Taarifa kwa vyombo vya Habari
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Telephone : 255-22-2114512, 211689
E-mail : ikulumawasiliano@yahoo.com
E-mail : press@ikulu.go.tz
Fax : 255-22-2113425
PRESIDENT’S OFFICE,
THE STATE HOUSE,
P.O. BOX 9120,
DAR ES SALAAM.
Tanzania
Ni ukosefu wa adabu kuwatukana waasisi wa Tanzania - JK
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho
Kikwete amesema kuwa ni utovu wa nidhamu na ukosefu wa adabu kuwa baadhi
ya Watanzania kuwatukana, kuwadhihaki na kuwakejeli Waanzilishi wa
Taifa la Tanzania, Hayati Julius Nyerere na Hayati Sheikh Abeid Amaan
Karume.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa viongozi hao wawili wameifanyia
Tanzania mambo mengi, mambo makubwa na mambo ya kihistoria kiasi cha
kwamba Watanzania wanao wajibu wa kudumisha na kuenzi heshima yao kwa
namna ya kudumu.
Akizungumza na Wahariri wa baadhi ya vyombo vya habari usiku wa jana,
Jumatano, Aprili 16 katika mahojiano maalum ya kuadhimisha Miaka 50 ya
Muungano, Rais Kikwete amesema: “Ni kukosa adabu na ni utovu
mkubwa wa nidhamu kwa Mtanzania yoyote kuwatukana, kuwadhihaki ama
kuwakejeli waasisi wa Taifa letu. Hawa ni watu ambao waliifanyia nchi
yetu mambo makubwa,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Mzee Karume yule aliongoza Mapinduzi yaliyoondoa dhuluma
na uonevu pale Visiwani. Waafrika walio wengi walikuwa wanaonewa sana
pale Tanzania Visiwani, pengine watu wamesahau, lakini hata pale
walipokuwa wanashinda uchaguzi bado walikuwa hawapewi nafasi ya kuongoza
maisha yao wenyewe.”
Amesisitiza Rais Kikwete: “Ni ukosefu wa adabu kwa yoyote
kumshutumu mtu aliyejitolea kiasi hicho ili kubadilisha mfumo dhalimu
na kujenga maisha na mazingira ya maisha bora kwa wengi.”
“Mzee Nyerere yule ametuachia Taifa moja, lililoungana,
lenye umoja, lenye amani na mshikamano. Misingi ambayo aliijenga yeye
ndiyo imeendelea kuongoza Taifa letu kwa miaka yote hii. Viongozi
wengine wote ambao wamemfuata yeye – Mzee Mwinyi, Mzee Mkapa na sasa
mimi mwenyewe, tumefuata na kuongozwa na misingi hii. Na siku nchi yetu
inaamua kuipuuza misingi hiyo, tutaingia katika matatizo makubwa.”
Rais Kikwete ametoa msimamo huo baada ya kuwa ameulizwa kuhusu
matusi, kejeli, dhihaki ambazo zimekuwa zinaonyeshwa na wajumbe wachache
wa Bunge Maalum la Katiba juu ya waasisi hao wa Tanzania na Wabunifu
Wakuu wa Muungano wa Tanzania.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
17 Aprili, 2014
0 comments:
Post a Comment