Na Bakari Kiango,
Wakati Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Wilfred Lwakatare anatarajiwa
kufikishwa mahakamani leo, jana mchana ofisi za makao makuu ya chama
hicho zilipekuliwa na polisi na kuondoka na nyaraka mbalimbali.
Tukio hilo lilitokea jana ikiwa ni mwendelezo wa
upelelezi wa tuhuma zinazomkabili Lwakatare ambazo zinazomhusisha na
picha ya video iliyorushwa kwenye mitandao ya kijamii. Lwakatare
alikamatwa Jumatano iliyopita akihusishwa na picha hiyo iliyomwonyesha
Lwakatare akiwaelekeza watu ambao hawakuonekana, kufanya vitendo vya
uvunjifu wa amani au uhalifu.
Upekuzi katika ofisi
Polisi hao wakiwa na Lwakatare na mmoja wa
mawakili wake, Nyaronyo Kicheere walikwenda kwenye ofisi za Chadema saa
9.00 alasiri kwa ajili ya kufanya upekuzi.
Upekuzi huo uliendeshwa zaidi kwenye ofisi za
Lwakatare kwenye Makao Makuu ya Chadema yaliyoko Mtaa wa Ufipa,
Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Upelelezi wa kesi hiyo unaongozwa na Kamishna
Msaidizi wa Polisi (ACP), Obadia Jonas. Uchunguzi wa gazeti hili
unaonyesha kuwa upekuzi huo ulikuwa na lengo la kupata hati zenye
mwandiko wa Lwakatare ili kufananisha na nyaraka mbalimbali walizonazo
polisi. Kwa nyakati tofauti, Nyaronyo Kicheere na Ofisa Habari
Mwandamizi wa Chadema, Tumaini Makene walithibitisha juu ya upekuzi huo.
Kicheere alisema aliitwa jana kwenda Kituo Kikuu
cha Polisi, alipofika alielekezwa kufuatana na mteja wake na polisi
kwenda Makao Makuu ya Chadema.
“Walifanya upekuzi kusaka nyaraka kwa ajili ya kuongeza ushahidi wa uchunguzi wao,” alisema Kicheere.
Naye Makene alikiri kufanyika kwa upekuzi na kufafanua ulifanyika ndani ya ofisi za Chadema.
Lwakatare kufikishwa mahakamani
Pia kwa nyakati tofauti Kaimu Mkurugenzi wa
Upelelezi, Isaiah Mungulu na Msemaji wa Polisi, Advera Senso
waliithibitishia Mwananchi kuwa Lwakatare atapandishwa kizimbani leo.
“Upelelezi umekwenda vizuri na kesho (leo) atapandishwa kizimbani ili kujibu mashtaka yanayomkabili,” alisema Mungulu.
Alipoulizwa kuhusu kupekuliwa kwa ofisi za Chadema jana alasiri, Mungulu alijibu suala hilo lilikuwa la kiufundi zaidi.
“Hilo suala ni `technical’ (kiufundi). Hilo siwezi kukujibu bwana,” aliongeza Mungullu.
Senso alisema kuwa upelelezi ulikuwa kwenye hatua
nzuri na alithibitisha kuwa walimwita Kicheere kwa mahojiano zaidi
kuhusu mteja wake.
“Tumemwita tena leo (jana) Wakili wa Lwakatare
kama mwendelezo wa upelelezi wetu, suala hili linatakiwa lifanyiwe
uchunguzi wa kina kwa hiyo siyo vibaya kumwita mara kwa mara,” alisema
Senso.
Lwakatare alikamatwa saa saba mchana Machi 13,
mwaka huu katika makao makuu ya chama hicho Kinondoni, ambapo alipelekwa
katika Makao Makuu ya Polisi kwa mahojiano na baadaye kushikiliwa
katika Kituo Kikuu jijini Dar es Salaam.
CHANZO: MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment