Na Saidi Mkabakuli, Kigoma
Serikali
imeazimia kuendelea kuboresha miundombinu ya bandari hususan miradi
iliyoibuliwa katika Programu ya Matokeo Makubwa Sasa ikiwemo kuanza kufanya
upanuzi wa Bandari ya Kigoma na
kuendelea kuboresha miundombinu na ununuzi wa vifaa mbalimbali vya kuhudumia
shehena katika Bandari ya Kigoma ili kuweza kukidhi mahitaji yanaongeza siku
baada ya siku katika bandari hiyo.
Ahadi
hiyo imetolewa na Kiongozi wa Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka
Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri wakati walipofanya ziara
ya kukagua maendeleo ya miundombinu katika Bandari ya Kigoma.
Bibi
Mwanri alisema kuwa serikali kupitia Mamlaka ya Bandari nchini nchini ipo kwenye
mkakati wa kuiendeleza bandari hiyo ili iwe ya kiwango kizuri kwa kuhudumia
watumiaji wa wa bandari hiyo.
“Kama munavyokumbuka Serikali katika mwaka huu wa fedha ilipanga
kuiendeleza na kuboresha miundombinu ya usafiri wa majini na anga ili kuongeza
ufanisi wa sekta hizi, ambapo Bandari ya Kigoma ni mojawapo ya bandari
zilizopewa kipaumbele kwa ajili ya uendelezaji,” alisema Bibi Mwanri.
Kwa mujibu wa Bibi Mwanri, upanuzi wa bandari hiyo upo kwenye hatua za
upembuzi yakinifu kwa ajili ya kuboresha bandari ya Kigoma na kutwaa maeneo
zaidi kwa ajili ya upanuzi wa bandari hiyo.
Akitoa taarifa ya maendeleo ya Bandari hiyo, Mkuu wa Bandari hiyo Bw.
Athuman Malibamba alisema kuwa mpaka kufikia Juni 2014 hatua ya utekelezaji
iliyofikiwa ni kukamilika kwa kazi ya uthamini wa mali eneo la Kibirizi lenye
hekta 10 kwa ajili ya upanuzi wa bandari hiyo. “Pia, Mamlaka imempata Mtaalam
Mshauri (M/S Royal Haskoning H.D.V Nederland, B.V) atakaefanya kazi ya Upembuzi
Yakinifu. Aidha, kazi ya uthamini wa mali imekamilika kwa eneo la Katosho lenye
hekta 69 kwa ajili ya kujenga bandari kavu,” alisema.
Kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi katika nchi za jirani kunatoa fursa
ya kuimarisha miundombinu ya bandari ya Kigoma ili kuwa na uwezo wa kuhudumia
shehena inayoongezeka na kukuza uchumi katika mkoa na Taifa kwa ujumla. Aidha
kuanzishwa kwa Eneo Maalum la Kiuchumi, katika mkoa wa Kigoma ni kichocheo
muhimu kwa Mamlaka ya Bandari (TPA) kuimarisha huduma katika bandari ya Kigoma
na hivyo kuweza kuzitumia fursa zitakazojitokeza mara baada ya shughuli
mbalimbali za kiuchumi kuanzishwa.
Mkuu wa Bandari ya Kigoma, Bw. Athuman Malibamba (Kulia) akimkaribisha Kiongozi wa Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya
Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri (Kushoto)
mara alipofika kujionea maendeleo ya bandari hiyo.
Sehemu ya chelezo zinazotumika kwa ajili ya matengenezo ya meli na boti
katika Bandari ya Kigoma.
Mkuu wa Bandari ya Kigoma, Bw. Athuman Malibamba (Katikati mbele)
akifafanua jambo kwa Timu ya Ukaguzi wa
Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango mara walipofika
kujionea shughuli za maendeleo kiwanjani hapo.
Mratibu wa Timu ya Ukaguzi wa
Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bw. Senya Tuni
(Wapili kushoto) akiuliza jambo kwa Mkuu wa Bandari ya Kigoma, Bw.
Athuman Malibamba (Wapili kulia)
walipofanya ziara bandarini hapo.
Kiongozi wa Timu ya Ukaguzi wa
Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri
(Aliyenyanyua mkono) akionesha kufurahia jambo wakati walipofanya ziara katika
Bandari ya Kigoma.
Mkuu wa Bandari ya Kigoma, Bw. Athuman Malibamba (Wapili kulia) akifafanua
jambo kwa Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya
Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango mara walipofika kujionea
shughuli za maendeleo kiwanjani hapo.
Afisa utekelezaji wa Bandari
Kigoma, Bw. Teophil Luoga (Kulia aliyechuchumaa) akiwaonesha eneo la upanuzi wajumbe
wa timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango
mara walipofika kujionea shughuli za maendeleo kiwanjani hapo.
Boti na meli zikipandisha shehena
kwenye Bandari ya Kigoma.
PICHA ZOTE NA SAIDI MKABAKULI
0 comments:
Post a Comment