Mbeya. Mfanyakazi wa Kitengo
cha Kuhifadhi Maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Mbeya, Eugene Vurugu
amemtisha Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid kuwa
ikitokea amefariki dunia akiwa mkoani Mbeya, basi maiti yake italazwa
kwenye sakafu hospitalini hapo.
Akizungumza kwenye mkutano wa wafanyakazi na naibu
waziri huyo mwishoni mwa wiki iliyopita, Vurugu alisema kitengo hicho
kimezidiwa na wingi wa maiti zinazopelekwa hospitalini hapo.
Alisema kitengo hicho cha kina majokofu sita tu na hulazimika kuhifadhi miili kwa zamu ili angalau maiti zisiharibike.
“Hata wewe Waziri ukifa leo, hakuna pa kukuweka.
Utawekwa sakafuni kusubiri maiti nyingine zipoe
halafu utaingizwa ndani kwa kuingizwa maiti mbili kwenye eneo la mtu
mmoja,’’ alisema Vurugu.
Aliiomba Serikali ifanye haraka kuboresha kitengo hicho ili kuepusha tatizo la kuoza kwa miili ya marehemu.
Kumekuwa na malalamiko kuhusu uchache wa majokofu
ya kuhifadhia maiti katika hospitali hiyo na baadhi ya watumishi
walisema hali kuwa mbaya zaidi inapotokea ajali ambayo inasababisha vifo
vya watu wengi kwa wakati mmoja.
Vurugu alidokeza pia kuwapo kwa tatizo katika
Idara ya Mifupa ya hospitali hiyo, akisema wakazi wengi wanaofika hapo
kwa matatizo hayo anawaona wakiondoka kwenda Hospitali za Peramiho ya
Ruvuma na Ikonda ya Makete huku wengine wakienda kwa waganga wa jadi
kuunga mifupa yao.
Vurugu alizungumza baada ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu
wa hospitali hiyo, Dk Humphrey Kiwelu kusoma taarifa ya utendaji mbele
ya Naibu Waziri iliyoonyesha hali iko shwari baada ya kudai kuwa
hospitali hiyo imepiga hatua kubwa kiutendaji na katika utoaji huduma
kwa wagonjwa.
Dk Kiwelu alisema hospitali yake ina mafanikio
makubwa yakiwamo ya kuwa na maabara ambayo imekubalika katika kiwango
cha kimataifa na kwamba majibu yanayotoka kwenye maabara hiyo kwa sasa
yanakubalika hata Uingereza na Marekani.
Hata hivyo, alisema hospitali hiyo haina mashine ya CT Scan licha ya kuiomba kutoka serikalini tangu 2003.
Akijibu hoja mbalimbali za wafanyakazi, Dk Rashid
aliwataka viongozi kujipanga na kuchangua vipaumbele kutokana na
mafanikio mazuri yanayoonekana hospitalini hapo.Alisema kwa kuwa hospitali hiyo imeongeza mapato ya ndani kutoka Sh60
milioni hadi Sh300 milioni kwa mwezi, ipo haja ya kutumia fedha hizo
kuiboresha kwa kuangalia vitendea kazi zaidi na masilahi ya watumishi
wote.
0 comments:
Post a Comment