Baadhi ya Wasichana hao katika picha ya pamoja |
Serikali ya Tanzania imesema kuwa,
itawarudisha nchini mamia ya wasichana raia wa nchi hiyo waliokwama
nchini India na mataifa mengine baada ya taasisi zilizowachukua kwenda
kuwatafutia ajira, kukiuka mikataba yao na kuwalazimisha kufanya kazi
tofauti ikiwemo ya ukahaba.
Hayo yalisemwa jana na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Mindi Kasiga wakati akizungumzia
matatizo wanayoyapata Watanzania wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi.
Kwa mujibu wa Kasiga, kati ya mwezi Machi hadi Mei mwaka huu, balozi za
Tanzania nchini India, Malaysia na nchi kadhaa za Mashariki ya kati,
zilipokea maombi ya kutaka kusaidia kuwarejesha nyumbani raia wa nchi
hiyo ambao walipelekwa katika nchi hizo kwa ahadi za kupatiwa ajira
ambazo hutolewa na watu wasio waaminifu ambao wengi wao wanashukiwa
kujihusisha na mtandao wa magendo ya biashara za binadamu. Aliongeza
kuwa, mtandao huo umekuwa ukiwatafuta wasichana wenye umri kati ya miaka
18 hadi 24 au chini ya umri huo na kuwalaghai kuwa kuna fursa za ajira
katika hoteli, migahawa, maduka makubwa au kazi za nyumbani katika nchi
za nje ambapo baada ya hapo huwawezesha kupata hati za kusafiria na
tiketi za ndege kwa ajili ya kusafiri kwenda nchi husika. Hata hivyo
alikiri kuwa, wasichana wengi huwa wanafahamu mapema kuhusu kazi
wanayoenda kuifanya huko ughaibuni na kwamba ugumu wa maisha ndio huwa
unawasukuma na kujikuta wanaingia kwenye matatizo makubwa.
0 comments:
Post a Comment