Na Oyuke Phostine -
Shinyanga
Serikali imetoa wito kwa Ofisi za
wakuu wa mikoa kuhamasisha uwekezaji katika sekta ya viwanda kwenye mikoa yao
ili kuweza kukuza uchumi wa mikoa husika na taifa kwa ujumla.
Wito huo umetolewa na Bw. Paul
Sangawe, Naibu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, anayeshughulikia Biashara za
Kimataifa wakati akiongoza timu ya wataalam kutoka ofisi hiyo iliyokuwa ikifanya ukaguzi wa miradi ya maendeleo
inayotekelezwa na Serikali na sekta binafsi katika mikoa ya Shinyanga, Mara,
Simiyu, na Mwanza.
Bw. Sangawe, alisema kuwa Wajibu
wa Serikali ni kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kuwekeza. Alifafanua kuwa, moja ya vipaumbele katika Mpango
wa Maendeleo wa Miaka Mitano ambao utekelezaji wake unaishia 2015/16, ni
miundombinu ili kufungulia fursa za ukuaji wa uchumi.
Aidha, Mpango wa Maendeleo wa Miaka
Mitano unaofuata kuanzia 2016/17 utalenga katika kuendeleza viwanda. Hivyo, alitoa rai kwa viongozi katika ngazi za
mikoa kuratibu masuala ya uwekezaji hususan katika viwanda ikiwa ni pamoja na
kuhakikisha kuwa uwekezaji huo unawanufaisha wananchi wa maeneo husika kwa
kuongeza fursa za ajira na masoko ya bidhaa za kilimo.
“Uwepo wa viwanda hivi unaonyesha
mwenendo na mwelekeo mzuri wa taifa katika kufungua fursa za maendeleo na
kiuchumi kupitia sekta ya viwanda, hivyo basi iwapo jitihada za kuhamasisha
uwekezaji wa viwanda katika kila mkoa zitatiliwa maanani ni dhahiri kuwa fursa
za ajira zitaongezeka na kasi ya ukuaji uchumi itaongezeka” alisema Bw.
Sangawe.
Akizungumza na timu hiyo ya
ukaguzi wa miradi ya maendeleo ilipotembelea na kukagua kiwanda cha kusindika mafuta
kwa kutumia alizeti na mbegu za pamba cha Jielong Holdings Mkoani Shinyanga, Kaimu
Meneja Utawala Bw. Atanas William alisema kuwa mpaka sasa kiwanda hicho
kinaweza kusindika na kuhifadhi lita milioni 2.4 kwa mwezi.
“Kwa sasa upatikanaji wa mali
ghafi ni wakuridhisha kwa sababu bado tunanunua alizeti kutoka kwa wakulima, na
mbegu za pamba katika vinu vya kuchambua pamba (Ginneries). Tuna mpango wa
kuhamasisha na kuwafundisha wakulima njia bora za kilimo na utunzaji wa mazao ili
kujihakikishia upatikanaji wa mali ghafi yenye ubora zaidi” alisema Bw. Atanas.
Viwanda vingine vilivyotembelewa
ni kiwanda cha Dahong kinachotengeneza nyuzi za pamba na kiwanda cha Xinghua
cha kusindika ngozi mkoani Shinyanga na kiwanda cha nguo cha Mwatex Mkoani Mwanza.
Kiwanda cha Dahong kina uwezo wa kununua tani 12,000 za pamba kwa mwaka na kuzalisha
tani 7 za nyuzi za pamba kwa siku. Kiwanda hiki kimeanza uzalishaji mwezi
Septemba 2014, na nyuzi zote zinazozalishwa zitauzwa nchini China.
Kwa mujibu wa bwana Luke Li, ambaye
ni afisa fedha wa kiwanda hicho, mipango ya baadae ya kiwanda hicho ni kutengeneza
nguo. Bwana Li pia alisema kuwa kuna
mpango wa kujenga kinu cha kuchambua pamba na kutoa mafunzo kwa wakulima ili
kuwezesha upatikanaji wa pamba yenye ubora unaotakiwa.
Kwa upande wake, Meneja wa
kiwanda cha Xinghua, Bw. Wang, alisema kuwa usindikaji wa ngozi unasuasua kutokana na upatikanaji hafifu wa
malighafi. Wafugaji wanapowekea alama mifugo na kutoboa ngozi wakati wa
kuchinja, wanaathiri sana ubora wa ngozi alisema meneja huyo. Katika
kukabiliana na changamoto hii, mwekezaji huyo ana mpango wa kujenga machinjio
ya kisasa ambayo pia itahusisha usindikaji wa nyama.
Aidha Bw. Sangawe alitoa rai kwa
viongozi wa mikoa inayotoa ngozi kwa wingi kuongeza jitihada za kutoa elimu kwa
wafugaji kuhusu umuhimu wa ubora wa ngozi ili kuhakikisha ngozi inayopatikana
Tanzania inakuwa na thamani ya hali ya juu.
Kaimu Meneja
Utawala Bw. Atanas William wa Kiwanda
Cha Mafuta (Jielong Holdings) akitoa maelezo kwa timu ya ukaguzi jinsi mafuta
yanavyofungashwa katika ndoo tayari kwa kwenda sokoni. Kiwanda hiki kina uwezo
wa kuzalisha lita za mafuta milioni 2.4 kwa mwezi.
Wakaguzi wa
Miradi kutoka Ofisi ya Raisi, Tume ya Mipango wakiwa na Kaimu Meneja Utawala
Bw. Atanas William wa Kiwanda Cha Mafuta
(Jielong Holdings) wakiangalia jinsi mitambo inavyomimina mafuta katika ndoo
tayari kwa kwenda sokoni.
Kaimu Meneja Utawala Bw. Atanas William wa Kiwanda Cha Mafuta (Jielong Holdings)
akimwonyesha Bw. Paul Sangawe, Naibu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango,
shehena ya mbegu za pamba zinazotumika na kiwanda katika usindikaji wa mafuta.
Afisa fedha wa
Kiwanda cha nguo Dahong Bw. Luke Li
akiwaonyesha Bw. Erasmus
Masumbuko na Bi. Angela Shayo (wachumi kutoka Tume ya Mipango) ubora wa nyuzi
za pamba zinazotengenezwa na kiwanda chake.
0 comments:
Post a Comment