pagead2.googlesyndication.com pagead2.googlesyndication.com

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Telephone : 255-22-2114512, 2116898
Fax : 255-22-2113425
PRESIDENT’S OFFICE,
THE STATE HOUSE,
P.O. BOX 9120,
DAR ES SALAAM.
Tanzania
Gazeti la Mwananchi la leo, Jumapili, Machi 9, 2014, kwenye ukurasa wake wa tano, limechapisha  habari zenye kichwa cha habari –“JK awatembelea Maranda, Mkambala Hospitali ya Taifa Muhimbili.”
Katika habari hiyo, Gazeti hilo limeripoti: “Rais Jakaya Kikwete jana alimtembelea mfungwa, Rajab Maranda anayetumikia kifungo cha miaka 18 gerezani kwa wizi wa fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), aliyelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili akisumbuliwa na tatizo la mgongo.”
Habari hizi ni uongo. Mhe. Rais hakumtembelea Ndugu Maranda jana (Jumamosi) kama ilivyoripotiwa na gazeti hili na wala hajawahi kumtembelea siku yoyote iwe ni hospitalini ama kwingineko. Kwa hakika, ni jambo la kusikitisha kuwa Gazeti lenye heshima na hadhi kama Mwananchi  linaweza kujiingiza katika utunzi na uandishi wa uongo wa kiasi hiki.
Ukweli wa mambo yaliyotokea jana ni kama ifuatavyo:
Ni kweli Mhe. Rais alitembelea Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Upasuaji wa Mishipa ya Fahamu (MOI) katika  Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jana (Jumamosi). Alikwenda kuwajulisha hali wanahabari wawili – Ndugu Salum Mkambala wa Channel Ten na Margaret Chambili wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Mhe. Rais alianza kumtembelea Ndugu Mkambala ambaye amelazwa wodi binafsi –Private Ward – D, kufuatia ajali ya gari iliyomfika kwenye eneo la Visiga, Mkoa wa Pwani, akiwa njiani kwenda Morogoro mwishoni mwa wiki. Chumba hicho kilikuwa na wagonjwa watatu.
Baada ya kuzungumza na Mkambala, Mhe. Rais, kama ilivyo kawaida yake anapotembelea wagonjwa hospitali, aliwasalimia na kuwajulia hali wagonjwa wengine wawili ambao wako katika chumba hicho kimoja na Ndugu Mkambala.
Wagonjwa hao wawili ni Ndugu John Mhina, ambaye huko nyuma alipata kusoma na Mhe. Rais na Ndugu Reuben Nyanga.
Baada ya kumaliza kuwajulisha wagonjwa hao wa Private Ward D, Mhe. Rais alikwenda kwenye wodi nyingine binafsi – Private Ward K – ambako alimjulia hali Ndugu Margaret Chambiri ambaye ni mgonjwa pekee aliyelazwa katika chumba hicho. Baada ya hapo, Rais Kikwete aliondoka Muhimbili kurudi Ikulu, Dar Es Salaam.
Hakuna wakati wowote, Mh. Rais alimtembelea Ndugu Maranda ama mgonjwa mwingine kwenye Hospitali hiyo ya Muhimbili.
Ni matarajio ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, kuwa Gazeti la Mwananchi na wahariri wake, watakuwa wakweli kwa nafsi zao wenyewe na watakuwa na busara ya kutosha kusahihisha makosa haya kwa misingi ya taaluma ya uandishi wa habari ambayo ni dhahiri wanaijua fika.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

09 Machi, 2014

0 comments:

Post a Comment