pagead2.googlesyndication.com pagead2.googlesyndication.com

Pinda afunga machimbo ya moramu yaliyoua watu 14 Arusha

Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania wakiwa wamebeba mwili wa mtu aliyepoteza maisha  kutokana na  kuporomoka kwa udongo katika machimbo ya Moramu yaliyopo eneo la Moshono, Arusha.  Picha na Filbert Rweyemamu 


Arusha. Waziri Mkuu Mizengo Pinda jana alitangaza kuyafunga rasmi machimbo ya moramu eneo la Moshono, Arusha hadi Serikali itakapoweka utaratibu mzuri wa shughuli mbalimbali za uchimbaji katika eneo hilo.

Hatua hiyo ya Pinda imetokana na ajali ya watu 14 waliopoteza maisha baada ya kufukiwa na kifusi juzi, wakati wengine wawili walijeruhiwa kwenye ajali hiyo iliyochangiwa kwa kiasi kikubwa na mvua zinazonyesha jijini Arusha.
Pinda alitoa agizo hilo alipotembelea eneo hilo pamoja na kuwajulia hali majeruhi wawili waliolazwa katika Hospitali ya Mkoa ya Mt Meru.
Majeruhi mmojawapo aliruhusiwa kutoka hospitalini hapo baada ya kuondoka Waziri Mkuu.
Baada ya kuwasili Arusha jana saa 7.30 mchana, Pinda alikwenda moja kwa moja katika Hospitali ya Mt Meru kuwatembelea majeruhi hao.

Wakati wa ziara yake alishuhudia majeneza 14 iliyokuwa na miili ya watu waliofariki kwenye tukio hilo ambayo imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti.

Akizungumza mara baada ya kutembelea eneo hilo Pinda alitoa salamu za pole kwa waathirika kutoka kwa Rais Jakaya Kikwete huku akilishukuru Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) na wananchi waliojitokeza kuokoa maisha ya watu katika tukio hilo. Alisema Serikali imeyafunga machimbo hayo, huku akisisitiza kuwa Serikali kamwe haiwezi kuruhusu uchimbaji wa namna hiyo.

“Tutafunga kwa muda kama tulivyofanya Mugusu ili tujipange vizuri na tupate nafasi ya kusaidiana, hatuwezi kuruhusu uchimbaji wa namna hii halafu kesho na keshokutwa tukaonekana wapuuzi,” alisema Pinda.

Waziri Mkuu pia alimwagiza Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo kushirikiana na JWTZ kuimarisha ulinzi mkali katika eneo hilo ili watu wasiweze kujipenyeza na kufanya uchimbaji nyakati za usiku.

“Mkuu wa Mkoa ashirikiane na jeshi kuimarisha ulinzi hapa najua ni gharama kwa Serikali lakini ni nafuu kwetu pia,”alisisitiza Pinda.

Naye Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stephen Masele aliwatupia lawama baadhi ya viongozi wa Serikali na Halmashauri ya Jiji la Arusha kwa tabia ya kuendekeza kuchukua mapato katika uchimbaji wa eneo hilo badala ya kuangalia usalama.

Masele alidai wizara yake imejipanga kutoa elimu bora ya uchimbaji kwa wachimbaji mbalimbali mkoani Arusha.

Alisema tukio hilo ni ajali na limetokana na wachimbaji wa eneo hilo kutojua sheria za uchimbaji na kusisitiza kuwa eneo hilo halikupaswa kuchimbwa kuelekea chini ardhini bali pembeni.



MWANANCHI

0 comments:

Post a Comment