pagead2.googlesyndication.com pagead2.googlesyndication.com

Wiki ngumu kwa Ngeleja, Chenge

 
Dar es Salaam. Hii ni wiki ngumu kwa wenyeviti watatu wa Kamati za Bunge ambao wanatakiwa kuachia nafasi za uongozi kutokana na kuhusika katika kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow ya Sh306 bilioni.
Wenyeviti wanaotakiwa kuvuliwa uongozi na Wajumbe wa Kamati husika ni Andrew Chenge (Bajeti) William Ngeleja (Katiba) na Victor Mwambalaswa (Nishati na Madini).
Katika mkutano wa 16 na 17 wa Bunge liliazimia watu walioshiriki katika kashfa hiyo wakiwamo viongozi wa kamati hizo tatu, wachukuliwe hatua za haraka na Kamati husika za Bunge kabla ya kuanza kwa mkutano wa 18 wa Bunge, Januari 27 mwaka huu.
Licha ya maazimio hayo ya Bunge, Kamati hizo zimeshindwa kutekeleza uamuzi huo huku wenyeviti hao wakiendelea kujitambulisha kuwa ni wenyeviti wa Kamati hizo jambo ambalo limekuwa gumzo tangu kuanza kwa vikao hivyo Januari 13 mwaka huu.
Januari 15 mwaka huu, Kamati ya Nishati na Madini iliyokuwa chini ya Makamu Mwenyekiti, Jerome Bwanausi ilikutana na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) na wakati wa kujitambulisha Mwambalaswa alijitambulisha kuwa ni mwenyekiti wa kamati hiyo.
Katika kikao kimojawapo cha Kamati ya Bajeti wiki iliyopita, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Dk Festus Limbu aliongoza na wakati kikao kikiendelea, Chenge alikuwa pembeni.
Hata hivyo, siku mbili baadaye, Chenge alisema kuwa hakuwahi kujitangaza kujiondoa katika nafasi ya uenyekiti lakini anashangaa kutangazwa katika vyombo vya habari.
Wiki hii pia, Ngeleja aliliambia gazeti hili kwamba anaendelea kushikilia nafasi hiyo kwa maelezo kuwa uchunguzi wa suala hilo bado unaendelea, ikithibitika ndipo Bunge litachukua uamuzi ambao alidai yupo tayari kuutekeleza.
Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashilillah alisema, “Kazi ya Spika (Anne Makinda) ni kusimamia utekelezaji wa maazimio hayo na jukumu la kuwaondoa lipo mikononi mwa kamati husika lakini hata hivyo bado kuna muda ambao kamati hizo zinaweza kutekeleza azimio hilo.”
Akinukuu azimio hilo Dk Kashilillah alisema, “Kamati husika za kudumu za Bunge zichukue hatua za haraka na kwa vyovyote vile kabla ya mkutano wa 18 wa Bunge, kuwavua nyadhifa zao kwenye kamati husika za kudumu za Bunge.”
Aliongeza: “Sasa kwa hili mimi na Spika tunaingiaje?, Spika yeye anasimamia utekelezaji wa maazimio hayo na kama itashindikana atachukua uamuzi wa kuwahamisha kamati jambo ambalo (mwenyekiti) akihamishwa anapoteza sifa ya kuwa mwenyekiti lakini kwa sasa waulizeni wao wenyewe wanafanya lini chaguzi hizo.”
Wiki ya mwisho
Vikao vya kamati hizo za Kudumu za Bunge, vitamalizika Ijumaa wiki ijayo hivyo basi zimesalia siku tano kwa wajumbe wa kamati hizo kuamua kunyoa au kusuka katika utekelezaji wa azimio hilo la Bunge.
Kamati hizo za Kudumu za Bunge, vitamalizika vikao vyake Ijumaa ijayo ikiwa ni siku tano kwa wajumbe wa kamati kufikia utekelezaji wa azimio hilo la Bunge.
Katika kuhitimisha vikao hivyo wiki hii, baadhi ya kamati; Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) itajadili Hesabu za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Hesabu Jumuishi za Taifa na kujadili taarifa ya Kamati ndogo ya Hesabu za Serikali kuhusu na ukusanyaji mdogo wa kodi za ardhi unaoikabili Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Pia, itakutana na viongozi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na kupitia rasimu ya taarifa ya mwaka ya utekelezaji wa shughuli za kamati kwa mwaka 2014/15.
Kamati ya Bajeti itapokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo hadi kufikia Novemba, 2014 na kupata mrejesho wa maoni ya wabunge kuhusu mapendekezo ya mpango wa maendeleo.
Pia, itapokea taarifa ya utekelezaji wa bajeti hadi kufikia Desemba 31, 2014 hususan makusanyo na mgawanyo wa fedha na kupata mrejesho kutoka kwa walipa kodi kuhusu mwenendo wa kodi mbalimbali.
Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala itapokea maoni ya wadau kuhusu Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali ya mwaka 2014 na majumuisho ya maoni ya wadau ili kupata maoni ya Kamati.
Mbali na muswada huo, kamati hiyo itajadili Muswada wa Sheria ya Kukabiliana na Maafa ya mwaka 2014.

0 comments:

Post a Comment