pagead2.googlesyndication.com pagead2.googlesyndication.com

NIMEJIUNGA RASMI NA ACT - ZITTO KABWE

Aliyekuwa mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe leo ametangaza rasmi kujiunga na Chama cha ACT Wazalendo.
Katika maelezo yake kwa waandishi wa habari jijini Dar es salaam leo, Zitto amesema kuwa amejiunga na chama hicho tangu jana Jumamosi (Machi 21, 2015) kupitia tawi la Tegeta Dar es salaam na kupewa kadi namba 71.
Amesema ameamua kujiunga na chama hicho ili kuendeleza mapambano ya demokrasia nchini kwa kuwa chama hicho ni wazalendo wa kweli.
Naye msanii wa Hip Hop nchini Seleman Msindi maarufu kwa jina la Afande Sele ametangaza kumfuata Zitto Kabwe kwa kuachana na CHADEMA na kujiunga na ACT Wazalendo.
Ifuatayo ni sehemu ya alichozungumza Zitto Kabwe mbele ya waandishi wa habari leo
 
"Nimejiunga na ACT kwa sababu ninaona kwamba huku ndiko kunakoendana na kile ambacho mimi nimekipigania kwa miaka yote tangu nianze siasa, ambacho ni kuweka mbele maslahi ya Taifa dhidi ya kitu kingine chochote. Kwa kifupi nimepigania uzalendo kwa nchi yangu na huu ndiyo msingi mama wa Chama cha ACT - Wazalendo.
Kama mnavyojua mimi ni mjamaa na ninaamini katika misingi ambayo Mwalimu Nyerere aliisimamia. ACT-Wazalendo ni chama pekee nchini kinachokubaliana na Itikadi ya ujamaa na kinaamini katika Falsafa ya Unyerere ikiwa na lengo la kuirudisha nchi katika misingi iliyoasisi taifa. Ninajiunga na ACT-Wazalendo kwa sababu ni chama kinachoamini katika msingi wa uadilifu na kimeweka miiko na maadili ya viongozi katika kuhakikisha kwamba viongozi wote wa ACT-Wazalendo wanakubaliana nayo kwa kusaini. Naamini kuwa na miiko na maadili kwa viongozi ni mwanzo wa kuhakikisha kwamba jamii yetu inaishi katika uadilifu na kwamba viongozi wanakuwa mfano wa uadilifu katika jamii. Uadilifu ni nguzo muhimu katika kujenga mfumo madhubuti wa uwajibikaji nchini kwetu.
Nimejiunga na ACT-Wazalendo kwa sababu ninakubaliana na imani yao kwamba Kujitegemea, bidii, umakini na weledi katika kazi ndiyo msingi wa maendeleo.
Hakuna namna nchi yetu na wananchi watapiga hatua ya kimaendeleo bila sisi sote kufanya kazi kwa bidii na kwa kuzingatia umakini na weledi. Ninakubaliana na ACT-Wazalendo kwamba raslimali za Taifa lazima zitumike kuondosha umaskini wa watu wetu.
Ninajiunga na ACT-Wazalendo kwa sababu ninakubaliana na imani yao kwamba Umoja ni ngao muhimu katika ujenzi wa taifa letu na Afrika kwa ujumla. Lazima tuirudishe nchi yetu katika misingi iliyoasisi taifa hili. Lazima tuirudishe nchi yetu katika heshima na uongozi wa bara hili la Afrika.
Ninaahidi kufanya kazi na vijana, wanawake, wanaume na watu wote wanaoamini katika siasa safi na siasa za hoja. Tunataka tufungue ukurasa mpya wa siasa hapa nchini. Siasa za masuala ya nchi yetu. Siasa za masuala ya vijana, wanawake, wazee, wakulima, wafanyakazi, wajasirialimali, wafanyabiashara na wote wanahangaika kuijenga nchi yetu na katika kuondoa umaskini.
Tunataka tuzungumze namna bora ya kuendesha elimu, afya, hifadhi ya jamii, na ajira. Tunataka tujenga hoja mbadala kuhusu namna endelevu ya kujenga uchumi shirikishi ambapo kila mwananchi anajisikia sehemu yake."

0 comments:

Post a Comment