Dar es Salaam. Kiongozi mkuu wa
chama chama cha ACT – Wazalendo, Zitto Kabwe jana alianika orodha ya
majina ya watu wanaotuhumiwa kuhodhi akaunti zenye mabilioni ya fedha
nje ya nchi, lakini akasita kuyataja kutokana na sababu za kisheria.
Zitto aliwapa waandishi wa habari orodha hiyo akisema waende kufanyia kazi kwa kuwahoji wahusika kulingana na taaluma yao.
Orodha hiyo ina majina yenye asili ya kiasia isipokuwa wachache ambao wanaonekana wana majina ya kibantu.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika
Uwanja wa Mwembeyanga, Temeke, Dar es Salaam, Zitto alisema: “Majina
ninayo haya hapa niwataje nisiwatajee! Ni wengi sana wengine wanamiliki
kampuni kubwa.”|
Alisema Zitto alisema wamejaribu kuishinikiza
Serikali ichukue hatua, lakini inaonekana kutotaka kufanya hivyo na
kwamba anaamini waandishi wa habari kwa kutumia taaluma yao wataweza
kuwaanika wahusika.
Wakati maofisa wa ACT wakigawa orodha ya majina
hayo, wananchi walionekana kuwa na shauku ya kupata nakala ya karatasi
hiyo yenye majina 99 ya wafanyabiashara hao maarufu ndani na nje ya
nchi, lakini kiongozi huyo hakuwa tayari kuwapatia na badala yake
akiwaambia wasome magazeti ya kesho (leo).
Zitto alisema kwamba kati ya majina ya raia hao
wenye mabilioni ya fedha nchini Uswisi, kuna wengine wanamiliki kihalali
lakini wengine wamejirundikia isivyo halali.
‘’Nimeamua leo kuiweka orodha hii wazi kama
shinikizo kwa Serikali kutoa taarifa ya uchunguzi kabla ya Bunge
kuvunjwa wiki ijayo. Kila mwandishi wa habari aliyepo kwenye mkutano huu
nimempatia nakala yenye majina 99 ya Watanzania au watu wenye uhusiano
na Tanzania ambao wana akaunti HSBC ya Uswisi. Jumla ya akiba katika
akaunti benki hii pekee ni Dola 114 milioni za Marekani,’’ alisema.
Wakati huohuo, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod
Slaa ametawazwa kuwa chifu wa mkoa na wazee wa Dar es Salaam na kuitaka
serikali kuhakikisha inawarudishia wananchi chenji zinazotokana na
ufisadi wa Escrow , EPA na Richmond. Akizungumza katika kongamano hilo
la wazee la kutafakari uchaguzi wa mwaka 2015, Dk Slaa alisema ingawa
wazee waliungana na Hayati Mwalimu Nyerere kupambana na maadui wa tatu
ambao ni ujinga, umaskini na maradhi lakini kwa sasa ameongezeka adui wa
nne ambaye ni ufisadi.
“Ujinga alioupinga Mwalimu na wazee umeondoka?
Lakini ujinga, umaskini na maradhi na kuna adui wa nne ambaye ni
ufisadi,” alisema.
Alisema hakuna Mtanzania ambaye atakwenda dukani
na Sh10,000 kununua chumvi na kibiriti halafu akaacha chenji yake dukani
kwa makusudi na hivyo Watanzania bado wanadai fedha zao zilizopotea
kutokana na ufisadi.
Kadhalika Dk Slaa alisema kitendo cha wazee hao
kukutana katika kongamano hilo kinaashiria kuwa wana kiu, njaa na
matumaini ya kutaka mabadiliko
“Mwalimu pia alipokewa na wazee wa Bagamoyo ambao walimuombea
dua, akaenda kwenye makaburi na waliunganisha nguvu kumng’oa Mwingereza
na kupata uhuru na mimi nawataka wazee wa Dar es Salaam kuongeza nguvu
kuing’oa CCM,” alisema Dk Slaa.
Alizungumzia pia uandikishaji wa Daftari la Kudumu
la Wapigakura na kuwataka wakazi wa Dar es Salaam kuwa makini na
kuhakikisha wanajiandikisha.
Awali, katika kongamano hilo, Naibu Katibu wa
Jumuiya na Taasisi za Kiislamu na Shura za Maimamu nchini Sheikh Rajab
Katimba aliizungumzia kauli ya Katibu wa Itikadi na Uenezi, wa CCM Nape
Nnauye ya kuwa CCM itashinda kwenye Uchaguzi Mkuu ujao hata kwa bao la
mkono na kusema ni ya kichochezi.
“Wakati nchi inajitahidi kuwa na amani na kuwa na
uchaguzi wa haki na huru, kiongozi wa chama anazungumza uchochezi mkubwa
ambao kama viongozi wengine wangeusema sidhani kama wangekuwa salama,”
alisema.
Sheikh Katimba aliwaasa Ukawa kuwa na umoja na
kuwataka wawaite wazee ili wawape ushauri badala ya kulumbana kwani huu
si wakati mwafaka wa kuwa na migogoro.
0 comments:
Post a Comment