JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limepiga marufuku watoto wadogo kwenda kuogelea kipindi cha Sikukuu ya Pasaka.
Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema
jana kuwa watoto wadogo hawataruhusiwa kuogelea mpaka kuwe na mlinzi
ambaye atakuwa nao na anayejua kuogelea.
Alisema hali hiyo inatokana na mvua zinazoendelea kunyesha, hivyo bahari haitakuwa shwari.
“Kutokana na hali ya hewa ilivyo pamoja na sababu za kiusalama na
matishio mbalimbali katika ukanda wa Afrika ya Mashariki, tumepiga
marufuku watoto kuogelea na kwenda disco toto katika kumbi mbalimbali
kwa kuwa sifa za kumbi kizo hazikidhi viwango vya kiusalama,” alisema.
Aliongeza kuwa madereva wanatakiwa kuzingatia sheria za usalama
barabarani ikiwa ni pamoja na kutoendesha vyombo vya moto kwa mwendo
kasi, wasiwe walevi, magari au pikipiki zenye sauti kali/zenye kuleta
mshtuko nazo ni marufuku.
Pia Kamanda Kova aliwataka wananchi wanapoona dalili zozote au
maandalizi ya uvunjifu wa amani watoe taarifa mapema iwezekanavyo
katika vituo vya karibu, ili hatua zichukuliwe haraka.
“Mtu yeyote atakayeonekana au atakayesababisha uvunjifu wa amani au
madhara yoyote atawekwa ndani mpaka sikukuu iishe na atapelekwa
mahakamani,” alisema.
Alisema jeshi hilo limejipanga vema, kwani kuanzia saa 10 jioni
kutakuwa na doria itakayofanywa angani kwa kutumia helikopta ya Jeshi
la Polisi kuangalia hali ya usalama katika Jiji la Dar es Salaam, pia
kutakuwa na doria za pikipiki na doria za miguu katika barabara zote
muhimu.
Pia alisema vikosi vyote vikihusisha askari wa vyeo vyote vitakuwa
barabarani saa sita kabla ya mkesha wa Pasaka pamoja na kutumia Kikosi
cha FFU kikijumuisha askari wa magari ya washawasha, askari wa Mbwa na
Farasi.
“Wananchi wanashauriwa kusherehekea Sikukuu ya Pasaka katika ngazi ya
familia au kukusanyika katika mitaa kwa amani,” alisema Kova.
0 comments:
Post a Comment