pagead2.googlesyndication.com pagead2.googlesyndication.com

WALIO MTEKA KIBANDA MAHAKAMANI KESHO

Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova

Hatimaye sakata la kutekwa, kuteswa na kujeruhiwa kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, (TEF), Absalom Kibanda, limepata mwanga na watuhumiwa wa kadhia hiyo wataanikwa hadharani kesho.

Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, amesema timu iliyoundwa kuchunguza kutekwa, kuteswa na kujeruhiwa kwa Kibanda, itatoa taarifa kamili na idadi ya watu waliowakamata kuhusiana na tukio hilo.
Wakati Kova akieleza hilo, mitandao ya kijamii jana ilieleza kuhusu taarifa za kukamatwa kwa mtu aliyejulikana kwa jina la Ludovick Joseph kwa tuhuma za kuhusika kuteswa kwa Kibanda.
Kova alipoulizwa kuhusiana na taarifa hizo, aliomba apewe muda ili awasiliane na mwenyekiti wa timu iliyoundwa kuchunguza tukio hilo.
“Tangu asubuhi nilikuwa Mabwepande, ndiyo nimerudi ofisini muda sio mrefu, kuhusu hilo nimelisikia kupitia kwa waandishi wenzako walionipigia simu, nipe muda nilifuatilie,” alisema.
Baada ya kupigiwa tena, Kova alisema kwa mujibu wa maelekezo aliyopewa na timu hiyo, haikuwa muda muafaka kulizungumzia suala hilo jana.
“Wameniambia taarifa kamili ya kile walichokuwa wakikichunguza kwa muda wote, kitatolewa siku ya Jumatatu (kesho) kupitia mkutano wa waandishi wa habari. Huko mtaelezwa wangapi walikamatwa na kuhojiwa na nini kitafuata,” alisema Kova na kukata simu.
Awali, taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zilieleza kuwa, Joseph alikamatwa akiwa mkoani Iringa.
Gazeti hili lilipowasiliana na Kaimu Kamanda wa mkoa huo, Wankyo Nyigesa, alisema tangu juzi amekuwa akipokea simu za waandishi wa habari zikiulizia tukio hilo.
Alisema amewasiliana na polisi kwenye eneo lake na kuthibitishiwa hakuna tukio la aina hiyo na kumwomba mwandishi ajaribu kuwasiliana na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Njombe.
Kupitia mtandano wa kijamii wa ‘Mjengwa’, katika ukurasa wake aliandika kuwa usiku (bila kutaja ni lini) akiwa kwenye shughuli ya shule ya watoto wake Highlands Hall Iringa, alipata habari kuwa Joseph amekamatwa.
Katika ukurasa huo alidai kuwa Joseph alikamatwa na polisi kuhusiana na tuhuma za kuhusika na kuteswa mwandishi Absalom Kibanda.
Pia alidai jinsi anavyomfahamu kijana huyo toka akiwa Chuo Kikuu (DUCE) na kwamba ni mmoja wa Watanzania anaowafahamu kupitia kazi zake za magazeti.
Taarifa hiyo ilisema, Joseph amekuwa akiishi Dar es Salaam na ni miongoni mwa waliokuwa wakimsaidia kwa kujitolea kwenye kazi zake za mitandaoni, hususan kwenye Mjengwablog na website (tovuti) ya kwanza ya Jamii.
Kadhalika, alisema miezi ya hivi karibuni Joseph ndiye aliyekuwa akifanya kazi ya kuingiza magazeti kwenye Mjengwa blog kila asubuhi.
“Akiwa Dar es Salaam na mimi nikiwa Iringa, Ludovick hakuwa mwajiriwa wangu kama wanavyodhani wengine, bali amekuwa ni mmoja wa vijana waliokuwa tayari kunisaidia kwa kazi za hapa na pale ikiwamo kunipelekea invoice (ankara ya malipo) kwa watangazaji kwenye Mjengwa blog. Mara nyingi nimekuwa nikimtambulisha kama ' Msaidizi wa Mwenyekiti” alisema.
Aliongeza kuwa juzi alimwomba aende Iringa ampelekee vitabu vyake vya invoice na risiti kutokana na kutegemea ugeni kutoka Mfuko wa Ruzuku kwa Vyombo vya Habari (TMF).
Mjengwa blog katika ukurasa huo, amedai kuwa katika hilo lililomtokea, hawezi kumtetea wala kumtia hatiani kwa kuwa naye ni binadamu kama wengine na hawezi kusema anamfahamu zaidi.
“Kwa vile yuko mikononi mwa vyombo vya usalama, nina imani, kuwa vyombo hivyo vitafanya kazi yake ili kutusaidia katika kupata ukweli wa jambo zima…”
“Na kama ni kweli kwa namna yoyote ile itathibitishwa kuwa ameshiriki njama za kupanga mikakati hiyo ya kigaidi, basi, ahukumiwe kwa dhambi hiyo,” alisema.
Kibanda ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa New Habari (2006), alijeruhiwa usiku wa kuamkia Jumatano iliyopita na watu wasiofahamika.  
SOURCE: NIPASHE JUMAPILI

0 comments:

Post a Comment