Rais ametoa msamaha huo kwa mujibu wa madaraka aliyopewa katika Ibara ya 45 ya Katiba ya nchiDar es Salaam. Rais Jakaya
Kikwete ametoa msamaha kwa wafungwa 3,967 katika magereza mbalimbali
nchini lakini msahama huo unawaweka kando waliofungwa kwa makosa ya
ujangili.Msamaha huo ambao ni sehemu ya maadhimisho ya
miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, pia hautawahusu wafungwa
waliohukumiwa kunyongwa, waliohukumiwa na adhabu hiyo ikabadilishwa
kuwa kifungo cha maisha, wanaotumikia kifungo cha maisha na wenye makosa
ya biashara ya dawa za kulevya.
Katika taarifa iliyotolewa jana na Waziri wa Mambo
ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe alisema Rais ametoa msamaha huo kwa
kutumia madaraka aliyopewa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano, ibara 45,
kifungu cha 1(d).
“Wengine ambao hawahusiki na msahama huo ni
wafungwa waliopatikana na makosa ya kupokea au kutoa rushwa na
wanyang’anyi wa kutumia silaha,” alisema alisema Chikawe.
Wengine ambao hawakupewa msamaha ni waliopatikana
na makosa ya kunajisi, kubaka na kulawiti, waliohukumiwa kwa kuwapa
mimba wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ambao walitenda kosa
hilo wakiwa na miaka 18 na kuendelea na wezi wa magari wa kutumia
silaha.
Pia wamo waliowahi kutoroka au kujaribu kutoroka
wakiwa chini ya ulinzi magerezani, waliowahi kupata msamaha wa Rais na
ambao bado wapo magerezani kutumikia sehemu ya kifungo kilichobaki na
wafungwa wa makosa ya biashara haramu ya kusafirisha binadamu na
wabadhirifu wa fedha za Serikali.
Wanaonufaika
Chikawe alisema wafungwa watakaonufaika na msamaha
huo ni wagonjwa wa Ukimwi, kifua kikuu na saratani pamoja na wazee
wenye umri wa miaka 70 au zaidi.
“Wafungwa waliosamehewa ambao ni wagonjwa na
wazee wamethibitishwa na jopo la waganga lililo chini ya uenyekiti wa
waganga wakuu wa mikoa na wilaya,” alisema Chikawe.
Alisema wengine walionufaika na msahama huo ni
wanawake walioingia magerezani wakiwa na mimba na watoto wanaonyonya na
wasionyonya, wenye ulemavu wa mwili na akili ambao wamethibitishwa na
jopo la waganga katika mikoa na wilaya.
Chikawe alisema wafungwa wote waliopata misamaha ya kupunguziwa adhabu, wataendelea kutumikia kifungo kwa miaka iliyobaki.
“Ni mategemeo ya Serikali wafungwa walioachiliwa
huru watarejea katika jamii na kushirikiana na wananchi wenzao katika
ujenzi wa taifa na kwamba watajiepusha kutenda makosa ili wasirejee tena
magerezani,” alisema Chikawe.
0 comments:
Post a Comment