja.
19. Kiongozi wa umma hataruhusiwa
kutumia au kuruhusu kutumika kwa mali yoyote ya umma, zikiwemo
zilizokodishwa kwa Serikali, kwa madhumuni ya kujipatia yeye binafsi au
kumpatia mtu mwingine manufaa yoyote.
20.-(1) Bunge litatunga sheria itakayosimamia, pamoja na mambo mengine:
(a) utaratibu wa utwaaji wa mali za viongozi wa umma zilizopatikana kwa kukiuka sheria;
(b) utaratibu wa kumwajibisha kiongozi wa umma aliyekiuka maadili na Miiko ya Uongozi; na
(c) uanzishaji wa mitalaa inayohusu Katiba, maadili na uraia, shuleni na vyuoni.
(2) Masharti yaliyoainishwa katika sehemu hii
ya Sura ya Tatu yatatumika pia kwa watumishi wa umma baada ya kufanyiwa
marekebisho stahiki.
63. Kwa ajili ya utekelezaji bora
wa shughuli za Serikali ya Jamhuri ya Muungano na kwa ajili ya mgawanyo
wa madaraka juu ya shughuli hizo baina ya vyombo vilivyotajwa katika
Ibara ya 61, Serikali ya Jamhuri ya Muungano itakuwa na mamlaka juu ya
mambo ya Muungano kama yalivyoorodheshwa katika Nyongeza ya Katiba hii.
Nchi Washirika.
64.-(1) Kwa mujibu wa Katiba hii, Nchi Washirika ni Tanganyika na Zanzibar.
(2) Serikali ya Tanganyika itakuwa na mamlaka juu ya mambo yote yasiyo ya Muungano yanayohusu Tanganyika.
(3) Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itakuwa na mamlaka juu ya mambo yote yasiyo ya Muungano yanayohusu Zanzibar.
(4) Nchi Washirika zitatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia masharti ya Katiba hii na Katiba zao.
(5) Nchi Washirika zitakuwa na
hadhi na haki sawa ndani ya Jamhuri ya Muungano na zitatekeleza majukumu
yao kwa mambo yote yasiyo ya Muungano katika mamlaka ya Nchi Washirika
kwa mujibu wa masharti yatakayowekwa na Katiba za Nchi Washirika.
67.-(1) Kila Nchi Mshirika
itateua Waziri Mkaazi atakayeratibu na kusimamia mahusiano baina ya
Serikali za Nchi Washirika na kati ya Serikali ya Nchi Mshirika na
Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
(2) Mawaziri Wakaazi watakuwa na ofisi zao na watafanya kazi wakiwa Makao Makuu ya Serikali ya Muungano.
(3) Pamoja na majukumu mengine watakayopangiwa na Serikali za Nchi Washirika, Mawaziri Wakaazi watakuwa na majukumu yafuatayo:
(a) kushughulikia mambo yasiyo ya Muungano yanayohusu ushirikiano au uhusiano wa kimataifa; na
(b) kuwa kiungo baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali za Nchi Washirika na baina ya Serikali za Nchi Washirika.
68.-(1) Serikali ya Jamhuri ya Muungano itapata
mamlaka yake kutoka kwa wananchi kupitia uchaguzi wa kidemokrasia
utakaoendeshwa na kusimamiwa na chombo kitakachopewa mamlaka na Katiba
hii, na vilevile, Serikali ya Tanganyika na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar zitapata mamlaka kupitia uchaguzi wa kidemokrasia
utakaoendeshwa na kusimamiwa na vyombo vitakavyopewa mamlaka chini ya
Katiba zao.
(2) Serikali za Nchi Washirika,
katika kutekeleza mamlaka zao, zitawajibika kustawisha mamlaka ya
wananchi kwa kugatua madaraka kwa serikali za mitaa zitakazoanzishwa kwa
mujibu wa Katiba ya Tanganyika au Katiba ya Zanzibar, kama
itakavyokuwa.
99.-(1) Kutakuwa na Waziri Mwandamizi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano atakayeteuliwa na Rais na kuthibitishwa na Bunge.
(2) Waziri Mwandamizi kabla ya
kushika madaraka yake, ataapa mbele ya Rais kiapo cha uaminifu na kiapo
kingine chochote kama itakavyoelezwa na sheria za nchi.
(3) Mtu anaweza kuteuliwa kuwa Waziri Mwandamizi endapo atakuwa na sifa zilizoainishwa katika Ibara ya 101.
(4) Bila ya kuathiri masharti ya Katiba hii, Waziri Mwandamizi atashika madaraka ya Waziri Mwandamizi hadi:
(c) siku ambapo Rais mteule ataapa kushika madaraka ya urais; au
(d) siku ambapo atafariki dunia akiwa katika madaraka; au
(e) siku atakapojiuzulu; au
(f) siku ambapo Rais atakapomteua mtu mwingine kushika madaraka ya Waziri Mwandamizi.
100.-(1) Waziri Mwandamizi atakuwa na madaraka ya udhibiti na usimamizi wa utekelezaji wa shughuli za Serikali za siku hadi siku.
(2) Bila ya kuathiri masharti ya
Katiba hii, Waziri Mwandamizi atatekeleza majukumu yote atakayoelekezwa
na Rais na katika utekelezaji wa majukumu yake atawajibika kwa Rais.
103.-(1) Mawaziri na Naibu Mawaziri hawatakuwa na haki ya kuhudhuria vikao vya Bunge isipokuwa tu:
(a) endapo kutakuwa na hoja mahususi ambayo Bunge linahitaji ufafanuzi kwa waziri husika; au
(b) endapo Serikali au waziri ataomba na kuruhusiwa kuwasilisha au kuitolea ufafanuzi hoja yoyote Bungeni.
(2) Kwa madhumuni ya ibara ndogo ya (1), waziri atakayeruhusiwa kuhudhuria kikao cha Bunge anaweza kulihutubia Bunge.
(3) Serikali ya Jamhuri ya
Muungano, chini ya mamlaka ya Rais, ndiyo itakuwa na uwezo wa kufanya
uamuzi juu ya sera za Serikali kwa jumla.
(4) Kila waziri atahudhuria vikao
vya Kamati za Bunge kila atakapohitajika na kutoa maelezo au ufafanuzi
wa suala lolote linalohusu utendaji katika nafasi ya madaraka yake.
(5) Kwa kuzingatia masharti
mengine ya jumla ya Katiba hii, mawaziri watatoa maelezo au taarifa
ambazo zinahitajika kutolewa bungeni kwa mujibu wa sheria za nchi.
106.-(1) Kutakuwa na Makatibu
Wakuu watakaoteuliwa na Rais kutoka miongoni mwa watumishi waandamizi
katika utumishi wa umma kama watakavyopendekezwa na Tume ya Utumishi wa
Umma.
(2) Kila Katibu Mkuu atakuwa
kiongozi na Mtendaji Mkuu wa Wizara ya Serikali aliyopangiwa na Rais na
atashika nafasi ya madaraka ya Katibu Mkuu na kutekeleza majukumu yake
kama itakavyoainishwa katika sheria za nchi.
(3) Rais anaweza, kwa mapendekezo
ya Tume ya Utumishi wa Umma, kumteua mtumishi mwandamizi katika
Utumishi wa Umma kuwa Naibu Katibu Mkuu.
(4) Kila Katibu Mkuu atakuwa
mshauri wa mwisho kwa Waziri kwa masuala yote ya utendaji na atatoa
ushauri kwa Baraza la Mawaziri katika vikao na kamati zitakazoitishwa na
Katibu wa Baraza la Mawaziri.
(5) Katibu Mkuu au Naibu Katibu
Mkuu hatashika madaraka yake hadi awe ameapa mbele ya Rais kiapo cha
utii na uaminifu au kiapo kingine chochote kinachohusu utendaji wa kazi
zake kitakachowekwa kwa mujibu wa sheria za nchi.
107. Kutakuwa na Kamati Maalum ya Makatibu
Wakuu itakayoongozwa na Katibu Mkuu Kiongozi ambayo itakuwa na majukumu
ya kuchambua na kulishauri Baraza la Mawaziri juu ya masuala mbalimbali
kabla ya kuwasilishwa na kufanyiwa uamuzi na Baraza hilo na itatekeleza
majukumu mengine kama itakavyopangiwa na Baraza la Mawaziri.
112.-(1) Kutakuwa na Sekretarieti
ya Tume ya Uhusiano na Uratibu wa Serikali itakayoongozwa na Katibu
akisaidiwa na Naibu Katibu ambao watateuliwa na Rais.
(2) Mtu atateuliwa kuwa Katibu au Naibu Katibu ikiwa ana sifa zifuatazo:
(a) ni mtumishi mwandamizi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano au Serikali za Nchi Washirika;
(b) ana shahada kutoka chuo cha elimu ya juu kinachotambulika kwa mujibu wa sheria za nchi; na
(c) ana mwenendo usiotiliwa shaka na jamii.
(3) Katibu na Naibu Katibu watawajibika kwa Tume na watafanya kazi na kutekeleza majukumu ya Sekretarieti.
(4) Uteuzi wa Katibu na Naibu
Katibu wa Tume utafanywa kwa kuzingatia msingi kwamba endapo Katibu
atateuliwa kutoka upande mmoja wa Jamhuri ya Muungano, basi Naibu Katibu
atateuliwa kutoka upande wa pili wa Jamhuri ya Muungano.
120.-(1) Bunge litatumia madaraka yake ya kutunga sheria kwa kujadili na kupitisha Muswada wa Sheria ambao utawekwa saini na Rais.
(2) Bila kuathiri masharti ya
Ibara ndogo ya (3), Muswada wa Sheria unaweza kuandikwa na Serikali,
Kamati ya Bunge au kikundi cha Wabunge.
(3) Wakati wa kuandaa Muswada wa
Sheria kuhusu jambo lolote la Muungano, Serikali ya Jamhuri ya Muungano
itahakikisha kwamba inawashirikisha wananchi kwa ajili ya kupata maoni
na mapendekezo juu ya muswada huo.
(4) Muswada wa sheria utahesabiwa
kuwa umepitishwa na Bunge iwapo utaungwa mkono kwa kura za wabunge
wasiopungua theluthi mbili ya wabunge wote kutoka Tanganyika na
wasiopungua theluthi mbili ya wabunge wote kutoka Zanzibar.
(5) Bila kuathiri masharti ya Ibara ndogo ya (4), Bunge litatunga Kanuni za Kudumu zitakazoweka utaratibu wa-
(a) kuwasilisha, kujadili na kupitisha Muswada wa Sheria; na
(b) utekelezaji bora wa masharti ya ibara ndogo ya (3).
129.-(1) Bila ya kuathiri
masharti ya Katiba hii, wananchi watakuwa na haki ya kumwondoa mbunge
wao madarakani, endapo mbunge atafanya moja wapo au zaidi ya mambo
yafuatayo:
(a) kuunga mkono sera ambazo zinaenda kinyume na masilahi ya wapigakura au kinyume na masilahi ya Taifa;
(b) kushindwa kuwasilisha au kutetea kwa dhati hoja zinazotokana na kero za wapigakura wake;
(c) kuacha kuishi au kuhamisha makazi yake kutoka eneo la Jimbo la Uchaguzi kwa zaidi ya miezi sita bila sababu za msingi; au
(d) mambo mengine yatakayoainishwa kwenye sheria ya nchi.
(2) Bunge litatunga sheria kuweka
masharti ya kuendesha uchunguzi kwa Mbunge atakayeshindwa kutekeleza
majukumu yake kwa wapigakura wake na utaratibu wa kumwondoa katika
ubunge.
146.-(1) Bila ya kuathiri
masharti ya Katiba hii yanayolinda na kuhifadhi uhuru wa mawazo na
majadiliano katika Bunge, ni marufuku kusema uongo bungeni na kwa sababu
hiyo, mbunge anapozungumza ndani ya Bunge ana wajibu wa kuhakikisha
kwamba anatoa kauli au maelezo kuhusu jambo au suala ambalo yeye
mwenyewe anaamini kuwa ni la kweli na siyo jambo la kubuni au la
kubahatisha.
(2) Mbunge anapokuwa akizungumza
bungeni hatahesabika wala kutafsiriwa kuwa anasema uongo iwapo anafanya
rejea ya habari kuhusu jambo lililotangazwa au lililoandikwa na vyombo
vya habari au nyaraka nyingine yoyote ambayo chanzo chake kinafahamika
au kitaelezwa na mbunge huyo.
231. Vyanzo vya mapato ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano vitakuwa:
(a) ushuru wa bidhaa;
(b) mapato yasiyo ya kodi yatokanayo na taasisi za Muungano;
(c) mchango kutoka kwa nchi washirika;
(d) mikopo kutoka ndani na nje ya Jamhuri ya Muungano; na
(e) mapato mengine.
234. Serikali za nchi washirika
zitakuwa na benki zitakazokuwa na jukumu la kutunza akaunti ya fedha za
Serikali ya nchi mshirika husika, kusimamia sera za kifedha na benki za
biashara katika mamlaka zao.
242.-(1) Kutakuwa na Tume ya
Utumishi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania itakayokuwa na
jukumu la kusimamia masuala yote ya utumishi katika Jeshi la Ulinzi la
Wananchi wa Tanzania.
(2) Bunge litatunga sheria
itakayoweka masharti kuhusu muundo, majukumu na mambo mengine yanayohusu
Tume ya Utumishi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.
244.-(1) Katika utekelezaji wa majukumu yake, Jeshi la Polisi la Jamhuri ya Muungano litazingatia-
(a) viwango vya juu vya kitaaluma na nidhamu miongoni mwa wafanyakazi wake;
(b) ulinzi na ukuzaji wa haki za binadamu;
(c) kanuni za uwazi na uwajibikaji; na
(d) kukuza uhusiano na jamii.
(2) Jeshi la Polisi, katika
kutekeleza majukumu yake, litashirikiana na vyombo vinavyohusika na
kupambana na uhalifu vya Nchi Washirika katika kufanya uchunguzi na
kushughulikia makosa ya rushwa na ufisadi.
246. Mkuu wa Jeshi la Polisi
atatekeleza kazi zake kwa uhuru, bila woga, upendeleo wala chuki na kwa
mujibu wa masharti ya Katiba hii na sheria za nchi.
247.-(1) Kutakuwa na Tume ya Utumishi wa Jeshi la Polisi itakayokuwa na jukumu la kusimamia utumishi wa Jeshi la Polisi.
(2) Katika uajiri wa askari wa
Jeshi la Polisi, Tume ya Utumishi wa Jeshi la Polisi itazingatia kanuni
na misingi ya utumishi iliyoainishwa katika Katiba hii.
(3) Bunge litatunga sheria kuweka masharti ya muundo na utekelezaji wa kazi na majukumu ya Tume ya Utumishi wa Jeshi la Polisi.
250.-(1) Bila ya kuathiri
masharti ya Sura hii, Wakuu wa Nchi Washirika wanaweza kumwagiza
kiongozi yeyote wa Jeshi la Polisi au Idara ya Usalama wa Taifa kuchukua
hatua yoyote ambayo ni muhimu kwa ajili ya kulinda au kuimarisha
usalama wa eneo lolote la Nchi Mshirika husika.
(2) Bunge litatunga sheria itakayoainisha masharti yanayohusu namna bora ya utekelezaji wa Ibara ndogo ya (1).
253.-(1) Watumishi wafuatao
hawatakuwa na haki ya kugombea, kuchaguliwa au kuteuliwa katika nafasi
ya kisiasa hadi utakapopita muda wa miaka mitatu tokea kuacha au
kustaafu nafasi ya madaraka aliyokuwa akiishikilia:
(a) Jaji Mkuu, Naibu Jaji Mkuu na Jaji wa Mahakama ya Juu wa Jamhuri ya Muungano;
(b) Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Jaji wa Mahakama ya Rufani;
(c) Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano;
(d) Spika na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano;
(e) Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama;
(f) Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano;
(g) Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano;
(h) Makatibu Wakuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano; na
(i) Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Wajumbe wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mkurugenzi wa Uchaguzi;
(j) Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Makamishna wa Tume ya Haki za Binadamu;
(k) Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Wajumbe wa Tume ya Maadili ya Uongozi na Uwajibikaji;
(l) Mwenyekiti na Wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Umma;
(m) Msajili wa Vyama vya Siasa.
(2) Bunge linaweza kutunga sheria
kuhusu aina nyingine ya watumishi wa umma ambao hawataruhusiwa kushika
nafasi za madaraka ya kisiasa kwa mujibu wa Ibara hii.
0 comments:
Post a Comment