pagead2.googlesyndication.com pagead2.googlesyndication.com

Baba, mama, mtoto wafa ajalini

Singida na Same. Familia inayowajumuisha baba, mama na mtoto ni miongoni mwa abiria 25 walipoteza maisha katika ajali za barabarani zilizotokea katika mikoa ya Singida, Lindi na Kilimanjaro.
Omari Shaban (44), mke wake Salma Omari na mtoto wao Nyamumwi Omari (10) wakazi wa Itigi, Singida, walifariki dunia baada ya gari walilokuwa wakisafiria aina ya Noah kugongwa na lori aina ya Scania katika ajali iliyosababisha vifo vya watu 13 mkoani humo.
Ajali hiyo ilitokea saa 1:32 asubuhi katika Kijiji cha Isuna, Wilaya ya Ikungi, Barabara Kuu ya Singida-Dodoma, ambapo watu watatu walinusurika na kupata majeraha madogo madogo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida, Geofrey Kamwela alisema Noah lilikuwa likitoka Itigi, wilayani Manyoni kwenda Singida Mjini na kwamba miili ya watu 10 walikuwa wameshatambuliwa na ndugu zao hadi jana mchana.
Alisema magari hayo yalikuwa yakipishana, lakini ghafla lori lilihama upande wake na kulifuata Noah upande wa kushoto mwa barabara, ambako lililigonga, kisha kuliburuza.
“Kwa sasa bado hatujajua chanzo cha ajali hiyo mbaya ingawa baadhi ya watu wanadai kuwa huenda dereva wa lori alisinzia na kusababisha lori hilo kuhama upande wake na kulifuata Noah. Uchuguzi utakapokamilika, tutatoa taarifa,” alisema Kamwela.
Aliwataja wengine waliofariki katika ajali hiyo kuwa ni Mkazi wa Msisi, Haji Mohammed (29), Wakazi wa Sajaranda; Mtunku Rashidi (68), Salehe Hamisi (28), Athumani Kalemba (38) na Ramadhan Mkenga, Mkazi wa Puma, Samir Shaban (20) na Mwaleki Nkuwi (35) ambaye ni mkazi wa Ikungi.
Miili ya abiria hao pamoja na watatu ambao walikuwa hawajatambuliwa, imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Mkoa wa Singida.
Mganga mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk Banuba Deogratius amekiri kupokea miili ya watu 13 na kwamba kati yao, watoto ni wawili.
JK atuma salamu
Rais Jakaya Kikwete ametuma salamu za pole kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida, Perseko Kone kutokana na vifo vilivyotokea katika ajali hiyo.
“Nimeshtushwa, nimesikitishwa na kuhuzunishwa mno na taarifa za vifo vya watu 13 akiwemo mtoto wa miezi minne,” alisema Rais Kikwete katika taarifa iliyotolewa na Ikulu jana.

Rais alisema inasikitisha pale makosa ya kibinadamu katika uendeshaji wa vyombo vya moto yanapoendelea kusababisha ajali ambazo zimekuwa chanzo cha kupoteza maisha ya watu wasio na hatia wakiwamo watoto, kusababisha ulemavu wa kudumu na uharibifu wa mali.
“Kupitia kwako (mkuu wa mkoa), naomba unifikishie salamu zangu za rambirambi na pole nyingi kwa familia zote zilizopoteza wapendwa wao katika ajali hiyo. Nawaomba wanafamilia wawe na moyo wa uvumilivu, subira na ujasiri hivi sasa wanapougulia machungu ya kupotelewa na ndugu zao,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Ajali Same
Katika tukio jingine, watu watatu wamepoteza maisha na wengine zaidi ya 30 kujeruhiwa vibaya baada ya gari walilokuwa wakisafiria kuacha njia na kupinduka katika Kijiji cha Mkwini, Barabara Kuu ya Same – Mombo wilayani Same mkoani Kilimanjaro.
Gari hilo la Kampuni ya Hood lililokuwa likitokea Iringa kuelekea Arusha lilianguka kati ya Makanya na Hedaru na kusababisha vifo vya watu wawili papo hapo na mmoja alipoteza maisha akiwa njiani akipelekwa hospitalini.
Mkuu wa Wilaya ya Same, Herman Kapufi alisema ajali hiyo ilitokea juzi saa 11:45 jioni ikihusisha Basi la Hood lililokuwa likiendeshwa na Baraka Juma ambaye alikimbia baada ya ajali hiyo kutokea.
“Nilifika katika eneo la ajali, dakika 10 baada ya gari kuanguka na tuliwatoa majeruhi 30 na wanaume wawili walikuwa wamekufa papo hapo na tulipofika Hospitali ya Same alifariki majeruhi mwingine na hivyo kufanya idadi ya waliokufa kufikia watatu,” alisema Kapufi.
Alisema majeruhi 25 wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Same wakati majeruhi watatu walipelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC kutokana na hali zao kuwa mbaya na kwamba miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Same.
Kapufi alisema abiria walionusurika walisema kuwa chanzo cha ajali hiyo kinaweza kuwa ni uchovu wa dereva, kwani basi halikuwa kwenye mwendo kasi bali alionekana akiwa kwenye hali ya kusinzia.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Same, Dk Ernest Kyungu alikiri kupokea majeruhi 30 na miili ya watu watatu ambao walipoteza maisha na majeruhi watatu ambao hali zao ni mbaya walipelekwa Hospitali ya Rufaa ya KCMC.
Mwanachi

0 comments:

Post a Comment