Dar es Salaam. Mali za Mbunge
wa Mbinga Magharibi, Kapteni John Komba zimetangazwa kupigwa mnada
kutokana na kushindwa kulipa deni analodaiwa na Benki ya CRDB.
Mali hizo zinahusisha eneo lenye ukubwa wa mita za
mraba 2,214 lililopo Mbezi Tangi Bovu, Dar es Salaam, kiwanja namba
1030 kilichosajiliwa kwa jina la John Damiano Komba na Salome Komba.
Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa kwenye vyombo
vya habari, Kampuni ya Uwakili ya Mpoki & Associates Advocates
inayoiwakilisha CRDB imetangaza kuuza eneo hilo la kibiashara
lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya mafuta, maduka makubwa,
benki, sehemu ya kufanyia mazoezi, hospitali na huduma nyingine za
kijamii.
“Tayari eneo hilo lina nyumba kubwa ya kuishi
upande unaotazamana na barabara mpya ya Bagamoyo. Kwa upande wa kusini
mwa jengo kuu linalotazama barabara hiyo kuna nyumba nyingine ya kuishi,
fremu za maduka na ofisi,” ilisomeka sehemu ya tangazo hilo.
Alipoulizwa juu ya gharama halisi anazodaiwa
Kapteni Komba na muda wa deni hilo, mmiliki wa Kampuni ya Mpoki &
Associates Advocates inayoratibu mnada huo, Mpale Mpoki alisema maelezo
yote yanayohusu kiasi cha mkopo na muda wa deni yatajibiwa na CRDB
wenyewe.
Hata hivyo, uongozi wa CRDB haukupatikana jana
kuzungumzia suala hilo na Kapteni Komba alipoulizwa alisema hakuna jambo
kama hilo... “Hakuna kitu kama hicho, waulize hao waliotoa hilo
tangazo.”
0 comments:
Post a Comment