WAZIRI
wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, amesema kivuko kitakachofanya safari zake
Dar es Salaam hadi Bagamoyo kinatarajiwa kuanza kutoa huduma kwa
wananchi wiki tatu zijazo.
Dk. Magufuli alitoa kauli hiyo jana alipotembelea karakana ya
kutengeneza na kukarabati meli na vivuko iliyopo Kurasini kwa ajili ya
kuangalia maendeleo ya ukarabati wa kivuko cha Mv. Kigamboni yaliyoanza
Agosti 14 mwaka huua.
Alisema mpaka sasa hivi wameshawasiliana na kampuni ya Denmark ambayo
ndio imepewa zabuni ya kutengeneza kivuko hicho na wamewaambia
wameshakidumbukiza majini tayari kwa safari ya kuja nchini.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, Kivuko hicho kimepewa jina la MV Dar es
Salaam na kitakuwa na uwezo wa kubeba watu zaidi ya 300 kinatarajiwa
kupunguza foleni na adha ya usafiri kwa wakazi wa maeneo ya Tegeta,
Bunju na Bagamoyo.
Akizungumzia kuhusu ukarabati wa kivuko cha MV Kigamboni, Dk.
Magufuli alionekana kuridhika nao na kusema Jeshi la Wanamaji ambalo
ndilo lilipewa zabuni ya kukikarabati limeonyesha uzalendo wa hali ya
juu na kupunguza gharama.
Alisema kama kingepelekwa Mombasa zingetumika sh. milioni 600, lakini
baada ya maamuzi ya kutengenezewa hapa nchini ni theluthi ya hela
zilizotengwa ndizo zimetumika (sh milioni 200).
Kutokana na hali hiyo alilizawadia jeshi hilo ng’ombe wawili ambao
alimkabidhi Mkuu wa Jeshi hilo, Brigedia Jenerali Regastian Laswai na
kuongeza kuwa hali hiyo iwe fundisho kwa taasisi mbalimbali zinazopenda
kupeleka vitu kukabatiwa nje ya nchi wakati tuna wataalam wa kutosha
hapa nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa), Mhandisi
Marecellin Magesa, alisema pamoja na ukarabati huo bado nia ya Serikali
ipo palepale ya kuongeza kivuko kingine kitakachosaidiana na vivuko
vilivyopo na tayari sh bilioni 3.7 zimetengwa kwa ajili ya ununuzi wa
kivuko hicho.
0 comments:
Post a Comment