pagead2.googlesyndication.com pagead2.googlesyndication.com

balaa: Baba wa mtoto azuiwa kuzika kisa Mahari

FAMILIA mbili mjini Mpanda zimejikuta zikiingia katika uhasama mkubwa, kiasi cha kupigana fimbo na ngumi makaburini katika ugomvi wa kugombea kuzika mwili wa mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu.
 
Sababu kubwa ya mpasuko huo imeelezwa kuwa ni mahari, kwani wazazi wa  upande wa mama wa mtoto huyo walikuja juu na kumzuia baba wa mtoto, Joseph Bacho mkazi wa Mtaa wa Kawajense- Madukani mjini hapa asishiriki katika shughuli zozote za maziko ya mtoto wake wakidai hawamtambui kwa kuwa hajatoa mahari kwa binti yao.
 
Inaelezwa kuwa, Joseph na mzazi mwenzake, Anna Kizo ambaye pia ni mkazi wa Mtaa wa Kawajense –Madukani walimzaa mtoto Junior Bacho nje ya ndoa ambapo hadi umauti unamfika mtoto huyo, baba yake mzazi alikuwa hajajitambulisha kwa upande wa mwanamke wala kutoa mahari.
 
Na kwamba, tangu kuzaliwa kwa mtoto huyo, alikuwa akiishi na kulelewa na mama yake mzazi, Anna nyumbani kwa wazazi wake katika Mtaa wa Kawajense.
 
Kwa mujibu wa waombolezaji ambao hata hivyo hawakuwa tayari kutajwa majina , vurugu hizo ziliibuka baada ya upande wa ndugu wa baba wa mtoto kuweka msiba nyumbani kwao na kuandaa taratibu za kumzika mtoto huyo.
 
Hata hivyo, kitendo hicho kilipingwa na upande wa mama wa mtoto, ukisema ndio wenye haki ya kumzika mtoto huyo ambaye hawakuwahi kumtambua kisheria baba yake mzazi.
kaburi1
 
Ndugu wa upande wa baba ulifanikiwa kuchimba kaburi, kuutoa mwili mochari na kuufikisha nyumbani tayari kwa maziko, lakini vurugu za upande wa pili ikiwa pamoja na ndugu upande wa mama kufukia kaburi, zilisimamisha shughuli zote, huku malumbano yakishika hatamu hadi askari wa jeshi la polisi kupitia kikosi chake cha kuzuia fujo (FFU) kilipolazimika kuingilia kati na kusimamia shughuli za kuurudisha mwili katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Wilaya ya Mpanda.
 
Inaelezwa kitendo cha upande wa mama wa mtoto kufukua kaburi ndiko kulikochangia kuchochea vurugu hadi FFU walipoingilia kati.
 
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi , Dhahiri Kidavashari amethibitisha kutokea kwa mkasa huo na kwamba hakuna mtu yeyote aliyejeruhiwa katika vuta nikuvute hiyo pia hakuna ayekamatwa kuhusiana na tukio hilo ambalo ni la kijamii zaidi.
 
Ilivyoanza
Mkasa mzima unadaiwa kutokea mtaani hapo Alhamisi wiki hii, siku ambayo mtoto huyo alifariki dunia katika Hospitali ya Wilaya ya Mpanda alikokuwa akiuguzwa na shangazi yake, Evelyne Komba na bibi yake mzaa baba, Teddy Francis.
 
Inaelezwa kuwa, wakiamini wana haki zote za kumzika mtoto huyo, waliuchukua mwili na kuweka msibani nyumbani kwao, jambo lililopingwa na upande wa mama wa mtoto waliokuja juu na kusema hawamtambui baba wa mtoto kwa kuwa hakuwa ametoa mahari.
 
“Ujue katika mila na desturi zetu mtu kama amezaa na msichana bila kuoana huwa hatambuliwi na upande wa mzazi wa kike mpaka atakapolipa mahari hapo ana kuwa na haki zote kwa mwanae …sasa kwa upande wa Joseph amezaa tu na binti yetu nje ya ndoa hivyo hatumtambui mpaka aje ajitambulishe na kulipa mahari.”
 
“Kwa utaratibu huo Joseph hana kabisa haki ya kuweka msiba wa mjukuu wetu wala kumfanyia maziko mpaka akamilishe taratibu zote za mila na desturi zetu ikiwemo kulipa mahari kwa wakwe zake “ alisisitiza mmoja wa wanandugu upande wa mama mzazi wa marehemu .
 
Licha ya kurushiana maneno makali pande hizo mbili, upande wa ndugu wa baba mzazi wa marehemu waliibuka na kumshutumu mama na ndugu zake kushindwa kumhudumia mtoto huyo wakati alipougua .
 
Inadaiwa mama wa marehemu hakumruhusu kabisa mzazi mwenzake kumwona mwanae alipokuwa mgonjwa na kuuguzwa nyumbani kwa mama yake katika Mtaa wa Kawajense – Madukani .
 
“Joseph kila alipofika nyumbani kwa mzazi mwenzake ili kumjulia hali mwanae aliyekuwa mgonjwa hakuruhusiwa kuingia ndani kwa mdai kuwa mtoto alikuwa amelala “ anadai mtoa taarifa .
 
Inadaiwa Joseph aliamua kumchukua mwanae huyo Juni 18 ,mwaka huu kwa nguvu kutoka kwa mama yake mzazi na kumpeleka hospitalini alikolazwa kwa matibabu baada ya kubainika kuwa anasumbuliwa na utapia mlo mkali .
 
Kwa mujibu wa mashuhuda ndipo upande wa ndugu wa mama mzazi wa marehemu walipozira ikidaiwa kuwa hawakuweza kufika hata siku moja kumjulia hali mtoto huyo aliyekuwa akiuguzwa hospitalini hapo na shangazi yake Evelyne na bibi yake Teddy hadi umauti ulipomfika .
 
Licha ya upande wa ndugu wa mama mzazi wa marehemu kushushiwa tuhuma na lawama hizo nzito waliendelea na msimamo wao kwamba walikuwa na haki ya kumzika marehemu hivyo nao wakaamua kuweka msiba nyumbani kwa mama wa marehemu katika Mtaa huo wa Kawajense.
 
Ndipo juzi , Juni 27 wazee wa Mtaa wa Kawajense waamua kuingilia kati mgogoro huo kwa kuzikutanisha pande hizo mbili zilizokuwa zikivutana na kufikia uamuzi kuwa msiba uwe nyumbani kwa baba wa marehemu.
 
Kufutia uamuzi huo shangazi wa marehemu aliongoza ndugu zake akiwemo baba mzazi wa marehemu hadi chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali ya wilaya ya Mpanda mjini hapa na kuuchukua mwili wa marehemu kisha kuupeleka nyumbani kwa bibi ya marehemu kwa ajili ya maandalizi ya maziko yake .
 
Maziko ya mtoto huyo yalipangwa kufanyika katika makaburi ya Kawajense –Msufini ambako upande wa ndugu wa baba mzazi wa marehemu walichimba kaburi katika eneo hilo, lakini muda mfupi baada ya kukamilisha kuchimba kaburi hilo ndugu wanaodaiwa wa upande wa mama mzazi wa marehemu waliwawavamia wachimba kaburi na kuwalazimisha kulifukia .
 
Waombolezaji waliokuwa msibani nyumbani kwa bibi ya marehemu baada ya kutaarifiwa tukio hilo lililotokea makaburini walitimua mbio na kuelekea makaburini na kukuta baadhi ya wanandugu upande wa mama wakimalizia kufukia kaburi hilo.
 
Walipoulizwa sababu za kufukia kaburi hilo, walianza kufoka ndipo inadaiwa kundi la ndugu wa mama wa marehemu waliibuka na kuanza kuwashambulia kwa kuwacharaza fimbo ndugu wa baba mzazi wa marehemu .
 
Hadi sasa mwili wa mrehemu huyo umehifadhiwa mochari katika Hospitali ya Wilaya ya Mpanda hadi hapo pande hizo mbili zinazovutana zitakapoafikiana ndipo ufanyiwe maziko .

0 comments:

Post a Comment