Dar es Salaam. Aliyekuwa
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema
wanasiasa wanaomtuhumu kwa kumsaliti Baba wa Taifa, Mwalimu Julius
Nyerere kuhusu Muungano, ndiyo wasaliti kwa kuwa waliingiza kwenye
Katiba, mambo yanayokinzana na makubaliano ya Muungano huo.
Jaji Warioba amesema usaliti huo ni pamoja na
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuondoa mamlaka ya Bunge la Muungano
katika utungaji wa sheria, kuitambua Zanzibar kuwa nchi inayojitegemea
na kuongeza mambo ya Muungano bila kufuata Katiba.
Ametoa kauli hiyo kujibu mwendelezo wa lugha za
kejeli na matusi anazorushiwa na baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la
Katiba wengi kutoka CCM na baadhi ya viongozi wa Serikali baada ya Tume
aliyoiongoza kupendekeza muundo wa serikali tatu.
Akizungumza juzi usiku katika kipindi cha Dakika
45 kinachorushwa na Kituo cha Televisheni cha ITV, Jaji Warioba alisema
viongozi wa pande mbili za Muungano wanaomtuhumu, ndiyo waliouvuruga
Muungano huo
“Mwalimu aliacha Bunge likiwa na mamlaka kamili,
aliacha nchi ni moja, aliacha mambo ya Muungano 11 sasa yamekuwa ni 22,
kwa bahati nzuri Rais Jakaya Kikwete alieleza bungeni hilo kwamba mambo
hayo yaliongezekaje,” alisema na kuongeza:
“Katika kubaini kuongezeka kwa mambo ya Muungano
ndivyo ilikuwa inapunguza mamlaka kwa Zanzibar, mambo 11 yaliyoachwa na
mwalimu yaliingizwa kikatiba lakini haya yaliyoongezeka yalipatikana
kienyeji.”
Jaji Warioba alisema enzi za uhai wake, Mwalimu
Nyerere aliheshimu na kuilinda Katiba hivyo, walioivunja ndiyo wasaliti
wa Muungano.
“Sasa kati ya mimi na wao ni nani msaliti kwa
Mwalimu, angekuwapo (Mwalimu) ni yupi angeonekana msaliti wa Serikali ya
Muungano? Wao ndiyo wameuvuruga, alichokiacha Mwalimu ni tofauti na
kinachoonekana kwa sasa,” alisema Jaji Warioba.
Kuhusu Bunge
Jaji Warioba alisema mipango mingi ya maendeleo inayopangwa ndani ya Bunge la Muungano inatekelezwa upande wa Bara pekee.
“Si hivyo tu, Bunge hilo linajadili mambo ya Bara
tu na halihusishi upande wa Zanzibar. Zanzibar nayo inajadili mambo yake
na kujiamulia lakini jina la Bunge hilo ni Muungano,” alisema Jaji
Warioba.
Kutokana na mazingira hayo, Jaji Warioba alisema
Zanzibar iliamua kuondoa mamlaka ya Bunge hilo katika utungaji wa sheria
kupitia Baraza la Wawakilishi Zanzibar.
“Katiba ya Jamhuri ya Muungano inasema sheria zinazotungwa
katika Bunge hilo zitatumika ndani ya pande zote za Muungano, lakini
Zanzibar wakabadilisha hilo kupitia Katiba yao wakasema sheria zote
zitakazotungwa ndani ya Bunge hilo, lazima zipitiwe tena na Baraza la
Wawakilishi,” na kuongeza: “(Zanzibar) Hawakuishia hapo, wakafanya
mabadiliko ya Katiba mwaka 2010 iliyovunja Katiba ikiitambua Zanzibar
kama nchi kamili, ikaondoa mamlaka ya Rais wa Jamhuri kugawa wilaya na
mikoa kwa Zanzibar tofauti na Katiba ya Muungano, kwa maana hiyo
Zanzibar ikavunja nguvu ya Bunge la Muungano.”
Aidha, alisema hatua hiyo ilionekana kuuvunja
Muungano kwa vitendo baada ya kuvunja mamlaka ya Rais na kutambua marais
kamili katika nchi mbili tofauti.
“Kwa kawaida nchi inakuwa na amri jeshi mkuu mmoja
ambaye anapigiwa mizinga 21, Jeshi la Muungano linapiga mizinga kwa
marais wawili kitu ambacho hakiwezekani,” alisema.
Malalamiko ya Watanganyika
Jaji Warioba alisema Kwa upande wa Tanzania Bara,
walibaini malalamiko ya Watanganyika kuwa ni pamoja na kukosa fursa
mbalimbali ndani ya Zanzibar. “Watu wa bara nao wanasema Zanzibar
inashiriki Bunge la Muungano, inakagua miradi ya bara na kuihoji lakini
wao hawana nguvu ya kushiriki mambo hayo kwa upande wa Zanzibar,”
alisema.
Aliongeza: “Mbaya zaidi wanasema Wazanzibari
wanaweza kumiliki ardhi na kupata uraia kwa upande wa bara lakini haki
hizo haziwezi kupatikana kwa Mtanganyika, njia pekee tukaona ni vyema
Zanzibar nayo ilete mambo yake ndani ya Muungano lakini ikashindikana.”
Hoja ya takwimu
Jaji Warioba aliwataka wajumbe wa Bunge
wasihangaike na takwimu badala yake wajibu maswali yaliyojitokeza kutoka
kwa washirika wa Muungano.
“Takwimu siyo tatizo, sisi hatukufanya jambo
jipya, ila ilikuwa ni kama marudio tu ya Tume ya Nyalali, wanahoji
takwimu hizo je, hawakuona dosari kwa takwimu za maoni ya asilimia 20
kwa jaji Nyalali?
Alisema Tume yake ilizunguka nchi nzima ikiwa na
waandishi waliorekodi kwa tepu, video na maandishi kwa ajili ya kuweka
kumbukumbu katika mtandao wa Tume.
mwananchi
0 comments:
Post a Comment