pagead2.googlesyndication.com pagead2.googlesyndication.com

JK atoa msamaha kwa wafungwa 3967, awanyima msamaha majangili


Rais ametoa msamaha huo kwa mujibu wa madaraka aliyopewa katika Ibara ya 45 ya Katiba ya nchiDar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete ametoa msamaha kwa wafungwa 3,967 katika magereza mbalimbali nchini lakini msahama huo unawaweka kando waliofungwa kwa makosa ya ujangili.Msamaha huo ambao ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, pia hautawahusu wafungwa waliohukumiwa kunyongwa, waliohukumiwa na adhabu hiyo ikabadilishwa kuwa kifungo cha maisha, wanaotumikia kifungo cha maisha na wenye makosa ya biashara ya dawa za kulevya.

Katika taarifa iliyotolewa jana na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe alisema Rais ametoa msamaha huo kwa kutumia madaraka aliyopewa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano, ibara 45, kifungu cha 1(d).
“Wengine ambao hawahusiki na msahama huo ni wafungwa waliopatikana na makosa ya kupokea au kutoa rushwa na wanyang’anyi wa kutumia silaha,” alisema alisema Chikawe.
Wengine ambao hawakupewa msamaha ni waliopatikana na makosa ya kunajisi, kubaka na kulawiti, waliohukumiwa kwa kuwapa mimba wanafunzi wa shule za msingi na sekondari  ambao walitenda kosa hilo wakiwa na miaka 18 na kuendelea na wezi wa magari wa kutumia silaha.
Pia  wamo waliowahi kutoroka au kujaribu kutoroka wakiwa chini ya ulinzi magerezani, waliowahi kupata msamaha wa Rais  na ambao bado wapo magerezani kutumikia sehemu ya kifungo kilichobaki na wafungwa wa makosa ya biashara haramu ya kusafirisha binadamu na wabadhirifu wa fedha za Serikali.
Wanaonufaika
Chikawe alisema wafungwa watakaonufaika na msamaha huo ni wagonjwa wa Ukimwi, kifua kikuu na saratani pamoja na wazee wenye umri wa miaka 70 au zaidi.
 “Wafungwa waliosamehewa ambao ni wagonjwa na wazee wamethibitishwa na jopo la waganga lililo chini ya uenyekiti wa waganga wakuu wa mikoa na wilaya,” alisema Chikawe.
Alisema wengine walionufaika na msahama huo ni wanawake walioingia magerezani wakiwa na mimba na watoto wanaonyonya na wasionyonya, wenye ulemavu wa mwili na akili ambao wamethibitishwa na jopo la waganga katika mikoa na wilaya.
Chikawe alisema wafungwa wote waliopata misamaha ya kupunguziwa adhabu, wataendelea kutumikia kifungo kwa miaka iliyobaki.


“Ni mategemeo ya Serikali wafungwa walioachiliwa huru watarejea katika jamii na kushirikiana na wananchi wenzao katika ujenzi wa taifa na kwamba watajiepusha kutenda makosa ili wasirejee tena magerezani,” alisema Chikawe.

0 comments:

Post a Comment