BARAZA
la Sanaa la Taifa (Basata), limeitaka Kamati ya Miss Tanzania
kutohusisha burudani zinazokiuka maadili ya Mtanzania wakati wa
mashindano yao mwaka huu.
Akizungumza wakati wa kikao cha tathmini ya mashindano ya Miss
Tanzania 2013 kilichofanyika kwenye ukumbi wa baraza hilo, Dar es Salaam
jana, Mkurugenzi wa Idaya ya Ukuzaji Sanaa Basata, Vivian Shalua,
alisema kuwa, maadili ni muhimu kuzingatiwa katika mashindano hayo ili
kuepukana na dhana potofu kuwa, yanahusiana na uhuni.
“Maadili yazingatiwe katika mashindano ya mwaka huu, kuanzia kwa
washiriki hadi burudani zitakazohusishwa, kama ‘vigodoro’, ‘kanga moja
mbendembende’ na nasikia siku hizi kuna ‘tisheti ndembendembe’,” alisema
mkurugenzi huyo.
Alisema kuwa, Basata ipo tayari kuyapigania mashindano ya Miss
Tanzania kuhakikisha yanakuwa katika ubora wa hali ya juu, kwa
kushirikiana na Kampuni ya Lino International Agency ambao ndio
waandaaji.
Mkurugenzi huyo pia aliitaka Lino kuwaelimisha mawakala wanaoandaa
mashindano hayo juu ya umuhimu wa kuwa na vibali kutoka Basata, ikiwa ni
pamoja na kutowavumilia watovu wa nidhamu bila kujali ukongwe wao
katika tasnia hiyo.
Kwa upande wake, Ofisa Sanaa Kitengo cha Matukio, Kurwijira Maregesi,
aliitaka Lino kujipanga kujiweka tayari kufanya mashindano hata pale
inapokosa mdhamini, huku mjumbe mwingine katika kikao hicho, ambaye ni
Ofisa Sanaa Basata, Philemon Mwasanga, akisisitiza mawakala kuwekeana
mikataba na warembo kabla ya mashindano kuanza.
“Lino isiwafumbie macho mawakala wasiojali mikataba na warembo, na
warembo waisome na kuielewa ili kuepusha migogoro inayoweza kutokea,”
alisema.
Akijibu hoja kadhaa zilizoibuliwa katika kikao hicho, Mkurugenzi wa
Lino International Agency, Hashimu Lundenga, alisema kuwa, wamejipanga
ili kuweza kufanya mashindano yao bila kutegemea wadhamini, huku
akiitaka Basata kuwasaidia katika hilo.
“Tatizo mashindano yetu gharama yake ni kubwa sana, nasi hatupendi
kuona ubora wake ukishuka kutokana na kushindwa kumudu gharama, ndio
maana tumekuwa tukihangaika kuomba udhamini kutoka katika makampuni
mbalimbali makubwa hapa nchini,” alisema.
Juu ya mikataba baina ya warembo na mawakala, Lundenga alisema:
“Mwaka huu tumesisitiza mawakala waingie mikataba na washiriki kabla ya
mashindano na tutakuwa makini katika kufuatilia hilo na changamoto
nyinginezo zilizoibuliwa katika kikao hiki.”
Mmoja wa warembo walioshiriki mashindano ya mwaka jana ambaye ni Miss
Sinza 2013, Prisca Clement, alisema kuwa, kuna umuhimu wa kuongezwa kwa
zawadi katika ngazi za chini ili kumwezesha mshiriki kujivunia na
kujitosa kwake katika mashindano hayo bila kujali kama ameshinda au la.
Mashindano ya Miss Tanzania 2014 yamezinduliwa mapema wiki hii,
ambapo fainali zake zinatarajiwa kuwa kati ya Septemba na Novemba mwaka
huu chini ya udhamini wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia kinywaji
chake cha Redd’s Original
Tanzania daima
0 comments:
Post a Comment