pagead2.googlesyndication.com pagead2.googlesyndication.com

Kutana na muuza dawa za kulevya aliyeishia kukatwa mkono, mguu

 


UKIMUONA kwa mara ya kwanza ni vigumu kufikiri kama anaweza akawa amepitia katika mikasa migumu ya kutisha ya maisha kama ilivyomtokea.
Nguo zake kuukuu, nywele za chafu na ulemavu alionao vinaficha historia nzito aliyonayo katika maisha pamoja na utaalamu wa kuongea kwa ufasaha lugha za Kiingereza, Kiitaliano na Kireno licha ya kutosomea.
Huyu ndiye ‘Wa Mbele’ kijana aliyejiwekea ndoto za kuishi nje hasa Ulaya akiamini kuna maisha mazuri ambayo yangemfanya naye awe tajiri.
Hata hivyo ndoto zake hizo zilizimika pale hali hali ilivyobadilika na kujikuta akililia kurudi Tanzania baada ya kukumbana na mateso, manyanyaso, ukatili na biashara za kuhatarisha maisha kiasi cha kumfanya awe mlemavu wa viungo vya mwili uliomdhoofisha na kumharibia maisha yake.
Wa Mbele ambaye jina lake halisi ni Mbembele Said Lipwata nilikutana naye katika safari yangu Mjini Mtwara. Mbali na ulemavu wake  wa mguu na mkono wa kulia, bado ana uwezo mkubwa wa kutembea kwa kuruka kwa masafa marefu.
Anasema alizaliwa mwaka 1967 mkoani Mtwara, alikulia huko hadi mwaka 1976 alipojiunga na elimu ya msingi katika Shule ya Shangani.
“Hali duni ya maisha ilinifanya nimkimbie baba aliyekuwa akiishi Mtwara, kwenda kwa mama Magomeni Kagera Jijini Dar es salaam, niliendelea na masomo yangu huko” anasimulia Mbembele akieleza kuwa wazazi wake hawakuwa wakiishi pamoja.
Kaka zake wakubwa walikuwa wanajishughulisha na kazi za ubaharia jambo ambalo lilimpa matumiani makubwa ya kukamilisha ndoto ambazo alikuwa nazo kwa miaka mingi kwamba siku moja angezamia kwenda Ulaya akiamini angepata maisha mazuri.
Baada ya kumaliza masomo yake ya msingi mwaka 1983, Mbembele hakuwa na kazi ya kufanya kutokana na kushindwa kuendelea na masomo ya Sekondari, akaanza kuzunguka na kaka zake katika meli tofauti ndani ya Pwani ya Afrika Mashariki na kujaribu mbinu za kuzamia Ulaya.
Majaribio ya kuzamia
Kutokana na kupata uzoefu kidogo katika safari za meli, Mbembele anasema alianza majaribio ya kuzamia yeye na rafiki zake. Bandari ya Mtwara na Dar es salaam ndiyo vilikuwa vituo vikuu vya majaribio yao.
“Kwa nyakati tofauti tangu mwishoni mwa mwaka 1984 nilianza kufanya majaribio ya kuzamia kwenye meli zilizokuwa zinaenda Asia na Ulaya lakini sikufanikiwa kwa sababu walinzi wa meli walinikamata mara kwa mara,” anasema Mbembele.
Muda mwingi alifanya mbinu apate vibarua vya kupakia na kupakua mizigo katika meli zilizokuwa zinaingia nchini zikitokea nje, lengo hasa likiwa sio kazi bali kutafuta kibali ambacho kingemruhusu kuingia sehemu mbalimbali za meli hizo.
“Mwishoni mwaka 1985 mimi na rafiki zangu watatu tulizamia kwenye meli ya watu kutoka India, iliyokuwa imekuja kubeba Korosho katika bandari ya Mtwara baada ya kupata kibarua cha kupakia mizigo” anasimulia.
Huku akivuta kumbukumbu kwa hisia, Membele anakumbuka meli hiyo ilikuwa inaitwa Vishva Bindu ambayo iliwapeleka mpaka Mumbai nchini India.
“Baada ya kufika India tulikamatwa na walinzi wa meli na kulazimishwa kushusha mzigo katika bandari ya Cochin kisha tulipelekwa katika kambi za uhamiaji”
Anasema baada ya kupata taarifa hizo, maofisa wa uhamiaji nchini India walifanya mawasiliano na meli ile, uongozi wa meli ulikubali kuwarudisha nchini.
“Polisi wale walitufunga pingu na kutuingiza ndani ya meli tayari kwa safari ili tusitoroke”
Anasema baada ya kufika Bandari ya Dar es salaam walipokelewa na maofisa wa polisi,  walipelekwa mahakamani na kushtakiwa kwa kosa la kuzamia na kufungwa mwaka mmoja katika gereza la Ukonga Jijini Dar es salaam.

Anaongeza kuwa “Hata hivyo tulitumikia gerezani kwa miezi nane tu na kuachiwa huru, tukaendelea na mihangaiko ya kutafuta maisha kwa kufanya kazi katika meli walizokuwa wanafanyia kazi kaka zangu”.
Anasema mara nyingi alikuwa akisafiri katika bandari za Mombasa, Lamu, Zanzibar, Mauritius na hadi Somalia.
Licha ya kuwa alishakamatwa na kuonja chungu ya kuzamia nchi za nje, Mbembele bado alidhamiria kufanikisha lengo lake la kuishi Ulaya kwa kufanya biashara yoyote ile.

mwananchi

0 comments:

Post a Comment