pagead2.googlesyndication.com pagead2.googlesyndication.com

Watumiaji mihadarati 1,714 wapatiwa tiba Dar

WATUMIAJI wa dawa za kulevya zaidi ya 1,714 wapo kwenye matibabu ya dawa aina ya Methadone inayotolewa jijini Dar es Salaam.
Dawa hizo hutolewa kwenye vituo maalum vilivyopo ndani ya hospitali za Mwananyamala, Temeke na Muhimbili, ambako watumiaji hufika kupata dozi kila siku.
Waandishi wa habari waandamizi wanaofanya mradi wa Fellowship unaopinga matumizi ya dawa za kulevya chini ya ufadhili wa Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF), walielezwa hayo wakati wa mafunzo yanayoendelea kabla ya kuanza kwa mradi huo.
Akizungumza na waandishi hao, Dk. Cassian Nyandidi anayesimamia utoaji wa Methadone, alisema lengo la ugawaji wa dawa hiyo ni kuokoa kundi la vijana linaloangamia kutokana na matumizi ya dawa za kulevya.
Kwa mujibu wa mtaalam huyo, kituo cha Mwananyamala kinahudumia waathirika 696, Temeke 119 na Muhimbili 899.
“Watumiaji wa dawa za kulevya ni wenzetu, wanahitaji msaada wetu, hasa wa matibabu, tukiwaacha tunaongeza ukubwa wa tatizo badala ya kudhibiti au kumaliza kabisa,” alisema Dk. Nyandidi.
Aliishauri jamii kuondokana na fikra potofu juu ya dawa hiyo huku akiipongeza serikali kwa kuruhusu tiba hiyo, kwani waathirika wengi wa dawa za kulevya ni vijana ambao ndio nguvu kazi ya taifa.

0 comments:

Post a Comment