STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 28 Februari, 2014
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein
amesema Serikali na wananchi wa Zanzibar wanajivunia uhusiano mzuri
uliopo kati yao na Serikali na wananchi wa Marekani.
Akizungumza
na ujumbe kutoka jiji laVellejo katika Jimbo la Califonia nchini
Marekani ulioongozwa na Meya wa jiji hilo Mstahiki Osby Davis, Ikulu leo
Dk. Shein alisema mbali ya kujivunia, Zanzibar inathamini na
kuridhishwa na uhusiano huo ambao umejengwa na historia inayowaunganisha
watu wa Zanzibar na wa Marekani kwa karne nyingi.
“Tangu
tulipoanzisha uhusiano kati yetu katika ngazi ya ukonseli mwaka 1845
tumejenga historia ya urafiki wa kweli kati ya serikali zetu na watu
wake na ndio maana hadi leo uhusiano wetu umekuwa mzuri huku sote tukiwa
na ari ya kuuimarisha kwa faida yetu sote” Dk. Shein alisema.
Aliielezea
ziara ya ujumbe huo kutoka jiji la Vallejo kuwa sio tu ni muhimu katika
kuwaunganisha wananchi wa Marekani na wenzao wa Zanzibar bali ni
uthibitisho wa urafiki uliopo kati ya Zanzibar na Marekani.
“Tumekuwa
watu wa kutembeleana na kusaidiana kwa miongo mingi. Vijana wengi wa
Zanzibar wamekaribishwa nchini Marekani na wengine wamepata fursa za
masomo na kuishi huko bila vikwazo” Dk. Shein alieleza na kuongeza kuwa
ndio maana Zanzibar ingependa kuona kila siku uhusiano wake na Marekeni
unaimarika.
Alibainisha
kuwa kutokana na uhusiano mzuri huo Zanzibar ambayo ni sehemu ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikipokea misaada mbalimbali
ambayo imekuwa chachu katika kuimarisha maendeleo humu nchini.
Miongoni
mwa misaada hiyo aliueleza ujumbe huo ni ujenzi wa barabara huko Mkoa
wa Kaskazini Pemba ambazo zimejengwa kwa msaada wa watu wa Marekani
kupitia Mfuko wa Changamoto za Milenia na zinatarajiwa kuzinduliwa hivi
karibuni
Aliongeza
kuwa Serikali na wananchi wa Zanzibar wamefurahishwa na uamuzi wa
Serikali na watu wa Marekani kwa kuwajumuisha tena katika awamu ya pili
na Utekelezaji wa Miradi ya Mfuko wa Changamoto za Milenia uamuzi ambao
unaonesha kuwa Marekani na Zanzibar ni marafiki wa kweli.
Kwa
hiyo Dk. Shein aliuthibitishia ujumbe huo dhamira ya kweli ya Serikali
na wananchi wa Zanzibar ya kuendeleza na kuuenzi uhusiano wake na
Marekani.
“Tuna
malengo yanayofanana na dhamira yetu ni moja hivyo kuimarisha uhusiano
wetu ndio nia yetu na ni wajibu wetu” Dk. Shein alisisitiza.
Aliutaka
ujumbe huo ambao utafanya mazungumzo na wadau mbalimbali katika sekta
binafsi hususan sekta ya utalii kuangalia namna ya kushirikiana na
Zanzibar katika kuendeeza utalii kati ya Zanzibar na Jimbo la Califonia
na Marekani kwa ujumla.
“Ningependa
kusisitiza ushirikiano katika sekta ya Utalii ambayo naamini nyinyi mna
uzoefu mkubwa na maarifa hivyo sio tu kuwa tunaweza kubadilishana
uzoefu lakini pia kuhimiza uwekezaji kutoka jimbo hilo kuja
Zanzibar”alieleza Dk. Shein.
Kwa
hiyo alimueleza Mstahiki Meya huyo kuwa ziara hiyo imefungua ukurasa
mpya katika kuendeleza na kuimarisha ushirikiano kati ya watu wa
Zanzibar na watu wa jimbo la Califonia na Marekani kwa ujumla.
Kwa
upande wake Mstahiki Meya wa Vallejo Bwana Osby Davis alisema kufika
kwao Zanzibar wanajiona wamefika nyumbani na kumshukuru Mheshimiwa Rais
kwa kumpa fursa yeye na ujumbe wake kuonana naye.
“Ni fahari na heshima kubwa kwetu kupata fursa ya kuonana nawe Mhe Rais wa
Zanzibar na pia kuonana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe
Kikwete na kufanya mazungumzo na ujumbe wangu” Alieleza Mstahiki Meya
Davis akionyesha furaha.
Amesema kuwa ziara yake hiyo ndio ni mwanzo wa ziara nyingi kama hizo kutembelea Zanzibar na Tanzania kwa jumla.
“Sisi
wananchi wa Marekani wenye asili ya Afrika tunajivunia kutambua asili
yetu na ndio maana tumeanzisha juhudi kuimarisha uhusiano na asili
yetu”alieleza Mstahiki Meya Davis.
Alibainisha
kuwa kusema hivyo sio kwamba wao si wa Marekani lakini ni ukweli kuwa
watu wa Marekani wana asili zao wengine wanatoka Japan, wengine
Ujerumani, wengine wa China na kadhalika hivyo wao Afrika ndio kwao na
wanajivunia kujitambua hivyo na kusisitiza kuwa huo ni ukweli wa
kihistoria.
0 comments:
Post a Comment