Dar es Salaam. Chanzo cha kifo cha Balozi wa
Malawi nchini, Flossy Gomile-Chidyaonga kimefahamika. Uchunguzi wa
madaktari umebaini kuwa kilitokana na moyo wake kushindwa kufanya kazi.
Balozi Gomile-Chidyaonga alifariki ghafla Ijumaa iliyopita na mwili wake umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, John Haule alisema jana kuwa taarifa za
madaktari zinaonyesha kuwa mshipa mkubwa wa moyo wake ulipasuka na
kusababisha kifo chake.
“Jana (juzi) madaktari waliufanyia uchunguzi mwili
wake (postmortem) na kubaini kuwa mshipa mkubwa wa moyo ulipasuka na
kutiririsha damu nyingi mwilini hali iliyosababisha kifo chake,” alisema
Haule.
Haule alisema Serikali ilikuwa karibu na familia
ya marehemu tangu ilipopata taarifa ya kuzidiwa kwake na ilishirikiana
vyema na ndugu na jamaa kumpeleka katika Hospitali ya Aga Khan na hatimaye Muhimbili.
“Kesho (leo Jumatatu) kati ya saa 3:30 na saa 4:00 asubuhi itafanyika misa ya kumwombea katika Ukumbi wa Mwalimu Julius Nyerere pia heshima za mwisho zitatolewa hapo.
Baadaye mwili wa marehemu utapelekwa Uwanja wa Ndege kwa ajili ya safari ya kwenda Malawi Jumanne,” alisema.
Marehemu anatarajiwa kuzikwa nyumbani kwake huko Blantyre, Jumatano na Haule alisema Serikali ya Tanzania itashiriki kikamilifu katika tukio hilo.
Juzi, Rais Jakaya Kikwete alimtumia salamu za rambirambi Rais wa Malawi, Joyce Banda kutokana na msiba huo mkubwa.
Alisema Balozi Gomile-Chidyaonga alikuwa kiungo
muhimu katika kukuza uhusiano baina ya Malawi na Tanzania na kwamba kifo
chake kimeshtusha kwa kuwa bado alikuwa anahitajika katika nchi hizo
mbili.
“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za msiba wa Balozi Gomile-Chidyaonga ni huzuni kwetu sote,” alisema.
Rais Kikwete.
huku akimwomba Rais Banda amfikishie salamu zake na za
Watanzania kwa jumla kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa na Wamalawi
wote.
Kabla ya kuwa Balozi Tanzania, Gomile-Chidyaonga
aliwahi kuwa Kaimu Balozi wa Malawi nchini Uingereza kabla ya kumwondoa
kutokana na mgogoro wa kidiplomasia baina ya nchi hizo.
Marehemu pia aliwahi kuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Malawi.
Mwananchi
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment