BAADHI
ya madereva wa Kampuni ya Usafiri Dar es Salaam (UDA), jana waligoma
kufanya kazi kwa muda wakipinga agizo la kupeleka hesabu ya sh. 205,000
wakidai kuwa haziwezi kupatikana kutokana na ushindani wa kibiashara.
Sambamba na hilo, pia wamedai kupandishwa mshahara kutoka sh. 150,000 hadi 350,000 kwa mwezi.
Mmoja wa viongozi wa madereva hao wa kituo cha Mbagala, akizungumza
kwa sharti la kutotajwa jina, alisema wanautaka uongozi wa UDA kusikia
kilio chao, kinyume chake wataendelea kuvutana kila mara.
Alisema hesabu hiyo haiwezi kupatikana baada ya kampuni hiyo kuingia
makubaliano na Mamlaka ya Usafiri Nchi Kavu na Majini (Sumatra), ambako
baadhi magari hivi sasa yamepigwa mkanda kuonyesha yanakokwenda, kitendo
kinachowazuia kupita njia yoyote kama ilivyokuwa awali.
“Hata hivyo baada ya kugoma, walifika baadhi ya viongozi na
kutushauri tukafanye kazi kwa makubaliano kuwa kwa siku ya leo tupeleke
sh 130,000 kwa sababu tulichelewa kuanza kazi…tena tukienda njia yoyote
ambako hata tungekamatwa kampuni ingehusika yenyewe,” alisema dereva
huyo.
Akizungumzia mshahara, dereva huyo alisema wanaitaka kampuni hiyo
iongeze mshahara kutoka sh 150,000 hadi 350,000 kwani unaolipwa sasa
haukidhi mahitaji.
“Mshahara tunaolipwa hautoshi, hata hivyo haulipwi kwa wakati kitendo ambacho ni kawaida kila mwezi,” alisema.
Aliongeza kuwa waliahidiwa na kiongozi huyo ambaye walishindwa kupata
jina lake kuwa madai yao yatashughulikiwa na kupatiwa ufumbuzi ndani ya
miezi miwili.
Alipotafutwa Msemaji wa Kampuni hiyo, George Maziku ili kutoa
ufafanuzi, alisema kuhusu makubaliano ya Sumatra na UDA hayaathiri
chochote kuhusu hesabu hiyo.
Alisema viwango hivyo hawakuviweka tu wakiwa mezani, bali vilifanyiwa
utafiti na wataalamu wa kampuni na kubaini kuwa ni sahihi na
kinapatikana.
Maziku, alisema suala la kupunguza kiwango hicho wasahau, kwa sababu
hesabu hiyo inapatikana kutokana na utafiti wa kampuni na kwamba
wanapata fedha nyingi zaidi ya hizo kwa siku.
Kuhusu kuchelewa mshahara, Maziku alisema kuwa suala hilo lilichangiwa na mifumo ya kibenki hata hivyo hivi sasa limekwisha.
0 comments:
Post a Comment