MASHINE ya kurushia matangazo
ya moja kwa moja na kuchanganya picha, imeibiwa ndani ya ukumbi wa
jengo la Bunge katika mazingira ya kutatanisha, Tanzania Daima
limebaini.
Mashine hiyo (Mixer), mali ya kituo cha Televisheni ya Star TV,
imeibiwa ikiwa imehifadhiwa kwenye chumba maalum cha kurushia matangazo
ya Televisheni na Radio za vituo mbalimbali baada ya kumalizika kwa
Bunge Maalum la Katiba.
Ingawa thamani halisi ya mashine hiyo haijajulikana, lakini inaelezwa
kuwa ina thamani kubwa ya mamilioni ya fedha na haipatikani nchini.
Mbali ya kuiba mashine hiyo, wajanja hao pia wameiba vingamuzi viwili
vilivyokuwa vikitumika wakati wa kurusha matangazo ya moja kwa moja
bungeni.
Uchunguzi uliofanywa na Tanzania Daima, umebaini kuwa mashine hiyo
imeibiwa baada ya kumalizika kwa Bunge Maalum la Katiba na hakuna
aliyenaswa wala kudaiwa kuhusika na wizi huo.
Habari za kiintelejinsia kutoka viwanja vya Bunge, zinasema kuwa
tayari maofisa usalama wa Bunge wameanza kupitia picha za kamera za
Bunge kusaka wezi hao.
Kutokana na kuibiwa kwa mashine hiyo, matangazo ya Televisheni ya
Star TV na zingine zilizokuwa zikishirikiana kutumia kifaa hicho,
yameathirika kwani hayako kwenye ubora unaotakikana.
Wizi huo umeibua maswali kutoka kwa baadhi ya wabunge na watumishi wa Bunge.
Baadhi ya wabunge walisema kwa namna jengo la Bunge lilivyo, hakuna
uwezekano wa mtu kutoka nje ya mazingira ya Bunge kuja kuiba.
"Milango ya Bunge inaingia kwa kadi maalum na muda wote kamera
zinamulika. Mwizi huyo ameingiaje na ametokaje bila kuonekana," alihoji
mmoja wa watumishi wa Bunge.
Katibu wa Bunge, Thomas Kashilila, alikiri kuibiwa mashine hiyo anazo na Bunge imeanza kuzifanyia kazi.
Alisema anataka kupata maelezo ya kutosha kwa waandishi na
wafanyakazi wa Star TV waliokuwa kazini wakati Bunge Maalum la Katiba
lilipoahirishwa na namna walivyoamua kuiacha mashine hiyo iendelee
kubaki ndani ya jengo la Bunge bila ofisi yake kuwa na taarifa.
“Kweli kuna hiyo mashine imeibiwa na jana nilipata barua rasmi ya
kujulishwa kupotea kwa kifaa hicho. Nimetoa maelekezo kwa askari na
wana usalama wa hapa kuanza kufuatilia na hatimaye tutalazimika
kuangalia kwenye kamera kuanzia tarehe ya Bunge hilo lilipoahirishwa
hadi sasa,” alisema Dk. Kashilila.
0 comments:
Post a Comment