Kwa
muda sasa kumekuwapo na tuhuma zinazohusu "wizi" wa fedha za akaunti ya
escrow iliyofunguliwa katika Benki Kuu ya Tanzania mwaka 2006. Akaunti
hiyo ilifunguliwa kwa ajili ya kuhifadhi fedha zilizokuwa zikilipwa na
Shirika la Umeme Tanzania {TANESCO} kwa kampuni ya kufua umeme ya IPTL.
Chimbuko la akaunti hiyo ni mgogoro wa tozo hiyo kwamba iligubikwa na
utata baada ya kudaiwa kwamba Tanesco ilikuwa ikitozwa fedha nyingi
kuliko inavyostahili.
Tuhuma
za huo "wizi" hata hivyo hazikuishia tu kwa wahusika wakuu yaani
makampuni ya umeme, bali zimetiririshwa hadi kwa watu binafsi ambao
kimsingi hawana uhusiano wowote na mgogoro huo wa malipo na wala
kuhusika kwa njia yoyote na hicho kinachodaiwa kwamba ni uporaji wa
fedha za akaunti hiyo ya Escrow.
Akaunti
Escrow ni akaunti ya amana ambayo inawekwa chini ya uangalizi wa mtu wa
tatu ili huyo mwangalizi aikabidhi kwa mlengwa pale tu masharti kadhaa
yatakapokuwa yamekamilishwa. Hivyo basi akaunti hiyo maalum ya amana
ilifunguliwa na kuwekwa chini ya Benki Kuu kama wakala anayesubiria
kutekelezwa kwa masharti maalumu ili aikabidhi kwa wenye kumiliki fedha
hizo watakapomaliza tofauti zao.
Ni
vizuri kuliangalia suala hili la akaunti maalum ya amana kwa namna
ambayo itawafanya wale wenye kiu ya kutaka kujua ukweli kukidhi hamu
yao.
Fedha
iliyokuwa ikiwekwa katika akaunti hiyo ni tozo ya uwezo wa mitambo ya
kufua umeme ambayo kampuni ya IPTL ilikuwa ikiitoza Tanesco. Baada ya
Mahakama ya Kimataifa ya Utatuzi wa Migogoro ya Uwekezaji (ICSID)
kupunguza tozo ya IPTL kutoka USD 3.6million kila mwezi mpaka USD
2.6million kila mwezi baadaye TANESCO ilishauriwa vibaya na wanasheria
kwamba tozo hiyo bado ni kubwa kuliko mkataba baina ya IPTL na TANESCO
Mei 26, 1995 unavyo eleza.
Ubishani
uliozuka kati ya mtoa huduma ya umeme yaani IPTL na mtumia huduma ya
umeme yaani Tanesco ndio uliosababisha kufunguliwa kwa akaunti hiyo
maalum ya amana yaani escrow account katika Benki Kuu ya Tanzania {BoT}
kama njia salama ya kutunza fedha hizo hadi mgogoro utakapokuwa
umetatuliwa.
Ni
muhimu kufanya hivyo ili kuhakikisha kwamba mtoa huduma yaani IPTL
hasitishi kufua umeme na mtumiaji wa umeme yaani Tanesco naye hakosi
umeme wa kuuza kwa walaji wake. Hiyo ni busara ya kibiashara. Fedha hizo
zililipwa katika akaunti hiyo maalum kutokana na hati za madai au
ankara kutoka kwa mtoa huduma na si vinginevyo.
Kitu
kimoja kilichojitokeza wazi ni kwamba suala la akaunti hiyo maalum
limekuwa likibeba sura mpya kila kukicha na la kusikitisha zaidi ni
kwamba vyombo vya habari vilivyo vingi ama vimekuwa vikipotosha kwa
makusudi au kwa kutokuelewa mada yenyewe ipasavyo. Vipo vyombo vya
habari kwa mfano ambavyo vimedai kwamba "Benki ya Standard Chartered
ndiyo mmiliki wa mitambo ya IPTL baada ya kupewa mamlaka hayo na
mahakama - Deed of Assignment- inayoiruhusu kuchukua na kumiliki mali za
IPTL kutokana na kushindwa kulipa mkopo.
Aidha
kwa mujibu wa gazeti la Mawio la Alhamisi Novemba 20-26, 2014 mkataba
huo uliipatia benki ya SCB haki za IPTL ndani ya mkataba wa kuuziana
umeme (PPA) na kumiliki mtambo wa kuzalisha umeme wa IPTL.
Kwa
mujibu wa gazeti hilo la Mawio Benki ya Standard Chartered inaidai
Tanesco dola za Marekani 258.7 milioni kama deni linalotokana na gharama
za umeme uliozalishwa na IPTL na dola za Marekani 138 milioni
zinazotokana na mkopo pamoja na riba. Kwa mujibu wa uchambuzi wa Mawio
madai hayo ni halali kwa mujibu wa sheria.
Kwa
mujibu wa gazeti hilo "nyaraka za serikali zinaonesha kuwa PAP
iliamuriwa kulipa wadai wote wa IPTL lakini haikuilipa Benki ya Standard
Charted ambayo inajitangaza kuwa ni moja ya wadai.
Ni
vyema na busara kuanza uchambuzi huu kwa kufanya nukuu hiyo muhimu sana
kutoka katika gazeti la kila wiki la Mawio kwa sababu inatusaidia
kuonyesha waziwazi kwamba hiki kinachodaiwa kwamba ni kashfa ya fedha za
Escrow kina sura nyingi sana kulingana na maslahi yanayolengwa
kutetewa.
Katika
muktadha huu ni wazi kwamba anayetetewa hapa ni Benki ya Standard
Chartered ambayo inadaiwa kwamba ndiyo yenye haki ya kulipwa fedha
kutoka katika akaunti ya Escrow na kwa mantiki hiyo imeishitaki Serikali
ya Tanzania katika Mahakama ya Uingereza.
Deni
linalodaiwa kwamba Tanesco inadaiwa na Standard Chartered la dola za
Marekani linatokana na gharama za umeme uliozalishwa na IPTL na nyingine
ni mkopo na riba. Inashangaza kwamba Tanesco inawezaje kudaiwa na Benki
ya Standard Chartered wakati aliyezalisha umeme ni IPTL? Abrakadabra
hiyo ndiyo inayomfanya ye yote yule mwenye akili timamu kutambua kwamba
kuna mchezo wa kiini macho unaochezwa na benki hiyo dhidi ya Tanzania.
Ni
wazi kabisa kwamba benki hiyo inalazimisha kuwapo na mgogoro wa kuhusu
akaunti ya Escrow kwa lengo moja tu nalo ni kuhakikisha kwamba wanapata
nafasi ya kukwapua hizo fedha wanazodai kwamba sio halali kuchukuliwa na
IPTL. Kwamba zikichukuliwa na Benki ya Standard Chartered ambayo
haijazalisha umeme wala kuwa na ushahidi wowote wa kushiriki katika
kuzalisha umeme ni halali kabisa na zikichukuliwa na IPTL ambayo
imezalisha umeme na inayo mikataba ya kuuziana umeme na Tanesco si
sahihi, ni wizi, ni ujambazi ni hila na kashfa. Hii inahitaji maelezo
zaidi kushinda haya yanayotolewa hivi sasa.
Ukweli
wa mambo ni kwamba mazungumzo kuhusu fedha za Escrow na hususan habari
za kujaribu kuonyesha kwamba umiliki wake ni batili una lengo moja tu
nalo ni kuandaa mazingira kwa ajili ya Benki ya Standard Chartered
hatimaye kuzichukua fedha hizo kwa kutumia kigezo cha kwamba
imemilikishwa mitambo ya IPTL na kwamba ndiyo iliyokuwa na haki ya
kulipwa tozo ya uzalishaji umeme na si kampuni nyingine yoyote. Hivyo
ndivyo kampuni hiyo inavyodai katika kesi iliyofungua dhidi ya Serikali
ya Tanzania huko Uingereza.
Benki
ya Standard Chartered inatumia mbinu mbalimbali ili kuhakikisha
inafikia lengo lake la kukwapua fedha za kigeni si chini ya dola milioni
200 kutoka kwa serikali ya Tanzania. Moja ya njia inayotumia ni
propaganda ambayo hupenyezwa katika vyombo vya habari kwa kutumia
majukwaa mbalimbali.
Moja
ya njia zinazotumika ni kujaribu kuufanya umma uamini kwamba fedha
zilizotoka katika ufungaji wa akaunti hiyo ya Escrow zimeibwa na kwamba
wahusika katika huo wizi ni pamoja na viongozi kadhaa wa Serikali.
Kinachosikitisha
zaidi ni kwamba kuhusishwa kwa watu hao kunafanyika bila hata ya
kuwataka wajieleze kama wanaelewa kile wanachotuhumiwa nacho. Wafadhili
wa propaganda hizo hawakubali kujitokeza hadharani moja kwa moja kwa
kuhofia kuumbuliwa. Matukio huchukuliwa si kwa ujumla wake bali upande
mmoja na kuyatangaza kwa namna ya kukidhi matakwa na matarajio yao tu.
Tumezoea
kuambiwa kwamba wakati suala linapokuwa mahakamani kwa ajili ya
kupatiwa ufumbuzi basi si sahihi kuendelea kulijadili kwenye vyombo vya
habari kwani kwa kufanya hivyo ni sawa kabisa na kuingilia uhuru wa
mahakama. Ni wazi kwamba hata suala linapokuwa katika uchunguzi au
upelelezi uwe kwa kutumia tume maalum au makachero basi ni muhali
kulizungumzia hadharani na kuwatuhumu na hata kuwahukumu watu kwa
ujasiri usio na kikomo kwamba ni wezi au mafisadi au wakumbatiaji wa
madhila hayo yote. Hili linafanyika kila siku kupitia vyombo vya habari
na chimbuko lake ni baadhi ya wabunge na wanasiasa ambao hufanya hivyo
huku wakitumia kila aina ya takwimu za kweli na za kughushi au kubuni tu
kichwani.
Nini
kinachowafanya au kuwapa jeuri hawa watu wanaowatuhumu na kuwahukumu
wengine bila ya kujali kwamba hilo halitakiwi wala kupaswa kufanyika
bila ya kupitia katika vyombo vya sheria ili kutoka fursa kwa wengine
kujitetea? Swali hilo linastahili kujibiwa kwa umakini mkubwa ili
kubaini kama kweli hao wanaodai kwamba wanapigania haki ya kiuchumi ya
Watanzania ni kweli wanafanya hivyo kwa dhati ya moyo wao kabisa bila ya
kuwa na nia nyingine iliyojificha ambayo hawathubutu kuiweka hadharani
kwani kwa kufanya hivyo watageuka viroja.
Pamoja
na kwamba kuna kesi mahakamani dhidi ya Serikali ya Tanzania ni wazi
kwamba ukiwauliza Standard Chartered kilichowapeleka mahakamani wanasema
kwamba wanaionea nchi yetu huruma, Hata hivyo, kamwe hakuna
atayekuambia kwamba amekuja hapa kwa ajili ya kujaribu bahati yake kama
wanaweza kufanya mbinu wakatengeneza fedha ya bure. Ili kufanikisha
malengo yao tuhuma hurushwa kwa yeyote na popote. Ili kufanikisha
malengo hayo mtu yeyote yule aweza kuunganishwa katika lolote lile ili
kufikia lengo.
Ni
kwa utaratibu huo huo ndio tunashuhudia jinsi jitihada za Profesa Anna
Tibaijuka za kuendeleza mtoto wa kike kielimu zinavyopakwa matope na
kukejeliwa mno kwa sababu tu ameomba msaada mahali na akaupata.
Tujiulize
inakuwaje wanasiasa wetu wanathubutu kumhukumu Profesa Tibaijuka na
kumuita kila aina ya majina machafu. Ametuhumiwa kwamba ni mwizi eti kwa
sababu aliomba msaada kwa ajili ya shule ya Babro Johansson ambayo ni
kwa madhumuni ya kuwasaidia watoto wa kike kupata elimu.
Profesa
Tibaijuka aliomba msaada kwa barua rasmi miaka kadhaa iliyopita na
kampuni hiyo haikuweza kumsaidia mapema kutokana na ukata na ni hivi
majuzi hali ilipokuwa njema ndipo ikatoa msaada huo.
La
kustaajabisha ni kwamba msaada huo haukuwa ni siri na ulitolewa kwa
uwazi mkubwa bila ya kificho. Sasa huo ujambazi wa Profesa Tibaijuka
umetokea wapi? Kosa lake ni kupatiwa fedha alizoomba kwa ajili ya
kuisaidia shule ambayo aliianzisha?
Tunajiuliza
hapa, baada ya VIP kuuza hisa zake kwa PAP na kulipwa na PAP stahili
yake, ilifanya kosa gani kutoa msaada kwa shule ya Babro Johansson?
Mahitaji
na umuhimu wa elimu yanajulikana. Viongozi wanahimiza kila leo umuhimu
wa Watanzania kubadilika kuchangia Maendeleo ya Elimu badala ya harusi
na sherehe nyinginezo. Leo hii anatokea Mtanzania anaomba msaada wa
kuendeleza elimu na anapatikana Mtanzania anakubali kuchangia vizuri
maendeleo ya elimu, wawili hawa baadhi ya wanaojiita viongozi wa siasa
tena wenye kutaka kuchukua madaraka ya juu kuiongoza nchi, wanalalamika
na hata kutamani kutoa roho ya mtu! Watanzania tuzipime dhamira zao. Ni
wadanganyifu wasio na uelewa halisi wa matatizo na vipaumbele vya taifa
na hivyo kukosa dhamira thabiti ya kuyashughulikia. Wanasukumwa zaidi na
tamaa zao binafsi.
Kwa
wanaong'ang'ania kudai damu za baadhi ya watu kutokana na hukumu ambayo
wao wameipitisha baada ya kufanya kila kitu wao ikiwa ni pamoja na
kutuhumu, kupeleleza, kufungua mashitaka, kusikiliza kesi na hatimaye
kuhukumu na sasa kutaka kukaza hukumu kwa njia yoyote ile hakuna jambo
zuri na jema kama kufanya kile wanachotaka wao yaani kukubali kwamba
fedha zote katika akaunti maalum ya escrow ni za serikali na kwamba
lazima zirudi serikalini.
Hata
hivyo, wakubwa hao hawataki kurudi nyuma na kujiuliza ni kwa njia gani
fedha hizo zimeingia katika akaunti hiyo. Aidha, hawataki kujiuliza
kwamba kama Tanesco ndio ilikuwa ikitumbukiza fedha katika akaunti hiyo,
ilikuwa ikifanya hivyo kwa kutumia vigezo gani. Swali linguine la
kujiuliza, je Serikali hutunza pesa zake kwenye Account zake Benki Kuu
au kwenye Escrow Account?
Hawaoni
mantiki ya kutulia na kujibu swali la msingi kwamba kama Tanesco
ingelikuwa inatumbukiza fedha katika akaunti hiyo kwa ajili ya
kugharamia tozo la uwezo wa mitambo kuzalisha umeme sasa
inakuwaje fedha hizo zirudi tena Tanesco? Ni maswali ambayo wanaojiamini
kwamba ukweli wanao wao tu hawataki kuyajibu hata kidogo kwani kwa
kufanya hivyo watakuwa wanaumaliza utamu wa mchezo wao wa kuigiza.
Fedha
hizo zinatakiwa zirudi Tanesco ili Benki ya Standard Chartered
izichukue kwa madai kwamba ndiye mmiliki halali wa IPTL na kwamba kuna
deni kama ilivyoainishwa awali katika makala haya.
Kutokana
na ufafanuzi huo hapo juu ni wazi basi kwamba Tanesco ilikuwa ikilipia
gharama za huduma ambayo ilikuwa inaipata kutoka kwa IPTL. Hilo halina
ubishi.
Lakini
pia suala lingine ambalo sasa halina ubishi japo halisemwi makusudi kwa
sababu za upotoshaji ni kwamba katika makampuni yote ambayo yanauzia
umeme TANESCO, IPTL ndiyo kampuni pekee inayotoza kiwango kidogo cha
malipo ya uwekezaji (capacity charges). Suala la kujiuliza hapa ni
inawezekanaje IPTL ambayo inatoza kiwango kidogo cha capacity charges
ionekane “kuiibia” Serikali kwa kulipwa halali yake wakati makampuni
mengine yanatoza capacity charges kwa kiwango cha juu zaidi ya IPTL na
hakuna malalamiko.
Swali
la kujiuliza ni kwamba ni kitu gani kinachowasukuma watuhumu kutafuta
kila njia ya kuonyesha kwamba kuna hitilafu kubwa sana kwa namna ambavyo
suala la akaunti hiyo lilivyohitimishwa?
Ukifuatilia
kwa karibu na umakini jinsi ambavyo tuhuma zimekuwa zikitolewa ni
kwamba kinacholengwa ni fedha zilizokuwa katika akaunti maalumu ambazo
ni tozo ya uwezo wa ufuaji wa umeme. Fedha hizo zinagombewa na Benki ya
Standard Chartered ambayo ina matawi yake hapa nchini.
Benki
hiyo inatumia kila njia kujaribu kuonesha kwamba fedha zilizokuwapo
katika akaunti ya Escrow ni fedha ya Serikali. Kwa mantiki hiyo
inachojaribu kufanya Benki hiyo ni kuonyesha kwamba fedha akaunti ya
escrow si kwa ajili ya kulipia gharama za uwezo wa mitambo kufua umeme
la hasha. Bali ni fedha za Tanesco na kamwe hakuna anayestahili
kuzipunguza kwa njia yoyote ile.
Cha
kushangaza, hata hivyo, ni kwamba benki hiyo, inayodai kuwa iliikopesha
fedha IPTL, katika madai yake yaliyopo mahakamani, inadai kuwa yenyewe
ndiyo ilistahili kupata fedha zilizokuwa kwenye escrow account! Swali
hapa ni je, hiyo asasi ndiyo Serikali? Je, fedha zilizokuwa kwenye
escrow account zinakuwa za Serikali na siyo IPTL kwa sababu benki hiyo
haijalipwa?
Jitihada
za kutaka kuhalalisha kwamba fedha hizo ni mali ya Tanesco na kwamba
haziwezi kumegwa hata kidogo zinafanywa na Benki ya Standard Chartered
ambayo inataka kutengeneza mazingira ya kuchota fedha kutoka Tanesco kwa
madai kwamba ndiyo inayostahili kuwa mlipwaji wa fedha hizo kutokana na
deni ambalo kwa mujibu wa madai yao ndio walioikopesha IPTL fedha kwa
ajili ya mradi huo wa umeme.
Mchezo
ambao benki hiyo inafanya hapa nchini ni kuhakikisha kwamba vyombo vya
habari vinaandika habari za kuigonganisha serikali na wananchi kwamba
Serikali ni ya mafisadi na inayokumbatia ufisadi, na haina ubavu wowote
wa kupambana na rushwa. Aidha, asasi hiyo imevirubuni baadhi ya vyombo
vya habari kuandika habari kwamba Mahakama za Tanzania haziaminiki na
zinakumbatia ufisadi na kwamba zimekubuhu kwa rushwa.
Cha
kushangaza, tuhuma hizi za rushwa kwa Mahakama za Tanzania zinakuja
muda mfupi tu baada ya benki ya Standard Chartered kuiambia mahakama New
York, nchini Marekani iliposhitakiwa na VIP kuwa Mahakama za Tanzania
ndizo zenye uwezo wa kusikiliza na kutatua migogoro ya IPTL.
Mchezo
ambao Standard Chartered Bank inaufanya ni kutumia vyombo vya habari
kutoa habari zisizo za kweli na za upotoshi ili kuwachochea watu dhidi
ya Serikali yao kutokana na nini kinaendelea ndani ya IPTL. Mambo mengi
yamesemwa na kuandikwa kuhusiana na Mahakama na watendaji wa Serikali
kula rushwa. Madhumuni ya kufanya hivyo ni kutaka kuonyesha kwamba
nchini Tanzania haki haiwezi kutendeka.
Madai
hayo yote, yanatokea wakati Standard Chartered Bank imefungua kesi
London, kwa kisingizio kwamba Mahakama za Tanzania haziwezi kutenda
haki
Kwa
vipi Standard Chartered Bank inatoa madai kulipwa dola za kimarekani
208 milioni kutoka TANESCO (katika kesi ilivyofunguliwa Mahakama ya
usuluhishi (ICSID)) kwa mkopo wa dola milioni 84 kwa IPTL, wakati
Serikali ya Tanzania na TANESCO tayari walikwishalipa takribani dola 200
milioni kwa IPTL kufikia mwaka 2006. Kiasi hicho kingelitosha kulipia
mkopo uliokuwa umechukuliwa na kulipa gawiwo kwa VIP na MECHMAR. Mpaka
mwaka 2013 VIP ilikuwa haijalipwa hata senti moja kwa jina lolote.
Kampuni
ya Mechmar ilitumia fedha zilizodaiwa na IPTL kutoka Serikali ya
Tanzania na TANESCO kwa kujilipa yenyewe na Kampuni ya Wartsila madeni
hewa (kwa makubaliano na benki ya Danaharta na baadaye Standard
Chartered Bank (Hong Kong) Ltd.
Standard
Chartered Bank (Hong Kong) Ltd inajaribu kutekeleza mpango haramu dhidi
ya IPTL kwa kutumia dhamana ya Serikali ya Tanzania na hivyo Serikali
ina sababu za kutaka Standard Chartered Bank ithibitishe kama inaidai
IPTL.
Mpaka sasa ukweli ni kwamba Standard Chartered Bank imekwepa kutoa
ushahidi kuwa ina madai yoyote dhidi ya IPTL na kwa sababu hiyo na
zingine VIP na IPTL/PAP wameifungulia kesi za madai ya fidia na hasara
ya TZS 787bilioni na USD 3bilioni katika Mahakama Kuu ya Tanzania.
(Imeandaliwa na mtandao wa www. habari za jamii.com)
0 comments:
Post a Comment