Kashfa ya aliyekuwa Miss Tanzania, Sitti Mtemvu imechukua sura mpya
baada ya Wakala wa Uzazi, Vifo na Ufilisi (Rita) kusema kuwa
wamekamilisha upekuzi wa taarifa alizotumia kuombea cheti cha kuzaliwa
na vielelezo hivyo vimelekwa polisi vikafanyiwe kazi.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti jana, Ofisa mtendaji
mkuu wa Rita, Phillip Saliboko na Meneja masoko na mawasiliano, Josephat
Kimaro walisema upekuzi wa nyaraka zilizotumiwa na Sitti uliofanywa na
wanasheria wao, tayari umekamilika.
“Kazi yetu (Rita) tumeimaliza na upekuzi wa taarifa za Sitti
umekamilika na kinachofuata sasa ni kupeleka nyaraka hizo kwenye mamlaka
inayohusika ambayo ni polisi, wao ndio wataamua nini cha kufanya,”
alisema Kimaro.
Alisema Rita haiwezi kumhukumu moja kwa moja mrembo huyo kuwa
alighushi nyaraka na kudanganya ili apate cheti hicho cha kuzaliwa
kilichotolewa na Rita Septemba na badala yake wanapeleka vielelezo
walivyonavyo polisi ili nao wavifanyie kazi.
“Sisi (Rita) jukumu letu lilikuwa ni upekuzi wa nyaraka, kazi ambayo
imefanywa kwa ustadi mkubwa na jopo la wanasheria wetu na hadi sasa
imekamilika na kinachofuata ni kuzipeleka nyaraka hizo polisi ambao wao
ndiyo wenye jukumu la uchunguzi na kumchukulia hatua Sitti au la,”
alisema.
Wakati huohuo, Saliboko akieleza kuwa bado wana changamoto ya baadhi
ya watu kudanganya taarifa zao ili wapate vyeti vya kuzaliwa na
kusisitiza kuwa wanaandaa mfumo maalumu ili kukomesha udanganyifu huo.
“Tukibaini mtu ametumia udanganyifu ili kupata cheti, kwanza huwa
tunamfutia cheti chake na taratibu nyingine za kisheria zinafuata.
Tunafanya hivyo kwa watu wote wanaokuja kuomba vyeti kwetu na siyo kwa
Miss Tanzania peke yake japo hili la Sitti tunaiachia mamlaka husika
ifanye kazi yake,” alisema.
Sitti Mtemvu aliingia kwenye kashfa ya kudanganya umri wake na
nyaraka zake mbalimbali zilionyesha alizaliwa 1989, umri ambao
umepitiliza ule unaotakiwa kwa mshiriki wa mashindano ya Miss Tanzania,
huku cheti chake kikionyesha alizaliwa 1991, hivyo kulazimika kuvua taji
hilo.
Wakati huohuo, mrembo aliyevikwa taji la Miss Tanzania nambari mbili,
Lilian Kamazima anatarajiwa kuwasili leo mjini Arusha na kupokewa kwa
shangwe akiwa na taji lake.
Taarifa iliyotolewa na mkurugenzi wa Kampuni ya Mwandago
Entertainment Ltd, Faustine Mwandago iliyosimamia ushindi wake ngazi ya
kanda ilisema kuwa mrembo huyo atawasili kwenye Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia) saa 6:00 mchana.
Mwandago alisema kuwa mrembo huyo atapokelewa na wenyeji wake,
wakiwamo wazazi wake na kisha kupanda gari la wazi ili kuwapa fursa
wakazi wa Arusha kumshuhudia.
Alisema kuwa mara baada ya kuwasili Arusha atapelekwa moja kwa moja
nyumbani kwao, Sakina ili kushiriki hafla aliyoandaliwa na wazazi wake
pamoja na ndugu, jamaa na marafiki.
Wakazi wa Arusha wametakiwa kujitokeza kwa wingi kumpokea mrembo huyo
kwa lengo la kumpa moyo na kulikaribisha taji hilo mara baada ya ukame
wa muda mrefu wa kupata taji la Miss Tanzania.
0 comments:
Post a Comment