OFISI
ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, imetoa siku nane kwa Mwenyekiti
wa Chama cha Tanzania Labour (TLP) Augustino Mrema kutoa maelezo kuhusu
tuhuma za kuendesha chama hicho kinyume na katiba.
Hayo
yalibainishwa juzi katika taarifa iliyotolewa Dar es Salaam na Naibu
Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza ambayo ilimtaka kuwasilisha
maelezo yake kabla ya Januari 23, mwaka huu ili ofisi hiyo iweze
kuyafanyia kazi na kuwajibu walalamikaji.
Kwa
mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Ukweli na Maridhiano TLP Taifa, Joram
Kinanda, pamoja na Mrema kukiuka katiba ya chama chao, pia anatuhumiwa
kuongoza chama kidikteta, kujilimbikizia madaraka na kuporomosha heshima
ya chama cha upinzani.
Kinanda
aliongeza kuwa Mwenyekiti huyo, anaendesha chama hicho kwa ukabila kitu
ambacho ni tofauti na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977
na ni tofauti na katiba ya chama chao.
Hata
hivyo katika barua yake kwa Msajili, Kinanda aliiomba ofisi hiyo
ifanyie kazi tuhuma hizo na kuruhusu Kamati ya Ukweli na Maridhiano
kutambuliwa na kupewa mamlaka ya kuongoza TLP kuelekea uchaguzi mkuu.
Pia aliomba Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa itangaze kwamba Uongozi wa Mrema umekoma.
Akifafanua
kuhusu hatua hiyo, Nyahoza alisema kwa mujibu wa kanuni ya 13 ya kanuni
za usajili wa vyama vya siasa mlalamikiwa huyo atatakiwa kuwasilisha
majibu ya tuhuma hizo kwenye ofisi yake siku iliyopangwa na sio zaidi ya
hapo.
0 comments:
Post a Comment