Takwa la hivi karibuni la serikali ya Cuba la kutaka
kurejeshewa Ghuba ya Guantanamo, limekabiliwa na radiamali hasi kutoka
kwa Marekani. Katika uwanja huo, ikulu ya Marekani (White House)
imetangaza kuwa juhudi zilizofanywa kwa ajili ya kuboresha uhusiano kati
ya Marekani na Cuba hazitafika kiwango cha kuifanya Washington
iirejeshee Havana Ghuba ya Guantanamo huko kusini mashariki mwa Cuba.
Msemaji wa White House, Josh Ernest, amesema japokuwa Rais Barack Obama
anaamini kuwa, jela ya Guantamano inapaswa kufungwa, lakini hana nia ya
kufunga kituo cha jeshi la majini la Marekani kilichopo katika eneo
hilo.
Eneo la Ghuba ya Guantanamo linalodhibitiwa na Marekani
lina kituo cha jeshi la majini la Marekani pamoja na jela ya kijeshi ya
nchi hiyo, na miezi minne tu baada ya mashambulizi ya Septemba 11 mwaka
2011, Washington iliwapeleka washukiwa wa ugaidi katika jela hilo. Ghuba
ya Guantanamo inakaliwa kwa mabavu na Marekani tangu nchi hiyo na Cuba
ziliposaini mkataba mwaka 1903. Hata hivyo Rais Raul Castro wa Cuba
Jumatano iliyopita alitangaza kuwa, kurejesha udhibiti wa eneo hilo
lenye ukubwa wa kilomita mraba 116 kwa serikali ya Havana ni sharti la
kuhuisha uhusiano kati ya nchi hizo mbili.
Inavyoonekana ni kuwa, mchakato wa kuhuisha uhusiano wa
Marekani na Cuba unakabiliwa na vizuizi vingi kinyume na ilivyotarajiwa
hapo awali. Baadhi ya vizuizi hivyo vinasababishwa na Marekani na
vingine ni kutoka upande wa Cuba. Pamoja na hayo ni wazi kwamba kiwango
cha vizuizi vya Marekani katika mchakato huo ni kikubwa mno kulinganisha
na Cuba. Pamoja na hayo yote, takwa la Cuba la kurejeshewa ardhi ya
nchi hiyo ambayo inashikiliwa na Marekani kwa zaidi ya miaka 112 sasa,
ni takwa halali na lililotolewa kwa misingi ya haki ya kujitawala
serikali ya Cuba.
Wakati huo huo hatua ya Marekani ya kukataa takwa hilo ni
hatua isiyo ya kirafiki na ishara kwamba, Washington ingali inataka
kuweko kijeshi katika bahari ya Caribbean. Aidha kuendelea shughuli za
jela ya Guantamano ni tatizo kwa Marekani yenyewe. Kwa sasa hakuna
mpango wa kuifunga jela hiyo, na kama alivyotamka hivi karibuni waziri
wa zamani wa ulinzi wa Marekani Chuck Hagel kwamba, hakuna matumaini ya
kufungwa jela ya Guantanamo kabla ya kumalizika kipindi cha uongozi wa
Barack Obama. Rais Obama wa Marekani katikati ya mwezi Disemba mwaka
jana alichukua hatua kadhaa kwa ajlili ya kufufua uhusiano wa
kidiplomasia na kupunguza vikwazo vya kibiashara ilivyokuwa imewekewa
Cuba na kwa msingi huo akahitimisha miaka zaidi ya 54 ya uhusiano wa
kiadui kati ya nchi mbili hizo. Marekani imekuwa na miamala ya kiadui
dhidi ya Cuba tangu baada ya ushindi wa mapinduzi ya nchi hiyo chini ya
uongozi wa Fidel Castro, na Washington ilizidisha vikwazo vya kiuchumi
dhidi ya nchi hiyo baada ya kushindwa kuipindua serikali ya kimapinduzi
ya Cuba katika tukio la Ghuba ya Nguruwe. Mwaka 1962 Cuba pia
iliondolewa katika Jumuiya ya Nchi za Amerika kutokana na mashinikizo ya
Marekani na kuanzia mwaka 1960 Washington ilianza kuiwekea Havana
vikwazo vikubwa katika nyanja za biashara, uchumi na fedha.
Japokuwa baadhi ya wachambuzi wa mambo walidhani kuwa,
mchakazo wa kuboresha uhusiano wa Marekani na Cuba ungeshika kasi zaidi
baada ya Rais Barack Obama wa Marekani kutoa tangazo la kurejeshwa
uhusiano wa kawaida na Havana na suala hilo kupasishwa katika Bunge la
Cuba, lakini inaonekana kuwa kuna vizuizi vikubwa katika uwanja huo.
Moja ya vizuizi hivyo ni kuendelea uingiliaji wa Marekani katika masuala
ya ndani ya Cuba. Ndani ya Kongresi ya Marekani pia kuna upinzani mkali
dhidi ya kuhuishwa uhusiano kati ya nchi mbili hizo.
0 comments:
Post a Comment