Dar es Salaam.Timu ya Watafiti
katika Chuo Kikuu cha North Carolina nchini Marekani, wamegundua aina ya
sumu ambayo ina uwezo wa kuua seli ambazo zimekwishaathiriwa na Virusi
Vya Ukimwi (VVU).
Sumu hiyo iliyopewa jina, 3B3-PE38, inaweza
kutumika kutengeneza dawa ambayo ikitumiwa na mtu aliyeathirika kwa VVU,
itasaidia kuua virusi.
Watafiti wamebaini pia kuwa dawa hiyo itaweza
kusaidia waathirika kutolazimika kutumia dawa za Kupunguza Makali ya
Ukimwi (ARVs) maisha yao yote.
Hii ni mara ya kwanza kwa wanasayansi kuweza
kugundua sumu maalumu ya kuua VVU. Tafiti nyingi zinazoendelea sehemu
nyingi duniani ni za kupata chanjo.
Kwa kawaida dawa ni sumu inayoua au kuathiri
kiumbe kilichokusudiwa wakati chanjo ni njia ya kuufanya mwili
kutengeneza wenyewe kinga dhidi ya vimelea, kulingana na aina ya
ugonjwa.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa wiki hii
na Taasisi ya Tafiti za Kukabili Magonjwa ya Kuambukiza na Mzio (NIAID)
ya Marekani, inasema ni ugunduzi wa kipekee.
Upekee huo unaoelezwa unatokana na ukweli kuwa kwa
sasa dawa zilizopo za ARV zina uwezo wa kuzuia seli nyeupe
iliyoshambuliwa isimamishe mvumo wa kuzalisha virusi.
Walivyoendesha utafiti
Utafiti huo uliofadhiliwa na Taasisi ya Afya ya
Taifa (NIH) ya Marekani, unaelezwa kuwa panya 40 walitumika katika
kutafiti 3B3-PE38.
Walichofanya watafiti hao ni kuwagawa panya kwenye
makundi kadhaa na kupewa dozi ya sumu ya 3B3-PE38 kwa viwango na muda
tofauti kuanzia wiki mbili hadi nne.
Baadhi walipewa ARV pekee na wengine walipewa pamoja na sumu hiyo ya 3B3-PE38.
Katika utafiti huo, walibaini kwamba wale ambao
walitumia ARV pamoja na sumu hiyo, waliweza kupunguza kwa kiwango
kikubwa VVU pamoja na seli ambazo tayari zimeathirika.Taarifa za awali
zinaelezwa kuwa sumu hiyo inaweza kusaidia kutibu watu walioathirika na
mojawapo ya aina ya VVU.
0 comments:
Post a Comment