Mahakama ya kijeshi nchini Somalia ilimuhukumu mwanachama wa
al-Shabaab, Awiye Ahmed Jama, adhabu ya kifo siku ya Jumatatu (tarehe 7
Julai) baada ya kugundua kwamba alihusika kwenye kuishambulia kwa mabomu Hoteli ya Makkah Al-Mukarama mwezi Novemba, liliripoti gazeti la Al-Shahid la Somalia.
"Awiye Ahmed Jama aliiambia mahakama kwamba yeye ni mwanachama wa
al-Shabaab. Pia alikubali kwamba alihusika na mlipuko kwenye hoteli ya
Makkah al-Mukarama," alisema mwenyekiti wa mahakama ya kijeshi ya
Somalia, Kanali Liban Ali Yaow. "Ni mhalifu hivyo mahakama imemuhukumu
adhabu ya kifo."
Jama, mwenye umri wa miaka 25, alikuwa amepokea mafunzo kwa miezi
tisa kwenye mji wa Bulo Marer unaoshikiwa na al-Shabaab kabla ya
kujaribu mashambulizi hayo, ilisema mahakama hiyo kwa mujibu wa gazeti
la Mareeg la Somalia.
Jama alikamatwa tarehe 8 Novemba 2013, baada ya kujaribu kujilipua
ndani ya hoteli hiyo kwa kutumia kompyuta ndogo ya kupakata iliyotegwa
bomu. Dakika kadhaa kabla ya kukamatwa kwake, al-Shabaab ilifanya
mashambulizi ya bomu lililotegwa kwenye gari nje ya hoteli hiyo, ikawaua
watu wanne na kuwajeruhi 15.
Miongoni mwa waliokufa alikuwa ni mmoja wa wanadiplomasia wa ngazi za
juu wa Somalia, kaimu balozi wa zamani mjini London, Abdulkadir Aden
Ali "Dhuub".
0 comments:
Post a Comment