Dar es Salaam. Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu imemwachia huru Mkurugenzi wa zamani wa Utawala na
Utumishi (DPA), Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba kutokana na
upelelezi uliofanywa kuwa mbovu na wakili aliyekuwa akiiendesha kesi
hiyo kuwa mzembe.
Liyumba alikuwa akikabiliwa na kesi ya kukutwa na
simu akiwa gerezani Ukonga, Dar es Salaam, wakati akitumikia kifungo cha
miaka miwili, kilichotokana na kupatikana na hatia ya matumizi mabaya
ya ofisi ya Umma.
Hakimu Mkazi, Augustina Mmbando alisema mahakama
inamwachia huru Liyumba kutokana na upande wa mashtaka kushindwa
kuthibitisha shtaka lililokuwa likimkabili pasipo kuacha shaka.
Alisema wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo,
shahidi wa upande wa mashtaka ambaye ni Ofisa Magereza, Patrick alidai
kuwa simu aina ya Nokia 1280 ilikutwa mikononi mwa Liyumba wakati akiwa
gerezani, huku Liyumba akidai kwenye utetezi wake kuwa siku hiyo
alikwenda nayo Patrick na kujifanya alimkuta nayo.
‘Wakati huo tulitegemea angeileta simu, lakini
alitoa mkebe wa kuhifadhia miwani na kuutenda kuwa kielelezo cha
ushahidi na badala ya simu. Akaitoa kama utambulisho tu, wakati shahidi
mhusika Patrick alikuwapo mahakamani na kutambua vielelezo vyote
alivyodaiwa kukutwa navyo Liyumba siku ya tukio.
Alisema hata huo utambulisho wa simu uliochukuliwa
na mahakama, ulichukuliwa kimakosa kwa sababu aliyepaswa kuomba kufanya
hivyo alipaswa kuwa shahidi na siyo Wakili wa Serikali kama alivyofanya
Kaganda.
Kwa upande wa mchunguzi wa kesi hiyo, Hakimu
Mmbando alisema alipaswa kubainisha ile laini ya simu yenye namba 0653
004662 ilikuwa ni ya nani kati ya mshtakiwa na shahidi kwa sababu
kulikuwa na utata.
“Kuna uwezekano ni kuwa ni kweli Liyumba alikutwa
na simu gerezani, lakini kutokana na upelelezi mbovu wa kufuatilia namba
iliyotumiwa ilikuwa ni ya nani, mazingira ya kuingizwa gerezani
inaonesha wazi kuwa mchunguzi alikuwa mzembe na uchunguzi mbovu.”
Alisema Hakimu Mmbando.
0 comments:
Post a Comment