pagead2.googlesyndication.com pagead2.googlesyndication.com

Kama Movie Vile: Majambazi walivouliwa Vikindu

Dar es Salaam. Siku kadhaa baada ya ofisa wa juu kuuawa kwa kupigwa risasi na watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi, Jeshi la Polisi limetoa taarifa ya kuthibitisha tukio hilo, huku likibainisha kuwa limekamata idadi kubwa ya bunduki, risasi, pingu na vifaa vingine katika msako wa wahusika wa mauaji hayo.
Jeshi hilo pia limesema watu watatu wanaotuhumiwa kuwa ni majambazi waliuawa wakati wa msako huo uliofanyika baada ya askari wanne kuuawa wakati wakibadilishana lindo la tawi la benki ya CRDB lililoko Mbande Agosti 23, na siku nne baadaye ofisa huyo wa cheo cha kamishna msaidizi wa polisi, Thomas Njuki, kuuawa katika mapambano yaliyotokea Mtaa wa Vikindu Mashariki mkoani Pwani.
Baada ya mauaji hayo ya ofisa huyo, Jeshi la Polisi liliahidi kuwa lingetoa taarifa kamili ya tukio hilo siku iliyofuata lakini halikufanya hivyo hadi jana.
Kamanda wa Polisi wa Kanda ya Dar es Salaam, Simon Sirro aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa jeshi lake limekamata bunduki 23, risasi 835, fulana maalumu za kuzuia risasi (bullet proof) tatu, sare moja ya polisi, pingu 48 na redio 12 za mawasiliano ambazo alisema zilikuwa zikitumiwa na majambazi katika kufanya uhalifu.
Alisema zaidi ya watuhumiwa saba wamekamatwa kuhusiana na mauaji ya askari polisi hao watano.
Kamanda Sirro alisema Septemba 3, majira ya saa 8:00 mchana askari wake waliweka mtego na kufanikiwa kukamata majambazi watatu ambao wanaishi maeneo ya Mbagala, Keko na Kawe.
Alisema waliweka mtego huo wakati wakifuatilia tukio la ujambazi lililotokea Agosti 29 kwenye jengo la Sophia House lililoko Barabara ya Chang’ombe karibu na Veta ambako majambazi kumi walivamia ofisi za kampuni ya Matrix International na kupora Sh35 milioni.
Amesema walipowahoji, watu hao watatu walikiri kuhusika katika matukio tofauti ya ujambazi wa kutumia silaha na kueleza kuhusu silaha walizo nazo na nyingine zilizofichwa msitu wa Vikindu.
“Majambazi hawa walikiri kuwa na silaha kwenye nyumba waliyokodi eneo la Mbezi Beach, ndipo askari walienda kufanya upekuzi na kupata silaha mbalimbali,” alisema Kamanda Sirro.
Amesema katika nyumba hiyo wamekuta silaha 23 kati ya hizo, tatu ni za kivita na 16 ni bastola. Pia alisema walikuta risasi 835, fulana tatu za kuzuia risasi (bullet proof) tatu, sare ya polisi, pingu 48, redio 12 za mawasiliano na magazini tisa. Vitu vingine vilivyokutwa ni panga, nyundo kubwa, mtambo wa kuchukulia matukio (CCTV), mtarimbo mmoja ambao Sirro alisema hutumika kuvunjia milango, gari aina ya Toyota Noah na jingine aina ya Toyota Alphard.
Sirro pia amesema katika mahojiano nao, majambazi hao walisema silaha nyingine walificha Msitu wa Vikindu wilayani Mkuranga, ndipo askari hao walipoambatana na watuhumiwa hao kwenda eneo hilo.

0 comments:

Post a Comment