Kiongozi Muadhamu wa
Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, kuondolewa vikwazo ni sehemu ya
mazungumzo ya nyuklia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kundi la 5+1.
Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei amesema hayo leo mbele ya hadhara
kubwa ya wafanyaziara na majirani wa haram tukufu ya Imam Ali bin Mussa
al-Ridha (as) mjini Mash'had ambapo sambamba na kuashiria mazungumzo ya
nyuklia ya Iran na nchi za Ulaya na Marekani amebainisha kuwa, upande wa
pili unaofanya mazungumzo na Iran hususan Marekani una haja na
mazungumzo na kwamba, hitilafu zilizoko baina ya Wamarekani hazina maana
kwamba, Washington haina haja na mazungumzo haya. Kiongozi Muadhamu wa
Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, salamu za Rais Barack Obama wa
Marekani kwa mnasaba wa sikukuu ya Nouruz hazikuwa na ukweli na
kubainisha kwamba, Marekani ndiyo sababu kuu ya mashinikizo dhidi ya
taifa la Iran na imekuwa ikifanya kila iwezalo ili kulitwisha taifa hili
ubeberu wake. Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa, hakuna mtu ndani ya
Iran ambaye hataki kadhia ya nyuklia ipatiwe ufumbuzi, bali kile ambacho
taifa la Iran halikitaki ni utumiaji mabavu, ubeberu na utwishaji mambo
wa Marekani. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa,
taifa la Iran halitishwi na vikwazo wala nguvu za kijeshi kwani
limesimama kidete na liko imara. Amebainisha kwamba, katika mazungumzo
yake na kundi la 5+1, Iran haifanyi mazungumzo kuhusiana na masuala
yasiyo ya kimantiki. Aidha Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu
amesema, inachotaka Iran ni utulivu na kushikwa hatamu na wananchi
wenyewe wa mataifa ya Mashariki ya Kati, lakini siasa za Marekani ni
kuleta vurugu na machafuko.
0 comments:
Post a Comment