
Ushahidi wa mambo yote unaonesha
kuwa hali nchini Libya imefikia hatua ya kutisha. Misri imeanzisha vita
dhidi ya nchi hiyo huku kundi la Daesh nalo likiendelea kufanya jinai
zake nchini humo. Kutekwa nyara raia 35 wa Misri ni habari nyingine
mbaya iliyoakisiwa kutokea Libya. Umoja wa Ulaya kwa upande wake
umesema, umeingia wasiwasi kutokana na hali ya hatari iliyoshadidishwa
na jinai za kundi la Daesh huko Libya, suala ambalo ni hatari pia kwa
usalama wa nchi za Ulaya. Umoja huo umezungumzia wajibu wa kuchukuliwa
hatua za pamoja za wanachama wake ili kupambana na mgogoro wa Libya.
Hata Federica Mogherini, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya
amesema kuwa, hatua za kijeshi ni miongoni mwa njia zinazoweza kutumiwa
ili kutuliza hali ya mambo nchini Libya. Tab'an amesema kuwa, hatua hiyo
haiwezi kuchukuliwa bila ya idhini ya Umoja wa Mataifa. Hata hivyo
jambo moja halikanushiki, nalo ni kwamba, jambo lolote lile linaweza
kutokea nchini Libya, kwani hali katika nchi hiyo imevurugika mno. Jeshi
la Anga la Libya limetangaza kufunga anga ya nchi hiyo. Wanajeshi wa
Misri wamepelekwa kwenye mpaka wa Libya wakiwa katika tahadhari kubwa.
Si hayo tu, lakini pia ndege za kijeshi za Misri zimefanya mashambulizi
katika maeneo ya kundi la Daesh kwenye mji wa bandari wa Derna nchini
humo, huku jeshi la Libya nalo likifanya mashambulizi dhidi ya kundi
hilo kwenye miji ya Benghazi na Sirte. Kwa upande wa miundombinu ya
Libya pia, hali ni mbaya mno. Hata shirika la taifa la mafuta la nchi
hiyo huenda likasimamisha kusafirisha nje mafuta. Ni wazi kuwa Libya
hivi sasa imo kwenye hali mbaya mno; hali ambayo tunaweza kusema kuwa,
imechochewa na baadhi ya nchi za Magharibi. Madola hayo ni yale ambayo
yaliona manufaa yao yamo katika kuitelekeza Libya baada ya kupinduliwa
utawala wa Kanali Muammar Gaddafi. Baada ya kufanya mashambulizi ya
kikatili yaliyoangamiza takriban miundombinu yote, nchi hizo wanachama
wa NATO ziliitelekeza Libya zikihakikisha kuwa silaha zimeenea mikononi
mwa watu na makundi yenye uhasama ambapo kila kundi lilikuwa
linapingania kuwa na nguvu zaidi kuliko kundi jingine. Baadhi ya duru za
kisiasa zinaamini kuwa shirika la kijeshi la NATO limeitumbukiza kwa
makusudi Libya katika hali hiyo mbaya. Duru hizo zinaamini kuwa, madola
ya Magharibi yanaweza kirahisi sana kudhibiti hali ya mambo nchini Libya
kama yatataka kufanya hivyo. Ni jambo lililo wazi kwamba uzembe wa
makusudi unaofanywa na nchi za Magharibi wa kuiacha Libya izame kwenye
mgogoro wa miaka mitatu sasa, si jambo linalofanyika vivi hivi. Hivi
sasa moja ya tatizo kubwa la kiusalama la Libya ni Daesh, kundi la
kigaidi ambalo limeingia hadi katika kitovu cha mji mkuu Tripoli. Kundi
jingine ni la Fajr la wapinzani wa serikali halali ya Libya ambalo
limeungana na Daesh ili kujiimarisha. Swali linalojitokeza hapa ni
kwamba, Ni vipi Libya itaweza kupambana na makundi yenye silaha likiwemo
kundi la Daesh linalopata msaada wa kila namna kutoka Magharibi na
kutoka katika baadhi ya nchi za Mashariki ya Kati wakati nchi hiyo haina
jeshi lenye nguvu? Itaweza vipi kupambana na makundi hayo wakati ina
serikali mbili na mabunge mawili hasimu? Kesho Jumatano, tarehe 18
Februari, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litaitisha kikao
kuzungumzia mgogoro wa Libya. Amma swali jingine linalojitokeza hapa ni
kwamba Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na nchi za Magharibi
zilikuwepo wapi miaka yote hii mitatu ya mgogoro wa Libya ambao sasa
umeingia kwenye hali mbaya sana?
0 comments:
Post a Comment