pagead2.googlesyndication.com pagead2.googlesyndication.com

Wabunge waanza kugomea bajeti


  Jenister Mhagama
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii, Jenister Mhagama alisema licha ya kwamba ajira ni moja ya vipaumbele vilivyoainishwa na Serikali, wameshangazwa na kutokupewa kipaumbele katika bajeti. Jumatatu wiki hii, Serikali ilitangaza mwelekeo wa bajeti inayofikia Sh17.7 trilioni kwa mwaka ujao wa fedha, huku ikisema itaongeza uwekezaji utakaotoa ajira mpya kwa vijana.


Tatizo la ajira kwa vijana ni ajenda ambayo imezua malumbano makubwa baina ya wanasiasa ambapo Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ndiye kinara wa ajenda hiyo.
Mhagama ambaye pia ni Mbunge wa Peramihlo alisema kamati yake imeshangazwa na kiasi cha Sh20 bilioni kwa wizara hiyo, huku fedha za maendeleo zikiwa ni Sh600 milioni sawa na asilimia tatu tu ya bajeti hiyo.

“Tumeikatalia Serikali kwani bajeti hiyo haiwezi kusaidia kutatua tatizo la ajira kama kweli ni kipaumbele chake, wametushangaza kwa kutenga kiasi kidogo cha fedha wakati wizara hii inasimamia kati ya mambo yaliyopewa umuhimu kwenye mwaka ujao wa fedha,” alisema Mhagama.

Alisema msingi mwingine wa kukataa bajeti hiyo ni azimio la Bunge ambalo linaelekeza kuanzishwa kwa mfuko maalumu kwa ajili ya vijana, pia lile linalotaka kuanzishwa kwa benki maalumu kwa ajili ya kuliwezesha kundi hilo.

Mhagama alisema kuwa katika bajeti hiyo inaonyesha kuwa Sh15 milioni kwa ajili ya ndiyo imetengwa kwa ajili ya benki ya vijana, wakati Shirika la Habari la Utangazaji Tanzania (TBC) halijatengewa fedha yoyote.

“Vijana ni watu muhimu kabisa. Kumbuka asilimia 63 ya wananchi na miongoni mwao kuna wasomi na wasio wasomi lakini hawana ajira, mambo haya yote hayawezi kutekelezwa kwa kiwango kidogo cha fedha kilichotengwa,” alionya Mhagama.

Alisema kuwa wizara hiyo iliomba Sh42 bilioni kwa ajili ya maendeleo, lakini imeambulia milioni 600, pia imepewa jumla ya Sh20,728,045,000 kwa matumizi yote.
“Tumekubaliana tukutane na Kamati ya Bunge ya Bajeti na Kamishna wa Bajeti wa wizara ili tujadili kwa kina kuhusu bajeti hii kwa kweli imetushangaza,” alisema.

Mbunge aanguka
Kwa upande wake, tukio la kuanguka kwa Mbunge wa Chambani (CUF), Salim Hemed Khamis lilitokea saa 10.50 wakati wajunbe wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje wakijadili masuala yanayohusu Kituo cha Mikutano ya Kimataifa cha Arusha (AICC).

Kabla ya tukio hilo, Khamis alikuwa anashiriki kwenye kikao hicho kama kawaida lakini baadaye alisema alikuwa anajihisi vibaya na kuanguka, hivyo wabunge wenzake walimbeba na kumtoa nje.

Baada ya kutolewa nje, hali yake ilizidi kuwa mbaya, kabla ya baadhi ya wabunge na waandishi wa habari kumbeba na kumwingiza kwenye chumba maalumu na baadaye kumpeleka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Edward Lowassa alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kudai kuwa baada ya kufikishwa Muhimbili, alipelekwa moja kwa moja katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu.

“Ni kweli mbunge mwenzetu Khamis amelazwa chumba cha wagonjwa mahututi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili baada ya kuugua ghafla,” alisema Lowassa.Mapema mwaka huu, Khamis alikuwa nchini India katika hospitali ya Apollo alikokuwa huko kwa matibabu na alirejea nchini ili kushiriki vikao hivyo.

JNIA kupanuliwa
Katika hatua nyingine imebainika kuwa Serikali imetenga kiasi cha Sh255 bilioni kwa ajili ya upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Mwalimu Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam.


Upanuzi huo ni wa kiwanja namba tatu (terminal three) ambacho kinahusisha kwenye eneo la Kipawa ambalo wananchi walihamishwa na kulipwa fidia zao.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu, Peter Serukamba alisema mbali na upanuzi wa uwanja huo, pia fedha hizo zitatumika kuboresha reli ya kati na bandari.

Chanzo mwananchi

0 comments:

Post a Comment