pagead2.googlesyndication.com pagead2.googlesyndication.com

Simulizi ya muuguzi alivyofanyiwa unyama Kibaha


 



Tarehe 26 ya mwezi wa 12, mwaka 2011, pengine ni siku isiyoweza kusahaulika katika kumbukumbu za msichana mrembo Mishaly Sumary.
Ni siku ambayo binti  huyu wa miaka 26 tu, alipokutana na mkasa uliomsababisha kupooza  mwili wake wote.
Ilikuwa ni siku moja tu baada ya sikukuu ya Krismas.Mishaly, alikuwa akitoka kazini kwake yeye ni muuguzi katika Hospitali ya Dk Joseph Bakes, Kibaha.
Saa moja na nusu jioni, alipigiwa simu na dada wa rafiki yake, ambaye alikuwa akihitaji ushauri.
Walikubaliana wakutane katika eneo la lango Kuu Kibaha. Mazungumzo yao yalipomalizika, Mishaly, alitaka kuchukua usafiri wa bodaboda, ili umuwahishe nyumbani kwake. Lakini rafiki  yake alimshauri atembee kwa miguu kwa kuwa usiku haukuwa mwingi.
Mishaly, aliukubali ushauri ule na akaanza kuchepuka akielekea nyumbani kwake.
Dakika kumi tu, baada ya kuagana na rafiki yake, Mishaly alisikia kishindo cha watu nyuma yake.
Ghafla aliwaona wanaume wawili  wakimwendea kwa kasi. Walimkaba, mmoja akimshika miguu na mwingine akiikamata shingo yake.
“Nilijaribu kupiga kelele, lakini mmoja wao alinikaba shingoni, nilijitahidi kupigana nao lakini haikuwa kazi rahisi,” anasema Mishaly
Wanaume wale walimwambia: “Sali sala yako ya mwisho”
Lakini Mishaly aliendelea kujitetea kwa kurusha miguu.
Walitaka kumrusha katika kisima cha Dawasco kilichopo karibu na eneo hilo, lakini wakaachana na wazo hilo.

Walipoona anajitetea kwa nguvu, mmoja akaikunja mikono yake miwili kwa nyuma…akaweka goti katikati ya mgongo… na kumvunja mithili ya mtu avunjavyo muwa.
“Nilipiga kelele kwa maumivu makali niliyoyapata, nikasikia watu wanakimbilia katika lile eneo, nikawasikia wale wanaume wakisema, maliza kazi tusiuze gazeti,” anasimulia Mishaly
Katika kumalizia uhalifu huo, mmoja wa  wanaume wale alichukua chuma bapa chenye urefu wa mkono wa mtu mzima, na kumpiga nacho mdomoni.
Kwa kitendo kile, Mishaly alivunjika meno mawili, na kupasuka mdomo sehemu ya chini.
Wakati huo huo, mwanaume mwingine aliishika shingo ya binti huyo na kuizungusha mithili ya dereva akataye kona kwa nguvu.
“Watu walianza kujaa katika lile eneo,  aliyenivunja shingo akakimbia, lakini nikamshika shati  yule wa mbele aliyenipiga na chuma,” anasema
Katika kujaribu kukimbia, kijana aliyeshikwa shati alimng’ata Mishaly mdomoni. Alimng’ata kwa nguvu kiasi kwamba meno yalipenyeza ndani ya mdomo.
Baada ya kumng’ata alivua shati lake na kukimbilia katika vichaka.
Mishaly alipelekwa polisi na wasamaria wema, hata hivyo ilimchukua saa nne kuandikiwa PF3, na aliendelea kuteseka na maumivu makali.
“Nilikimbizwa katika hospitali ya Tumbi, lakini hali iliendelea kuwa mbaya na nikapewa rufaa ya kwenda Muhimbili. Hata hivyo nilikutana na mgomo mkali wa madaktari,” anasema
 Ilimchukua muda kupata huduma stahiki, na akiwa hapo Muhimbili, mwili wake wote ukaingia ganzi.
 “Sikuwa na hisia zozote kuanzia mikononi hadi miguuni…sikuweza kufanya chochote, kichwa changu tu ndicho kilikuwa na ufahamu” anasema
Alihamishwa tena na kupelekwa katika hospitali ya Dk Bakes ambapo ndipo kazini kwake. Hapo Mishaly alipata matibabu mazuri, anakiri kuwa mwajiri wake alitumia ujuzi wake kumtibu pale alipoweza.
Picha ya X-ray ilionyesha kuwa pingili tatu za uti wa mgongo wa Mishaly zimekatika. Lakini pia, nyonga yake ilikuwa imeharibiwa vibaya.
 Aidha, shingo yake lilikuwa limeharibiwa na kuvunjika vunjika.
“Nilitakiwa kwenda Muhimbili kwa wataalamu wa mishipa lakini hata hivyo wakasema hawataweza kunifanyia upasuaji kwa sababu mishipa yangu ya damu imekufa. Wanachoweza kunisaidia ni mazoezi tu,” anasema
Mishaly anatakiwa kufanyiwa upasuaji nchini India, ili arejee tena katika uzima wake wa awali.
Akiwa ni mtoto wa pili kati ya watoto tisa, Mishaly hana ndugu hapa jijini na hivi sasa amepewa hifadhi katika familia ya mzee wa kanisa lake.
“Familia yangu ni ya kimaskini, mama yangu ni mgonjwa yu taabani, na sijui nitapata wapi fedha za kutibiwa nje ya nchi,” anasema
 Hata fedha za kwenda kufanya mazoezi Muhimbili, Mishaly huchangiwa na waumini wenzake.
 Mishaly, binti mdogo ambaye bado mchango wake unahitajika kwa taifa, hajiwezi kwa lolote. Ni wa kubebwa, kufuliwa, na muda wake mwingi anautumia akiwa kitandani.
 Baada ya mazungumzo yetu, Mishaly anamaliza na ujumbe huu:
“Namuomba Mungu aninyanyue hapa kitandani, na iwapo haitampendeza mimi kunyanyuka, basi …namsihi niwepo katika ufalme wake”.
Familia ya Mzee Nyange inayomtunza Mishaly haikutaka kuzungumza lolote.Ili kumsaidia Mishaly, piga namba 0764-438084

0 comments:

Post a Comment