Dar es Salaam. Wakati Taifa zima likiwa katika kitendawili cha kumjua kiongozi wa nchi atakayepatikana baada ya Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu, Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema Rais ajaye anafahamika.
Akizungumza katika mahojiano maalumu jana, Jaji
Warioba alisema si kazi ngumu kwa Watanzania kumfahamu rais ajaye kwa
kuwa katika miaka 50 tangu tupate uhuru, Watanzania wanazijua sifa za
kiongozi bora.
Jaji Warioba alisema; “Tatizo la kumjua rais
afaaye tunalikwepa lakini linafahamika. Wanaotumia fedha na lugha chafu
katika kampeni na hao ndiyo wasiotakiwa.”
“Katika miaka 50 tunazijua sifa za kiongozi bora.
Hapa tunakwepa tatizo tu. Tatizo ni matumizi ya fedha na lugha chafu
katika kampeni,” alisema Jaji Warioba ambaye pia ni waziri mkuu mstaafu.
Hadi sasa wanasiasa zaidi ya 20 wakiwamo wa CCM na
upinzani wamekuwa ama wanatajwa au wameonyesha nia ya kugombea nafasi
ya urais katika uchaguzi mkuu ujao.
Ukiacha wale wanaotajwa, wanasiasa waliotangaza
nia hiyo kutoka CCM ni Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia, Januari
Makamba, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, Mbunge wa
Nzega, Hamis Kigwangala na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, huku Mbunge wa
Wawi (CUF), Hamad Rashid Mohamed akitangaza nia kupitia ADC.
Akifafanua zaidi, Jaji Warioba alisema kila mtu
anaweweseka kuhusu kiongozi anayefaa ingawa ni kazi rahisi kumjua
kutokana na ujuzi tulionao wa miaka zaidi ya 50 ya uhuru.
Kadhalika, Jaji Warioba alisema viongozi wa
Serikali hawana budi kuangalia taswira ya uchaguzi mkuu ujao kupitia
uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambao umeonekana kuwa na kasoro
zilizosababisha vurugu.
“Nchi hii ina amani na tujitahidi kuilinda amani
yetu. Katika uchaguzi huu tufanye kila tuwezalo kuweka maandalizi yenye
umakini,” alisema Warioba na kuongeza: “Nasisitiza amani. Uchaguzi wa
Serikali za Mitaa ni funzo.”
Tetesi kuwania urais
Hivi karibuni baadhi ya vyombo vya habari,
likiwamo gazeti la chama tawala, viliripoti tetesi kuwa Jaji Warioba
anaandaliwa kuwania urais kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa),
tetesi ambazo kiongozi huyo alizikanusha vikali.
Jaji Warioba alisema amelitumikia Taifa kwa muda mrefu na aling’atuka kwa mapenzi yake, hivyo hawezi kurudi tena katika siasa.
“Nimetukanwa sana, nimebezwa, nimekejeliwa kwa mambo mengi
lakini ukweli ni kuwa nilifanya uamuzi wa kung’atuka katika siasa miaka
20 iliyopita na siwezi kubadili uamuzi wangu,” alisema.
Akizungumzia baadhi ya wanasiasa kutumia jina lake
katika majukwaa na baadhi kumkashifu kwa madai kuwa alimsaliti Baba wa
Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Jaji Warioba aliwataka wanaofanya hivyo
wasitumie jina lake kusafisha njia zao katika siasa.
“Nimeitumikia nchi hii kwa miaka 30, kuanzia mwaka
1966 hadi 1995 nikang’atuka. Niliufanya uamuzi huo miaka 20 iliyopita,
nikabaki katika uongozi wa chama nako nikaachia ngazi 2002. Mjue kuwa
nilifanya hayo kwa umakini mkubwa,” alisema.
Utata Kura ya Maoni
Katika mahojiano hayo, pia Jaji Warioba
alizungumzia mchakato wa kuboresha Daftari la Wapigakura na Sheria ya
Kura ya Maoni kuwa mwingiliano wake hasa katika kipindi cha uchaguzi
utaleta mkanganyiko.
Akizungumzia mkanganyiko huo, Jaji Warioba alisema
sheria inaweka utaratibu maalumu wa mchakato wa kura ya maoni ambao
alisema hautaendana na ratiba ya uandikishwaji katika daftari hilo.
“Kwa utaratibu uliowekwa, Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC) itamaliza kazi Machi na wakati huo kura ya maoni
imepangwa kufanyika Aprili. Kwa hali hiyo hatuna uhakika kama Tume
itakamilisha kazi yake katika kipindi hicho,” alisema.
Jaji Warioba alisema Sheria Kura ya Maoni Na. 3 ya
mwaka 2014 inasema kuwa wananchi wanatakiwa kupewa elimu ya kura ya
maoni kwa kipindi cha miezi miwili na mwezi mmoja wa kampeni lakini hadi
sasa hakuna ratiba inayoeleweka, jambo ambalo linaleta mwingiliano.
“Hii ni Januari, kama watafuata sheria na kuanza
kutoa elimu kwa kipindi cha miezi miwili, ina maana itakuwa ni Aprili na
Mei, ukijumlisha mwezi mmoja wa kampeni ambao ni Juni ina maana kura
itapigwa Julai. Ikumbukwe kuwa mwezi huo mbio za uchaguzi zitakuwa
zimepamba moto,” alisema. Kura hiyo ya maoni imepangwa kufanyika Aprili
30.
Jaji Warioba alisema ni vyema kama mchakato wa
Katiba mpya ukaenda kama sheria inavyosema kwani kinyume na hapo mambo
yataharibika na pengine vurugu zinaweza kutokea katika uchaguzi mkuu.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju hakupatikana kuzungumzia utata huo wa kisheria.
Kuhusu matumizi ya BVR
Kadhalika, Jaji Warioba alisema kwa matumizi ya
teknolojia BVR katika hatua ya maboresho ya daftari la kudumu la
wapigakura, kwa uzoefu alio nao, vifaa hivyo vina utata mkubwa hivyo
unahitajika umakini mkubwa.
“Nilikwenda Malawi mwaka 2004 nikaona utaratibu wa
BVR umeleta changamoto kwa sababu tu ni teknolojia mpya. Inahitajika
elimu ya kina kabla ya matumizi yake,” alisema Jaji Warioba.
Alitoa mfano wa utata wa BVR kuwa iwapo mpigakura
atafanya udanganyifu na kujiandikisha mara mbili au zaidi (hata kama
atatumia majina tofauti), mashine itafuta majina yaliyozidi na kubaki na
taarifa zake katika kituo kimoja tu.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Damian
Lubuva alisema tume hiyo imeshazifanyia majaribio mashine hizo katika
majimbo matatu na zimeonyesha ubora na upungufu ulikuwa mdogo huku zile
zenye kasoro zikifanyiwa marekebisho.
0 comments:
Post a Comment