Dar es Salaam. Mwenyekiti wa CUF, Profesa
Ibrahim Lipumba ameiponda Serikali kwa kuwa na uchumi unaokua kwenye
makaratasi wakati maisha ya wananchi yakiendelea kuwa magumu siku hadi
siku.
Profesa Lipumba alisema hayo jana kwenye mkutano wa 18 wa mwaka wa Taasisi ya Utafiti ya Kuondoa Umaskini Tanzania (Repoa).
Akizungumza mbele ya Makamu wa Rais, Dk Mohamed
Bilal, Profesa Lipumba alisema uchumi wa Tanzania hivi sasa unakwenda
kama mtoto anayetambaa akiwa na watu wazima wanaokimbia.
“Tulikuwa na mipango mingi lakini isiyotekelezeka,
tulielezwa ni lazima tukimbie wakati wenzetu wanatembea, lakini badala
ya kuongeza mbio, sasa tunatambaa wakati nchi za wenzetu zinakimbia kwa
kasi kimaendeleo,” alisema Profesa Lipumba.
Alisema ingawa uchumi unakua kwa asilimia saba kwa
mwaka, lakini ukuaji huo haulingani na maisha ya wananchi ambayo
yanazidi kuwa magumu siku hadi siku.
Profesa Lipumba ambaye kitaaluma ni mchumi,
alisema sekta ya kilimo ambayo inaajiri asilimia 75 ya wananchi inakuwa
kwa asilimia 25.
“Unategemea nini kama sekta ambayo inawahusisha
wananchi wengi, lakini bado haijaboreshwa ili iwanufaishe,” alisema
Profesa Lipumba.
Alisema ingawa Serikali imekuwa na mipango mizuri,
lakini imeshindwa kuitekeleza hatua ambayo inawafanya wananchi wakate
tamaa ya maisha.
Akitoa mfano, alisema kitendo cha kuwa na vipaumbele vingi wakati uwezo wa fedha ni mdogo ni kikwazo cha kuleta maendeleo.
“Hata kwenye bajeti zetu tumekuwa na vipaumbele
vingi kiasi kwamba hata kuvitekeleza inakuwa vigumu, tuchague vipaumbele
vichache na tuvifanyie kazi,” alisema Profesa Lipumba.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais, Dk Bilal alisema
kukua kwa uchumi unaowafikia wananchi ni mchakato ambao hauwezi kuja
ghafla. Alisema kitendo cha Serikali kutengeneza miundombinu ikiwamo
barabara ni moja ya juhudi zinazofanywa ili wananchi waweze kunufaika.
“ Ni kweli ukuaji wa uchumi haufanani na maisha ya
wananchi wengi, lakini hatua zinazochukuliwa na Serikali kama kujenga
barabara, maji ,huduma za afya na elimu zinasaidia kukuza uchumi kwa
watu walio wengi,” alisema Dk Bilal.
Naye,Mkurugenzi Mtendaji wa Repoa, Profesa Samwel Wangwe alisema
mkutano huo wa watafiti unaangalia namna ukuaji wa uchumi na maisha ya
wananchi walio wengi.
Kwa upande wake,Mtaalamu wa masuala ya uchumi
kutoka Malaysia, Datuk Chris Tan alisema uchumi utakuwa juu kama
viongozi watakuwa na nia ya dhati ya kuleta mabadiliko
MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment