Na
Khamis Malik,
IMEELEZWA
asilimia 25 ya wanawake wanafanya mapenzi kinyume cha maumbile ama na waume zao
au na wanaume wengine kama njia ya kukimbia
kupata ujauzito na mambo mengine.
Takwimu
hizo zimetolewa na Katibu wa Jumuiya ya Maimamu Zanzibar kutoka wilaya ya
magharibi, Sheikh Nassor Hamad Omar, wakati akiwasilisha ripoti ya awali ya utafiti
wa kamati ya kupambana na vitendo vya liwati katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa
Kusini Unguja Tunguu, kwenye kongamano la vijana kuhusu udhalilishaji wa
kijinsia na mimba za mapema.
Alisema
takwimu hizo zimekusanywa kutokana na utafiti uliofanywa na Jumuiya ya Maimamu
(JUMAZA) katika maeneo mbali mbali ya Zanzibar.
Alisema
sababu ya kufanya hivyo, ama wanawake hao wanaogopa kupata ujauzito hasa wale
ambao bado hawajaolewa lakini wako kwenye mahusiano na hata wale walioko kwenye
ndoa.
Aidha
alisema utafiti huo umegundua watoto wengi wenye umri wa kuanzia miaka tisa
hadi 20, wanaingizwa katika vitendo viovu ikiwemo liwati na usagaji.
Alizitaja
sababu kubwa zinazopelekea kuenea kwa uovu huo kuwa ni pamoja na tamaa,
matumizi mabaya ya utandawazi, imani za kishirikina kwa kupiga ngoma kama vile
vibuki, kupenda kuiga tabia mbaya na watalii wakorofi.
Alisema kutokana na tatizo hilo, kamati yake imefanya
utafiti wa tatizo hilo na kutoa elimu kwa taasisi mbalimbali ambapo nyengine
zimekubali kushirikiana nao bega kwa bega ili kuondoa tatizo hilo.
Alisema
Jumuiya imeandaa kitabu ambacho kimeandikwa kwa kuzingatia zaidi misingi ya
dini mbili za Kiislamu na Ukiristo.
Aidha,
alisema wamefanikiwa kuvitembelea vyuo vya Quran na taasisi nyengine na
kukutana na walimu, wanafunzi, wazazi na walezi ili kufikisha ujumbe na taarifa
za utafiti huo.
Akizungumza
kwa huzuni kubwa Shekhe huyo alisema inasikitisha kuona vijana wa kizanzibari
wanafanya liwati huku wengine wakishangiria na kuchukua picha.
Nao
vijana walioshiriki kongamano hilo, wakichangia ripoti hiyo, wamekiri kuwa
vitendo vya liwati vipo na ni maarufu na vinafanywa kwa wingi hata maeneo ya vijijini.
“Vyombo vya habari vinapaswa kutumiwa
kikamilifu kutambulisha na kutangaza uchafu huu unaotia doa jamii ya
Kizanzibari na taifa letu” alisikika mmoja wa vijana hao akizungumza kwa
masikitiko.
Washiriki
hao walisema kuwa sheria zilizopo sasa zinatoa mwanya kwa wahusika kutotiwa
hatiani na kutoa nafasi ya kuendelea kufanya makosa.
Walisema
serikali kwa asilimia kubwa inapaswa kuwajibika na ni lazima iweke mikakati
imara ya kutunga sheria ya kudhibiti suala hilo.
Aidha,
waliahidi kuvitumia vikundi vyao
kuelimisha juu ya mapambano hayo na kwamba watazitumia maskani zao
kulizungumzia tatizo hilo
kwa uwazi.
Kongamano kama hilo linatarajiwa kuendelea katika mkoa wa mjini magharibi.
0 comments:
Post a Comment