Waombolezaji katika ibada ya mazishi ya Martha Ngunjiri, 6, kijiji cha
Tambaya, Kaunti ya Nyeri
POLISI katika Kaunti ya Nyeri wanamzuilia mwanamume aliyekiri kuua watoto watano wachanga katika kijiji cha Tambaya, eneo la Mukurwe-ini.
Mshukiwa
alikamatwa Jumanne mchana alipojiunga na wanakijiji waliokuwa wakiandaa
mazishi ya mtoto aliyeuawa, na akadai yeye ndiye aliyemuua mtoto huyo wa
kike, Martha Ngunjiri aliyekuwa na umri wa miaka sita.
Mshukiwa huyo
pia aliwaambia wakazi hao waliokuwa wamepigwa na mshangao kuwa alikuwa
amewaua watoto wengine wanne awali katika kijiji jirani cha Gatura na
alikuwa na mipango ya kuua wengine sita.
Wanakijiji hao walisema mshukiwa huyo aliwaeleza kwamba alikuwa anafuata agizo la majini waliomwambia lazima aue watoto kadhaa.
Wanakijiji
hao waliwaita maafisa wa polisi kutoka kituo cha Mukurwe-ini ambao
waliwasili na kumwokoa mshukiwa kutoka mikononi mwa wakazi wa Tambaya
waliokuwa wakitaka kumuua.
Babake
msichana aliyeuawa, Bw Charles Ngunjiri alisema kuwa Alhamisi iliyopita
alipigiwa simu na jirani yake aliyemwambia kuwa mtoto wake wa pili
alitumbukia kwenye tangi la maji la lita 2,800 na akafariki.
Alisema
walichukulia binti yao alianguka kwenye tangi kwa ajali na hivyo basi
wakaanza mipango ya mazishi hadi Jumanne wakati mwanamume huyo
alipojitokeza.
Alisema baada
ya mwanamume huyo kukiri mauaji na kukamatwa, waliamua kufanyia mwili
wa binti yao ukaguzi wa maiti ili kubaini kiini cha kifo chake.
Ripoti
iliyotolewa na madktari ilionyesha kuwa msichana huyo alifariki kwa
kunyongwa na wala sio kufa maji ilivyodhaniwa awali. “Alinyongwa kisha
akatupwa kwenye tangi la maji,” akasema Bw Ngunjiri.
Akisumulia
kuhusu jinsi mshukiwa huyo alivyoungama, mjomba wa msichana huyo Bw
Peter Kibara alisema walimwona akiwa amesimama bomani na baadaye mchana
walipokuwa wakichimba kaburi alionekana kuhangaikahangaika.
“Tulianza
kuchunguza mienendo yake na alipogundua tunamfuatilia, alianza kukimbia
nasi tukamfuata. Tulipomkamata na kuanza kumhoji ndipo alikiri yale
aliyotenda na kuanza kutusihi tusimuumize,” akasema Bw Kibara. Alisema
hata baada ya kukamatwa na polisi alizidi kusisitiza yeye ndiye muuaji.
Afisa wa
polisi katika kituo cha Mukurwe-ini ambaye aliomba asitajwe
alithibitisha kuwa mshukiwa huyo yuko kizuizini na atapelekwa mahakamani
Alhamisi.
“Mshukiwa
amekiri kuwa alimuua msichana huyo, na pia ametuambia mambo mengine
mengi na tunajaribu kuyachanganua,” akasema afisa huyo.
0 comments:
Post a Comment