MWANADADA
anayetamba katika tasnia ya muziki wa mduara pia katika uigizaji wa
filamu, Snura Mushi ‘Snura’ amesema ameamua kupunguza kukatika viuno
katika video za nyimbo zake kutokana na kukosolewa na hata kutolewa
kwenye baadhi ya vipengele vya tuzo za Kilimanjaro Music Awards (KTMA).
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Snura alisema hata kabla
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) hawajapiga stop ushiriki wa nyimbo
zake kwenye kinyang’anyiro hicho, alikuwa ameshabadilika kwa kuwa tayari
video yake ya ‘Nimevurugwa’ ilikuwa imefungiwa.
Alisema yeye ameshabadilika kabla hata hatujafika huko kwenye Kili
kwa sababu ‘Nimevurugwa’ ilifungiwa muda kidogo kabla ya Kili kuikosoa
na kwamba wimbo wake wa ‘Ushaharibu’ alikuwa ameshafanya video ikitoka
watu watajua ni jinsi gani ameweza kubadilika.
Ameeleza kuwa si kwamba kwenye ‘Ushaharibu’ hakutakuwa tena na
uchezaji ule wa kukata viuno bali atapunguza kidogo, akitofautisha na
video nyingine zilizotangulia.
“Kweli kwenye video si kwamba hakuna kabisa kiuno ila nimepunguza,
nimeacha viuno ambavyo nina uhakika kwamba siwezi kufungiwa jamani,
sijakatika kama kwenye ‘Nimevurugwa’, wakati nafanya wimbo wa
‘Nimevurugwa’ sikuhisi kama ninaweza nikafungiwa kiukweli, laiti kama
ningejua nisingeweza kufanya vile, mimi nilichukulia kama ni ubunifu na
utundu wangu ndiyo maana nikafanya vile,” alisema Snura.
Hata hivyo, amedai kuwa kuna mashabiki wake ambao wangependa kuona
anacheza kama alivyokuwa akicheza zamani, hivyo ataendeleza mchezo huo
kwenye shoo zake atazofanya kwenye kumbi mbalimbali.
freemedia
0 comments:
Post a Comment